Wivu wa mapenzi wampeleka jela miaka 25

Arusha. Usemi wa Kiswahili usemao hasira hasara umetimia kwa Jumanne Mlanda, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 25 jela baada ya kukutwa na hatia ya kuua watu wawili bila kukusudia, akiwemo mkewe akiwatuhumu kuwa na uhusiano ya kimapenzi.

Hukumu hiyo imetolewa jana Septemba 30,2025 na Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Geita na Jaji Griffin Mwakapeje aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, na kueleza baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili Mahakama imemkuta mshtakiwa na hatia ya mauaji bila kukusudia na kumuhukumu kifungo cha miaka 25 jela.

Jumanne alishtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha sheria ya kanuni ya adhabu, makosa aliyoyatenda Januari 16, 2025, katika Kijiji cha Nyashinge Wilaya ya Mbogwe Mkoa wa Geita.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa siku ya tukio wakiwa wamelala kwenye msiba wa mwanakijiji mwenzao (Zacharia Changanya), Jumanne alimuua Thomas Kadama kwa kumchoma visu kisha kuelekea nyumbani kwake na kumuua mkewe Angelina Jeremia.

Ilielezwa saa sita usiku waombolezaji wengine wakiwa wamelala, kilio kilisikika kutoka kwa Thomas, baada ya kushambuliwa kwa kisu na mshtakiwa ambaye baada ya kutekeleza hilo alielekea nyumbani kwake na kumshambulia mkewe mbele ya watoto wao, ambao mmoja wao alikuwa shahidi katika kesi hiyo.

Januari 17, 2025 Jumanne alijisalimisha Polisi akiwa na kisu chenye mpini mweusi uliokuwa na madoa ya damu, upinde na mishale minne na kukiri kufanya mauaji hayo.

Hakuishia hapo kwani hata wakati anajitetea mahakamani alikiri kosa hilo la mauaji na kudai hayakuwa ya makusudi.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 10.

Shahidi wa kwanza James Misalaba, alisema siku ya tukio alihudhuria maziko ya Zachari na wakiwa nje kwenye mkesha na waombolezaji wengine walimuona mshtakiwa akimchoma kisu Thomas. Alisisitiza kuwa aliona tukio hilo kwa kuwa kulikuwa na mwanga wa moto na tochi.

Alisema mshtakiwa alikimbia eneo   baada ya tukio hilo na  Thomas aliyekuwa akivuja damu nyingi aliwaambia amechomwa na mshtakiwa na wakiwa njiani kumpeleka Zahanati ya Isebya  alifariki dunia.

Alisema baadaye alijulishwa mshtakiwa alimuua mkewe, Angelina ambaye pia akiwa hospitali kabla hajafariki alimtaja mtuhumiwa kuwa ndiyo kamjeruhi.

Shahidi wa pili, ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyikonga, Philip Kadogosa alisema siku ya tukio alisikia kelele na alipokimbilia eneo zilipokuwa zikitoka   alimkuta Thomas akiwa amejeruhiwa, ambapo shahidi wa kwanza alimweleza kuwa amemuona mshtakiwa akimchoma kisu Thomas.

Shahidi huyo alisema dakika kati ya 10 hadi 15 baadaye alisikia yowe kutoka nyumba ya mshtakiwa na kujulishwa kuwa mshtakiwa alimchoma kisu mkewe.

Alisemamuda mfupi baadaye watoto watano wa mshtakiwa walipelekwa kwake na mmoja wao akamweleza kuwa baba yao (mshtakiwa) alifika nyumbani akamchoma mama yao kisu.

Shahidi wa tatu, Dk Lubinza Mazike kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mbongwe, alisema Januari 16,2025 usiku alimuhudumia Angelina ambaye alifikishwa Kituo cha Afya akiwa na majeraha na utumbo ulikuwa umetoka nje na alikuwa katika hali mbaya.

Aliieleza Mahakama kuwa alimfanyia upasuaji wa dharura na kukuta lita mbili za damu kwenye tundu la tumbo, matundu matatu kwenye utumbo mwembamba na moja kwenye tumbo, baadaye Angelina alifariki kutokana na kupoteza damu nyingi.

Shahidi wa nne, ambaye alikuwa binti wa mashtakiwa mwenye umri wa miaka 13, alisema siku ya tukio akiwa nyumbani kwao na ndugu zake wanne, baba yao alirudi kutoka kwenye maziko ambapo alipiga mlango na kuingia ndani.

Alisema baada ya kutaka apewe mkuki, alimuamuru mkewe aketi, na alipomuhoji kisha akamchoma kisu na kuwa anakumbuka mama yake alipiga kelele kwamba anakufa kwa kuuawa na mumewe.

Shahidi huyo alidai kuona tumbo la mama yake likiwa limejeruhiwa na   alimpa kitambaa ili kufunika kidonda hicho na  baada ya kutekeleza tukio hilo baba yao aliondoka akiwa amebeba mkuki.

Aliendelea kuiambia mahakama kuwa walipiga kelele lakini mlango ulikuwa umefungwa, hadi wanakijiji walipofika na kumpeleka mama yao hospitalini.

