Songwe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limethibitisha kutokea kwa ajali mbili mfululizo zilizopoteza maisha ya watu wanne na kujeruhi watano, baada ya magari mawili kugonga tela la Lori lililokuwa limeharibika na kuegeshwa barabarani.
Ajali hizo zilitokea Septemba 29, 2025 saa 5 usiku katika eneo la Hanseketwa, Kata ya Ihanda, Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga amesema ajali ya kwanza ilihusisha gari dogo aina ya Toyota IST, lililokuwa likiendeshwa na Musa Elton (38), fundi ujenzi mkazi wa Tunduma, ambalo liligonga nyuma ya tela la lori aina ya Scania.
Kamanda Senga amesema katika ajali hiyo, abiria wawili walifariki dunia papo hapo ambao ni Queen Sampamba (36) na Berdon Mgalla (42), wote wakazi wa Tunduma.
Ameongeza kuwa, dereva Njowela amepata majeraha mabaya na amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi.
Kamanda Senga ameeleza kuwa dakika chache baadaye, gari jingine aina ya Toyota Surf, lililokuwa likiendeshwa na Abdul Mwakapesa (50), nalo liligonga tela hilohilo.
“Ajali hiyo ya pili ilisababisha vifo vya watu wawili ambao ni Emmanuel Mwangemile (55), mfanyabiashara, na Emmanuel Kandonga (50), Ofisa elimu Kata ya Mpemba, Halmashauri ya Mji Tunduma, wilayani Momba,” amesema Kamanda Senga.
Aidha, watu watano walijeruhiwa katika ajali hizo, ambao ni Winfrida Mwandule (30),Merisenti Kimpa (41), Suzie Mwakabonga (28) na Elisha Sindwani (30), pamoja na dereva wa IST,Njowela (38), wote wakazi wa Mpemba.
Kamanda Senga amesema ukiacha dereva wa IST ambaye amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi, majeruhi wengine wote wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe.
Hata hivyo, Kamanda Senga amesema dereva wa Toyota Surf, Abdul Mwakapesa, alitoroka baada ya ajali na polisi wanaendelea kumsaka ili afikishwe mbele ya sheria.