Dar es Salaam. Jamhuri ya Watu wa China iliadhimisha miaka 76 tangu kuanzishwa kwake rasmi mwaka 1949, hafla iliyofanyika Jumatatu, Septemba 29, 2025 katika Ubalozi wa China jijini Dar es Salaam.
Shamrashamra hizo zilihudhuriwa na viongozi wa serikali, raia wa China pamoja na Watanzania kutoka sekta mbalimbali.
Tukio hilo lililoandaliwa na Ubalozi wa China nchini Tanzania liliashiria urafiki na mshikamano uliodumu kwa miongo kadhaa kati ya mataifa haya mawili, urafiki ambao umeendelea kuimarika na kutoa matokeo chanya ya kiuchumi, kijamii na kidiplomasia.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa China nchini, Chen Mingjian alisema taifa hilo limekuwa nguzo muhimu ya biashara na uchumi duniani huku uhusiano wake na Afrika ukiendelea kukua kwa kasi.
“China imekuwa taifa imara katika biashara za kimataifa likiwa na idadi kubwa zaidi ya watu duniani ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi. Kwa mwaka jana pekee, mchango wa China kwa Afrika ulifikia zaidi ya Shilingi bilioni 780 na Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi zinazofaidika moja kwa moja na uhusiano huo,” alisema.
Balozi Chen aliongeza kuwa mchango wa China haujajikita tu katika biashara bali pia katika kulinda haki za binadamu na kuimarisha mshikamano wa kimataifa.
Alibainisha kuwa chini ya uongozi wa Rais Xi Jinping, taifa hilo limekuwa mstari wa mbele kupigania utu, usawa na utawala bora duniani, huku uhusiano wake na Tanzania ukiwa mfano bora wa urafiki wenye matunda.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabiti Kombo, alisema Tanzania inauona uhusiano huo kama sehemu muhimu ya kufanikisha dira ya Taifa ya mwaka 2050 na katika kuboresha maisha ya wananchi.
“Mahusiano ya Tanzania na China yamevuka hatua ya urafiki wa kawaida. Licha ya umbali wa kijiografia, tumekuwa pamoja katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo Tehama na kilimo. Tunawakaribisha wawekezaji wa China kuendelea kuwekeza kupitia fursa tulizonazo, hususan bandari na mtandao wa reli za kisasa,” alisema.
Waziri Kombo pia alisisitiza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo ya kuimarisha uzalishaji wa soya, bidhaa yenye soko kubwa nchini China.
“Najua ndugu zetu Wachina mnakula sana soya. Niwahakikishie kuwa Tanzania itatosheleza mahitaji hayo, kwani Rais ameshaagiza Waziri wa Kilimo kuhakikisha zao hili linapewa kipaumbele,” alisema.
Aidha, sherehe hizo zilitoa nafasi ya kutazama historia ya taifa hilo. Oktoba Mosi, 1949 baada ya vita vya muda mrefu kati ya Chama cha Kikomunisti cha China (CCP) na Chama cha Kitaifa cha Kuomintang (KMT), Mao Zedong alitangaza rasmi kuundwa kwa Jamhuri ya Watu wa China katika Uwanja wa Tiananmen, Beijing. Ushindi huo uliwezeshwa na uungwaji mkono wa wakulima na mikakati madhubuti ya kijeshi. Serikali ya Chiang Kai-shek na wafuasi wake walikimbilia Taiwan, na hivyo kuzaliwa kwa China mpya chini ya utawala wa kikomunisti.
Miaka 76 baadaye, taifa hilo limejidhihirisha kama moja ya nguvu kuu duniani, huku mchango wake barani Afrika ukiendelea kupanuka. Waziri Kombo alibainisha kuwa mwaka uliopita peke yake, mchango wa China kwa Tanzania ulifikia Sh23.3 trilioni.
Aliongeza kuwa Tanzania inanufaika na uhusiano huo kwa ajira, uwekezaji na ukuaji wa uchumi. Aliitaja kilimo cha uyoga kama fursa mpya, akisema Tanzania inaweza kujifunza kutoka China kwa kuanzisha uzalishaji wake katika mashamba ya mkonge yaliyopo kwa wingi nchini.
Kwa upande wake, Balozi Chen alisema uwekezaji wa Wachina umechangia kwa kiasi kikubwa katika viwanda, Tehama, ajira kwa vijana na miradi ya ujenzi wa miundombinu. Aidha, ushirikiano huo umeenea kwenye sekta za afya na elimu, Tanzania imekuwa ikipokea madaktari kutoka China na vijana wa Kitanzania kupata elimu ya juu nchini humo.
Waziri Kombo aliongeza kuwa miradi ya reli ya kisasa (SGR), uboreshaji wa bandari na sekta ya Tehama ni nyanja muhimu zinazothibitisha mchango wa China katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Alisisitiza pia nafasi ya taifa hilo katika kuunga mkono bara la Afrika kupata nafasi kubwa zaidi ndani ya Umoja wa Mataifa.
Kwa ujumla, maadhimisho ya miaka 76 ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China hayakuwa sherehe za kawaida pekee, bali pia ni ukumbusho wa historia ya urafiki uliojengwa enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na kuendelea kuzaa matunda yanayogusa maisha ya wananchi.
“China na Tanzania si marafiki wa maneno bali wa vitendo. Mahusiano haya yamekuwa nguzo ya maendeleo kwa pande zote mbili,” alisema Balozi Chen.
Kwa Tanzania, China imekuwa zaidi ya mshirika wa biashara; ni rafiki wa maendeleo ambaye mchango wake unaonekana wazi kuanzia kilimo na viwanda hadi elimu na afya.
Kadri dunia inavyobadilika, urafiki huu unaendelea kuimarika, ukiwa mfano bora wa mshikamano kati ya taifa kubwa la Afrika na taifa kubwa zaidi duniani.