Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, iliyoketi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu Suleiman Kwata (33) kunyongwa hadi kufa, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa makusudi, Editha Charles.
Mshtakiwa anadaiwa kumuua Editha Charles, ambaye ni dada wa kazi (house girl), kwa kumchoma kisu shingoni, tukio alilolitenda Julai 6, 2022 eneo la Kimara Temboni.
Siku hiyo, Kwata alimuua kwa makusudi Editha kwa kumchoma kisu shingoni na kumkaba shingo na hivyo kupelekea kutoka damu nyingi hadi kufa kisha kuchukua mwili huo na kwenda kuuficha stoo.
Mwili huo wa Editha baada ya kuuficha stoo, aliufunika kwa mabaki ya vifaa vya ujenzi na akasafisha nyumba kuficha alama za damu na kisha akaondoka na fedha zote alizoiba kwa bosi wa Editha.
Hata hivyo Julai 9, 2022, Agatha aliaanza kusikia harufu mbaya ya kitu kilichooza nyumbani kwake na walianza kuchuguza pamoja na majirani zake kitu hicho na baadaye walikuta mwili wa Editha akiwa uchi ndani ya stoo, huku ukiwa umeanza kuharibika.
Hukumu hiyo imetolewa leo Oktoba Mosi, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya, aliyepewa mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi ya mauaji.
Hakimu Mbuya alisema upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi 12 na vielelezo 10 vilivyowasilishwa mahakamani hapo.
Alisema Editha alikuwa ni mfanyakazi wa ndani kwa Agatha Stanslaus ambaye aliishi naye na mtoto wake wa kike alikuwa mwanafunzi.
Akipitia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, Hakimu Mbuya alisema siku ya tukio Agatha alitoka kwenda kazini na mtoto wake, alikwenda shuleni huku nyumbani akiwa amebaki Editha kuendelea na shughuli zake za kila siku
Kwata ambaye alikuwa ni jirani alikubaliana na Editha (marehemu) kuiba fedha zilizohifadhiwa katika kibubu chumbani kwa Agatha (bosi wake Editha) ambapo mshitakiwa alifika nyumbani kwa Agatha na kuingia ndani alivunja dirisha na kuingia chumbani akachukua kibubu kisha alivunja kibubu ambacho kilikuwa na fedha,” alisema Hakimu Mbuya na kuongeza
“Baada ya kuvunja kibubu walikaa kuhesabu hizo fedha akiwa na huyo Editha, ambapo walikuta kiasi cha Sh1.6 milioni,” alisema hakimu.
Akiendelea kuchambua ushahidi, alisema walipokuwa wanaendelea kuhesabu hizo fedha mshitakiwa alitawaliwa na tamaa za ngono kwa kutaka kufanya mapenzi na Editha.
Ilielezwa kuwa baada ya Editha kukataa ndipo alimshambulia na kumbaka kwa nguvu kitendo ambacho Editha alikasirika na kumtishia kufichua siri ya wizi kwa mwajiri wake na alivyobakwa.
Mshitakiwa baada ya kutishiwa aliamua kumuua Editha kwa kumchoma na kisu shingoni na kumkaba hadi kusababisha kifo.
Akiendelea kupitia ushahidi huo, hakimu Mbuya alisema mshitakiwa baada ya mauaji hayo alificha mwili huo katika stoo na kufunika kwa mabaki ya vifaa vya ujenzi na akasafisha nyumba kuficha alama za damu, akaondoka na fedha zote.
Baada ya kuondoka Kwata, mtoto wa Agatha alirudi kutoka shuleni na kukuta nyumba ikiwa wazi huku dirisha la chumbani likiwa limevunjwa ndipo alimpigia simu mama yake kuhusu tukio hilo.
“Agatha alivyorudi nyumbani kwake aliingia chumbani, alikuta kibubu kimevunjwa na fedha zote zimechukuliwa alipojaribu kupiga simu ya Editha kabla ya kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi Temboni haikupatikana baadaye akapata ujumbe mfupi uliosema ‘Samahani mama nimeamua kutoroka naomba unisamehe”…ujumbe huo ulitumwa na Kwata kwa kutumia simu ya Editha,” alisema Hakimu, wakati akipitia baadhi ya ushahidi wa Jamhuri.
Ushahidi mwingine ulikuwa ni wa mfanyakazi wa nyumba ya jirani ambaye alimuona mshitakiwa anaingia ndani kwa bosi wake Editha huku akiwa ameshika balbu na bisibisi.
