Mwendokasi yazidi ‘kupasua’ vichwa wananachi

Dar es Salaam. Wakati wananchi wakiendelea kulazimika kusubiri muda mrefu kupata huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka maarufu mwendokasi, Serikali mkoani Dar es Salaam imetoa taarifa ya namna inavyoshughulikia kero hiyo, ambayo wengi hulazimika kuyapanda kwa kugombea.

Asubuhi ya leo Oktoba mosi, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amefanya ukaguzi kwenye baadhi ya vituo vya mabasi hayo na kushuhudia kero wanazokabiliana nazo wananchi.

Akiwa kituo kikuu cha Kimara Mwisho, wananchi walikuwa katika hekaheka za kugombea mabasi machache yanayofanya safari, baadhi walisikika wakiimba: “Hatuitaki CCM, hatuitaki CCM.”

Chalamila alipowatuliza na kuwasihi kuwa shida hiyo itakwisha hivi karibuni, baadhi ya abiria walikuwa wakiendelea kugombea kuingia kwenye basi, huku wakiendelea kuimba hata pale walipokuwa ndani ya basi.

Kwa wale waliomsikiliza Chalamila, wakiwamo wanaotoka Mbezi, ambao hushushwa Kimara Mwisho ili kuendelea na safari, walieleza kero inayowakabili ya kusubiri mabasi muda mrefu, huku wakiyapanda kwa taabu kwa kuwa hulazimika kugombea kuingia ndani na wakati mwingine hushushwa, ili mlango uweze kufungwa.

Chalamila akizungumza na wananchi hao amesema: “Leo saa 11:00 alfajiri nimefanya ziara katika baadhi ya vituo vya mabasi yaendayo haraka kuanzia Gerezani hapa Kimara na nitamalizia Mbezi. Hapa tupo na Jeshi la Polisi – RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) na RTO (Mkuu wa Trafiki Kinondoni).”

Amesema amefanya safari kwenye vituo hivyo baada ya kuona video fupi zikionyesha watu wanagombea kuingia kwenye mabasi.


“Nikiri kuwa mabasi yameshapungua sana kutoka kwenye idadi yake mpaka yalivyo sasa. Hivi tunapoongea mabasi ya kampuni ya Udart yanayotoa huduma hayafiki hata 40. Hayo yanayotoa huduma ndiyo yenye uafadhali,” amesema.

Mradi wa BRT katika barabara hiyo ulilenga kuwa na mabasi 305. Hata hivyo, mpaka ulipoanza kufanya kazi mwaka 2016 ulikuwa na mabasi 140.

Mwaka 2021 mabasi 70 yaliyokuwa yamezuiwa baada ya kutokamilika taratibu za kuingizwa nchini, yaliruhusiwa kuingia barabarani, hivyo kufanya idadi kufika mabasi 210, ingawa wakati huo mengine yalikwishahabariki kutokana na mafuriko na sababu nyingine.

Chalamila amesema kutokana na hali hiyo, amepatikana mtoa huduma mwingine nje ya Udart (Kampuni ya Uendeshaji Usafiri wa Haraka) katika njia hiyo, hivyo mabasi yatakayoingia yatakuwa tofauti na Udart.

Hatua hiyo, amesema inalenga kumpata mtu mwingine mwenye nguvu, uwezo na teknolojia ili kuongeza ushindani katika utoaji huduma.

“Barabara ya Kilwa, tulisema ifikapo Agosti 15, mwaka huu kutakuwa na mabasi mapya yatakayoingia kutoka nchini China. Ni kweli ilipofika siku hiyo mabasi yote yaliwasili kwenye Bandari ya Dar es Salaam, baada ya hapo yalianza kushughulikiwa mambo mengine ikiwepo kodi,” amesema.

Amesema mabasi ya Barabara ya Kilwa yaliyowasili ni 151 ambayo yapo kwenye karakana iliyopo Mbagala yakisubiri vibali vyote vikamilike ili yaingie barabarani.