Akihojiwa na upande wa utetezi, shahidi huyo alisema wazazi wake hawakuwa na maelewano mazuri lakini hakuwahi kuwasikia wakipigana.

Shahidi wa saba ambaye ni daktari kutoka Zahanati ya Isebya, alisema Januari 16,2025 usiku alipokea Thomas ambaye tayari alishafariki na baadaye alimtibu Anjelina na kumuhamishia kituo cha afya Iboya kutokana na majeraha makubwa ya tumbo.

Alisema aliufanyia uchunguzi mwili wa Thomas na kubaini majeraha ya kisu kwenye kifua na mgongoni ambayo yalisababisha apoteze damu nyingi.

Shahidi wa nane, G 5901 Sajenti Shahibu alisema  kuwa Januari 17,2025 saa 5 asubuhi Jumanne alijisalimisha Kituo cha Polisi Lawangasa na kukiri kumchoma kisu Thomas katika msiba wa mtu mwingine kutoka na tuhuma za kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkewe.

Alisema mshtakiwa alisalimisha na upinde uliokuwa na mishale minne na kisu chenye mpini mweusi, uliokuwa na madoa ya damu yanayoonekana.

Shahidi wa 10, WP 5982, alieleza mahakama Januari 17,2025 alirekodi maelezo ya onyo mshtakiwa, ambapo mshtakiwa alikiri mauaji yote mawili, lakini  kutokana na kutofautiana katika kurasa za taarifa hiyo   Mahakama iliyakataa.

Katika utetezi wake mshtakiwa aliieleza mahakama usiku wa kuamkia Januari 16, 2025 akiwa kwenye msiba, Thomas (marehemu kwa sasa) alimkuta kwenye hema alilokuwa amelala na kumsukuma pembeni akimweleza asogee kando alale, kwani hata mke wake hapendezwi naye na kuwa mke wake tayari ni wake yeye.

Mshtakiwa huyo alisema alikasirishwa na maneno hayo kwani kwa muda mrefu alimshuku Thomas kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkewe, na kwamba hapo awali aliwapata pamoja mara mbili, mara moja ndani ya nyumba yake na nyuma ya nyumba yake.

Alisema akiwa na hasira, alishindwa kujizuia na kumchoma marehemu kwa kisu alichokuja nacho msibani na baadaye kumchoma kisu mkewe na kueleza kuwa alikimbia baada ya tukio na baadaye kujisalimisha polisi.

Mshtakiwa huyo alikiri kuwaua watu wote wawili (mkewe na Thomas) na kwamba alibeba kisu na upinde kwenye mazishi, ambapo watu wengine walikuwapo lakini walikuwa wamelala.

Aidha alifafanua kuwa alibeba silaha hizo kwa ajili ya kujilinda na hakukusudia kumdhuru mtu hadi alipochokozwa.

Jaji Mwakapeje alisema baada ya kuchunguza kwa kina rekodi ya ushahidi na ushuhuda uliotolewa na upande wa mashtaka na utetezi, suala kuu sasa la kuamuliwa ni ikiwa upande wa mashtaka ulithibitisha kosa hilo kwa kiwango kinachohitajika, bila shaka yoyote.

Alisema katika sheria ya makosa ya jinai ni kanuni ya msingi kwamba mzigo wa kuthibitisha hatia ya mshtakiwa iko upande wa mashtaka ambao unapaswa kuthibitisha vipengele muhimu vitatu.

Alivitaja vipengele hivyo ni kwamba mtu amefariki, kifo hakikuwa cha kawaida na kuonyesha uhusiano wa moja kwa moja wa mshtakiwa na kifo hicho na upande wa mashtaka lazima uthibitishe kwamba mauaji hayo yaliambatana na ubaya uliofikiriwa hapo awali.

Jaji alisema ushahidi wa kimatibabu na wa kimazingira unaonyesha kwamba vifo vya watu hao wawili vilisababishwa na mtu havikuwa vifo vya asili.

Kuhusu iwapo kuna ubaya uliofikiwa awali, alisema katika kesi hiyo Jamhuri imeeleza kuwa kuchomwa visu kwa makusudi kwa Thomas  na Angelina  kunaonyesha nia ya kuua au kusababisha madhara makubwa.

“Hata hivyo, mshtakiwa Jumanne ametoa utetezi wa uchochezi unaohitaji kuangaliwa kwa umakini wa mahakama kabla ya kubainika kwa ubaya,”alisema.

Jaji alisema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, mahakama imemkuta Jumanne na hatia ya kuua bila kukusudia kinyume na kifungu cha 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu.

Mshtakiwa huyo kupitia wakili wake, wakati wa maombi ya kupunguziwa adhabu aliiomba mahakama impunguzie kwa sababu ni kosa lake la kwanza, alionyesha majuto ambapo baada ya mauaji alijisalimisha mwenyewe polisi na kukiri makosa yake mahakamani.

Aliieleza mahakama kuwa kwa sasa yeye ndiye mzazi pekee wa watoto sita ambao wanamtegemea.

Jaji alihitimisha kwa kueleza kuwa mahakama inamuhukumu Jumanne kifungo cha miaka 25 jela kwa kosa la kuua bila kukusudia, kinyume na kifungu cha 195 na 198 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.