Siku kumi na nne kumbeba Maximo KMC FC

KOCHA Mkuu wa KMC, Marcio Maximo amesema atatumia wiki mbili za mapumziko kusawazisha upungufu uliopo kwenye kikosi cha timu hiyo kabla ya kurudi Oktoba 18 wakiikaribisha Mbeya City.

Ligi Kuu Bara inatarajia kusimama kwa wiki mbili kupisha kalenda ya Fifa kwa timu za taifa, huku timu hiyo ikirudi mapumziko ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi mbili na kushinda moja kati ya tatu ilizocheza.

Akizungumza na tovuti ya Mwanaspoti, Maximo amesema hawatakuwa na muda mrefu wa kupumzika zaidi na watatumia wiki hizo mbili kujenga kikosi ili watakapolejea waweze kuwa na timu iliyokamilika.

“Kumekuwa na makosa mechi kwenye mechi tatu tulizocheza. Hatuwezi tukapeana mapumziko ni lazima tutumie muda huu wa mapumziko kusawazisha makosa na kuimarisha timu ili ligi itakaporudi tuwe tayari kwa ushindani,” amesema.

“Nafikiri kila mchezaji anatambua umuhimu wa kutumia kipindi hiki kusahihisha makosa ili kuiweka timu kwenye nafasi nzuri ya kufanya vizuri baada ya kufanya makosa mechi mbili mfululizo.”

MAXI 01


Maximo amesema bado ataendelea kutafuta muunganiko mzuri na kuboresha kikosi chake alichokitaja kuwa kina wachezaji wengi vijana ambao wanafundishika na kubadilika siku hadi siku.

“Najivunia kujenga timu ya vijana ambao tumaini langu kubwa ni kuendelea kuwajenga siku hadi siku ili waweze kuendana na mahitaji yangu. Hili linawezekana kutokana na umri wao,” alisema.

Mechi ya kwanza katika ligi KMC ilicheza uwanja wa nyumbani dhidi ya Dodoma Jiji na kuibuka na ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Singida Black Stars ilikubali kichapo cha bao 1-0 na pia ilifungwa dhidi ya Tanzania Prisons ugenini mabao 1-0.