HAKUNA KODI YA KITANDA KWA WAMILIKI WA NYUMBA ZA KULALA WAGENI- TRA


:::::::::

Mamlaka ya Mapato Tanzania ( TRA), imefafanua kwamba hakuna Kodi inayotozwa kwa kila kitanda kwa wamiliki wa nyumba za wageni bali kuna kodi ya Uendelezaji utalii inayotozwa kwa baadhi ya hoteli zilitangazwa kwenye gazeti la Serikali, na hutokana na malipo ya malazi kwa watalii kwa siku na siyo kwa kitanda kwa kila nyumba ya wageni kama ilivyoripotiwa.

Maneja wa TRA Mkoa wa Kagera ndugu Castro amefafanua zaidi kwamba Tozo hii ilianzishwa na Serikali chini ya kifungu cha 59(1) cha sheria ya Utalii ya 2008 ili kusaidia Maendeleo ya sekta ya utalli nchini, na inatozwa kwa nyumba za kulala wageni/Hoteli zilizosajiliwa na kutangazwa Kupitia tangazo la gazeti la Serikali (GN 823 ya tarehe 02/10/2020).

Tozo hii sio mpya na imekuwa ikitozwa kwa Mmiliki wa jengo linalotoa huduma ya malazi kwa watalii/wageni wa ndani na nje ya nchi kupitia kanuni zilizotangazwa katika gazeti la Serikali GN No 352 ya tarehe 1/10/2013.

Mmiliki wa nyumba ya kulala wageni/Hoteli iliyosajiliwa anatakiwa kulipa asilimia moja (1%) ya gharama ya chumba iliyolipwa na Mgeni.

Ritani na malipo ya kodi hii huwasilishwa kabla au mnamo tarehe ya mwisho wa mwezi unaofuata.