” Siku hiyo nilikuwa kibarazani nilimuona mshitakiwa akiwa ameshika balbu na bisibisi na aliingia ndani kwa kina Editha, baadaye mshitakiwa alitoka peke yake,” alisema hakimu Mbuya na kwamba maelezo ya ushahidi huyo yalisomwa mahakamani hapo baada ya shahidi huyo kutofika Mahakamani kutoa ushahidi.
Mshitakiwa alikuwa anaishi jirani na nyumba hiyo na walikwenda kumuuliza kuhusu kuonekana akiwa na Editha, lakini alikana.
Hata hivyo Julai 9, 2022, walianza kusikia harufu ya kitu kilichooza ndipo walianza kufuatilia wakiwa na majirani walikuta mwili wa Editha akiwa uchi ndani ya stoo umeanza kuharibika na walikwenda kituo cha polisi Temboni walifika kisha mwili ulipelekwa hospitali ya Mlonganzila kwa uchunguzi na mshitakiwa alikamatwa.
Hata hivyo, maelezo yake ya onyo, kwa mlinzi wa amani mshtakiwa alikiri kuwa ndiye aliyefanya mauaji hayo na sababu za kufanya hivyo.
Pia, taarifa ya uchunguzi wa daktari ulieleza kuwa Editha alichomwa na kitu chenye ncha kali shingoni ambacho kilisababishwa na kutokwa damu nyingi.
Kwa upande wa mtaalamu wa vinasaba aliyechukua vina saba kutoka katika mwili wa Editha, ambayo ni michubuko na mpanguso wa ndomo wa kinywa cha mshtakiwa, ushahidi umethibitisha kuwa ndiye aliyemuua.
“Kwa mazingira haya nimeridhika ushahidi huo Kwata ndiyo uliyokuwa mtu wa mwisho kuwa na Editha siku ya Julai 6, 2022, ushahidi mwingine katika kesi hii ni mshtakiwa kukiri maelezo ya onyo na kueleza wazi kilichotokea eneo la tukio,” alisema na kuongeza.
” Hivyo, mahakama imeengemea maelezo ya polisi na maelezo ya ungamo, hivyo inakutia hatiani kama ulivyoshtakiwa,” alisema Hakimu Mbuya.
Awali, kabla ya kutoa hukumu, Wakili wa Serikali Tumaini Mafuru, alidai kuwa hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya mshtakiwa, lakini aliiomba mahakama itamke bila hiyana wala uwoga, kuwa mshtakiwa alishtakiwa chini ya kifungu 197 cha Kanuni ya Adhabu na adhabu yake ni moja nayo ni kunyongwa hadi kufa.
“Hakuna binadamu ambaye ana mamlaka ya kutoa uhai wa binadamu mwenzake isipokuwa Mwenyezi Mungu pekee ndiye mwenye mamlaka,” alidai Mafuru na kuongeza…
Alidai uhai ni zawadi pekee inayotolewa na Mwenyezi Mungu na inatolewa mara moja na ikitoweka haiwezi kurejeshwa na mwenye mamlaka ya kuiondoa ni Mungu peke yake, hivyo apewe adhabu kali ili iwe fundisho.
“Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ibara ya 13 (1) ya katiba inampa kila raia wajibu wa kulinda kwa gharama yoyote uhai wa mwenzake.”
“Hivyo kifo kinaleta huzuni kwa ndugu wa marehemu na kuacha simanzi isiyoisha na Editha alikuwa bado ni binti mdogo na tegemeo kwa ndugu na taifa kwa ujumla, hivyo mahakama yako isione haya kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na jamii kwa ujumla,” alidai wakili Mafuru.
Kwa upande wake, Wakili wa mshtakiwa, Mohamed Majaliwa alidai mteja wake bado ni kijana na taifa linamtegemea, hivyo aonewe huruma kwa kadri itakavyoona inafaa.
Hakimu Mbuya baada ya kusikiliza shufaa za pande zote, alitupilia mbali ombi kuonewa huruma na badala yake alikubaliana na ombi la Jamhuri na kumhukumu kunyongwa hadi kufa.
” Kwa kosa ulilotenda, adhabu pekee kwa mujibu wa kifungu ulichotakiwa ni kunyongwa hadi kufa,” alisema Hakimu Mbuya.
Licha ya kuhukumiwa adhabu hiyo, mshtakiwa alionekana mwenye furaha na yuko kawaida, lakini hata baadhi ya ndugu ambao hawafiki watatu waliohudhuria chumba cha mahakama, hao hawakuonyesha kushtuka na adhabu hiyo, tofauti na hukumu nyingine za adhabu kama hiyo ambapo ndugu, jamaa na marafiki huangua kilio kwa sauti ndani ya chumba cha mahakama hata kama hakimu au jaji hajaondoka ndani ya mahakama.