Dodoma. Vita ya kuisaka Ikulu ya Tanzania sasa imeshika kasi, wagombea 17 wanapishana kuchanga karatasi zao.
Mgombea wa kiti cha urais kupitia chama hicho, Twalibu Kadege akizungumza leo Jumatano Oktoba Mosi, 2025 jijini Dodoma, amesema hana shaka kwamba ataingia ikulu kwa kuwa ni zamu yake.
Amesema anaamini hivyo kutokana na ahadi zake kwa wananchi, watampatia ridhaa ifikapo Oktoba 29 siku ya kupiga kura.
Huku akitumia kauli mbiu yake ya Spidi Mpele mpela hadi Ikulu, mgombea huyo amesema tayari ameshatangaza kuwa kila Mtanzania popote alipo atakuwa mmiliki wa kipande cha ardhi cha ekari tano.
Hata hivyo ameahidi neema zaidi itawaangukia wakulima ambao watamiliki zaidi ya hekari hizo hizo bila kusema watapewa kwa ukubwa gani.
“Nayasema haya siyo kwa maagizo bali namaanisha, angalia watu walisema reli ya SGR isingewezekana, lakini imewezekana na mambo makubwa mengine tumeweza, naomba wananchi wakiamini UPDP na kukipa kura za kutosha ili tukayatende,” amesema Kagede wakati akihutumia kwenye mkutano huo.
Katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na waendesha pikipiki 11 waliokuwa wamefunga bendera za chama hicho, Kadege amebainisha kuwa maeneo makubwa ya ardhi yatatengwa kwa ajili ya wakulima na wafugaji.
Pia amesema serikali yake haitakuwa na muhali na wazembe na wanaokiuka sheria za nchi, na hivyo ametangaza kuwashughulikia kwa kuwapa kifungo cha kuanzia miaka 50 jela.
“Hatutaongoza Serikali ya watu wabadhirifu na wavunja sheria, tutashughulika na kila mtu bila kumuonea aibu wala hadhi yake, adhabu ya kifungo itatembea kwa kila mtu ili kuweka hali ya utulivu nchini,” amesema Kadege.