Pacome amtikisa beki City, mastaa wazuiwa kambini

PAMOJA na kuchekelea kiwango alichonacho na matokeo ya pointi moja waliyopata dhidi ya Yanga, beki wa Mbeya City, Baraka Maranyingi amesema haikuwa rahisi kumkabili Pacome Zouzoua kutokana na msukosuko aliompa uwanjani, huku mastaa wa timu huyo wakizuiwa kambini.

Mbeya City iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, ikicheza kwa ubora chini ya kocha mkuu Malale Hamsini ilifanikiwa kuwadhibiti mabingwa watetezi Yanga katika sare ya bila kufungana kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini hapa.

Timu hizo zilikutana ikiwa kila upande unakumbuka sare ya mabao 3-3 tangu zilipokutana Juni 6, 2023, huku rekodi zikionyesha kuwa Mbeya City imeshinda mara moja tu dhidi ya Yanga katika mechi 21 tangu ilipopanda daraja 2013-2014, huku yenyewe ikipoteza mara 11 na sare zikiwa tisa.

TATI 03


Katika mechi hiyo ya jana timu zote zilitengeneza nafasi za mabao, ambapo Yanga itajilaumu kwa mpira wa friikiki uliopigwa na Edmund John na kugonga nguzo na kutoka katika dakika ya 82.

Kwa upande wa Mbeya City, watajilaumu kushindwa kuondoka na pointi zote tatu katika dakika ya 90+5 pale Vitalis Mayanga aliposhindwa kumtungua kipa Djigui Diarra, aliyeokoa kishujaa mpira miguuni mwake wakiwa wamebaki wawili tu, baada ya Omary Chibada kuwachekecha nyota wawili wa Yanga  Ibrahim Baka na Aziz Andabwile — na kumtilia bonge la pasi.

TATI 01


Akizungumza na tovuti ya Mwanaspoti, Maranyingi amesema matokeo waliyopata yalikuwa ni sehemu ya matarajio yao licha ya kwamba hesabu zilikuwa ni kupata pointi tatu baada ya kupoteza dhidi ya Azam kwa mabao 2-0.

Amesema licha ya kiwango binafsi alichoonyesha hadi kuchaguliwa Mchezaji Bora wa Mechi, alikutana na upinzani mkali dhidi ya Pacome ambaye hakumpa utulivu kwa dakika zote.

“Ilikuwa mkakati wa kila mmoja kutimiza wajibu wake, nilifanya kile nilichoelekezwa na kocha kwa kuwa tulihitaji ushindi baada ya kupoteza mechi iliyopita, kwa ujumla Pacome alinipa ugumu kumzuia kwa dakika zote ila nilifanikiwa,” amesema Maranyingi.

Ameongeza kuwa matokeo hayo yanaongeza nguvu na hamasa kwa wachezaji kuendelea kujipanga na kusahihisha makosa kuhakikisha mechi zinazofuata wanafanya vizuri zaidi ili kujiweka katika nafasi nzuri.

TATI 02


Wakati huohuo, benchi la ufundi limezuia mapumziko kwa mastaa kuhakikisha timu inabaki kambini kuendelea na mazoezi kujiwinda na mchezo ujao wa Oktoba 18 utakaopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine.

Ikumbukwe Ligi Kuu imesimama kwa muda kupisha kalenda ya michuano ya kimataifa.