Baba mdogo adaiwa kubaka, kulawiti na kumuua mtoto wa miaka minane

Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Emmanuel Kirangi (30) kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wa kaka yake, Winfrida Kafumbo (8) mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Hamkoko wilayani Ukerewe.

Mtuhumiwa huyo ambaye ni mkazi wa kijiji hicho  anadaiwa kumuua kwa kumnyonga shingo binti huyo baada ya kumbaka na kumlawiti.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema tukio hilo limetokea Septemba 30, 2025 saa 9:45 usiku katika Kijiji cha Muluseni kata ya Ngoma wilayani Ukerewe.

Mutafungwa ameyasema hayo leo Oktoba Mosi, 2025 katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Mwanza.

Ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea wakati mtoto huyo akiwa amelala na wenzake, ndipo mtuhumiwa alimchukua na kwenda kumfanyia kitendo hicho cha kinyama nje ya nyumba aliyokuwa amelala, huku watoto wengine wakiwa wamesinzia.

Amefafanua kwamba, mtuhumiwa huyo alifanya kitendo hicho cha kinyama baada ya wazazi wa mtoto huyo (kaka wa mtuhumiwa) kumuacha kwake kwa ajili ya uangalizi baada ya wao kusafiri.

“Ni kwamba wazazi wa mtoto walimuacha kwa baba yake mdogo (mtuhumiwa) kwa ajili ya uangalizi wakati wao wameenda wilayani Sengerema kwa ajili ya matibabu,” amesema Mutafungwa.

Ameongeza kwamba; “Ndipo mtuhumiwa huyo alitumia nafasi hiyo kumfanyia vitendo hivyo vya ukatili na baadaye kumuua kwa kumnyonga kwa kutumia nguo aliyokuwa amejifunika ili kupoteza ushahidi.”

Mutafungwa amesema mwili wa mtoto huyo umefanyiwa uchunguzi wa kitaalamu na umekabidhiwa ndugu kwa taratibu za mazishi, huku mtuhumiwa akiendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani kwa taratibu za kisheria.

“Tunatoa wito kwa wazazi na walezi kuchukua tahadhari kwa watu wa karibu wakiwemo ndugu, wafanyakazi wa ndani na marafiki kwa kutowaamini na kuwaachia watoto, kwani watoto wanapaswa kulindwa kwa ukaribu kama sheria zinavyoelekeza,” ameonya Mutafungwa.