Viongozi watano Chadema Mwanza wakamatwa, sababu zatajwa

Mwanza. ‎Makada watano wa Chama cha Demokrasia  na Maendeleo (Chadema) wamekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa tuhuma za kuchana mabango ya wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

‎Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema  makada hao walikamatwa Septemba 30, 2025 saa 8:00 mchana katika maeneo tofauti jijini Mwanza‎, wakiendelea kuratibu mipango ya kuharibu mabango ya wagombea wa CCM.

Akizungumza leo Oktoba ‎Mosi, 2025 na waandishi wa habari, Mutafungwa amewataja waliokamatwa ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Nyamagana, Charles Chinchibela (50).

Wengine ni Mwenyekiti Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) Wilaya ya Nyamagana, Marko Christian (30), Enock Mpaka (55) ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho kata ya Igogo, Salum Libaba (33) ambaye ni Katibu wa Chadema kata ya Mabatini, na Mwenyekiti wa chama hicho kata ya Igoma, Dioniz Leons (33).

‎”Tumewakamata na tunaendelea kuwahoji viongozi watano wa Chadema ngazi ya wilaya kwa tuhuma ya kuharibu mabango ya wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa nafasi ya urais, ubunge na udiwani, yaliyowekwa sehemu mbalimbali za Jiji la Mwanza,” amesema Mutafungwa.

Kufuatia tukio hilo, Mutafungwa amewataka viongozi wa vyama vya siasa, mashabiki, wafuasi na wanachama kuendelea kuheshimu sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) ili kudumisha amani.

“Aidha, tumeendelea kuimarisha usalama likishirikiana na vyombo vingine vya usalama na wananchi kiasi kwamba kampeni hadi sasa zinafanyika salama, hivyo, watu waendelee kujitokeza katika mikutano mbalimbali ya kampeni bila hofu ya aina yoyote,” amesema Mutafungwa.

‎Akizungumzia sakata hilo, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi amekiri kukamatwa kwa makada hao huku akidai waliokamatwa mpaka sasa ni zaidi ya idadi inayotajwa na polisi wakiwemo waliokwenda kuwaona viongozi hao.

“Wamekamatwa wakiwa wanaenda kutoa huduma za kijamii na mpaka sasa hivi kama chama hatujaelezwa sababu ya kukamatwa kwao, na idadi ya waliokamatwa inafikia 16 kwa sababu hata waliokwenda kufuatilia na kuwaona kituoni nao wamewekwa ndani,” amesema Obadi.