“Mungu akijalia wiki hii au ijayo mabasi ya Mofat (kampuni ya wazawa iliyopewa zabuni) yatakuwa yaanza kufanya kazi. Kilichopo kwenye barabara hii (Morogoro) kwa kuwa mabasi ni machache na uhitaji ni mkubwa, tulishakaa na kampuni ya Mofat ili angalau baadhi ya mabasi yaanze kutoa huduma kwenye barabara hii, halafu mabasi ya Morogoro Road yatapokuwa yamefika basi haya ya Mofat yataendelea na route nyingine.”


Chalamila amesema: (Suala la msingi ni mabasi haya yatakuwa yamefika kwenye barabara hii muda wowote kuanzia kesho (Oktoba 2). Mungu akijalia tuwe tumetatua angalau nusu ya tatizo hili, huku tukisubiri mabasi ya kudumu.”

Ametoa rai kwa wananchi akiwaomba msamaha na kuwataka radhi akisema: “Najua hakuna Serikali yenye lengo la kutenda uovu kwa wananchi wake na kuwataka wahangaike.”

Amesema huduma zinatolewa kwa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi: “Kwa hiyo nimeona ndugu zangu niwaeleze haya Watanzania wa Dar es Salaam waendelee kuvumilia.”

“Tumeona baadhi ya clip wakisema hatuitaki CCM, hatumtaki mama, naomba niwaeleze ukweli kwamba hizi ni hasira za muda mfupi. Mara Serikali itapoingiza mabasi haya naamini kabisa unaposema leo huitaki CCM sawa, usipoitaka ndiyo mbadala wa mabasi? Hapana, kwani lazima tutatue mambo haya kwa kutumia kauli moja, kwa ushirikiano kwa kujua kwamba, hatuna nchi nyingine,” amesema.

Chalamila amesema mabasi hayo yalipoanza miaka mingi nyuma watu wengi waliyabeza na kuonyesha kuwa ni mradi wa aina gani, lakini siku zinavyozidi kwenda wanagundua mabasi hayo ni msaada mkubwa.

“Tunachokiona leo mahitaji ni makubwa, ingekuwa siyo kitu kizuri, usingemuona mtu anasukumana mlangoni kwenye hayo mabasi. Kwa hiyo hakuna namna, Serikali lazima isimamie mradi huo,” amesema na kuongeza:

“Katika hili nashukuru sana Waziri Mkuu wetu amekesha usiku na mchana kuendesha vikao kuona namna ambavyo tunaweza kutatua jambo hili. Zitakuja mamlaka zingine za juu kuja kuwaeleza Watanzania na pengine wasiwe na wasiwasi kuhusu huduma hii ya mabasi yaendayo kwa haraka.”

Watendaji wa Mofat hawakupatikana kuzungumzia makubaliano hayo.

Alipotafutwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Dk Athuman Kihamia kutoa ufafanuzi kuhusu kauli ya Chalamila amesema:

“Nadhani kwa kuwa Mkuu wa Mkoa ndiye aliyeongea ni vema akatafutwa yeye kulifafanua zaidi kama hamjalielewa au hata msaidizi wake, lakini kwa mimi sina cha kuongea juu ya hilo.”

Huduma ya usafiri huo hayo katika Barabara ya Kilwa ilipangwa kuanza Septemba baada ya mabasi 151 kuwasili nchini lakini hilo halikifanyika, moja ya sababu ilitajwa ni kutokuwapo mageti janja kwa ajili ya malipo.

Mabasi hayo yatafanya safari kati ya Mbagala-Gerezani, Mbagala –Kivukoni na Mbagala- Morocco.

Mradi huo wa awamu ya pili utakaotekelezwa ukiwa wa pili baada ya ule wa Kimara ulioanza mwaka 2016, utaendeshwa na kampuni ya wazawa ya Mofat kwa mkataba wa miaka 12. Kampuni hiyo inatarajiwa kuingiza nchini mabasi 255.

Leo Oktoba mosi, Mwananchi imeshuhudia mashine zikiwa zimeshafungwa kwenye mageti janja ya vituo vingi, huku kazi ikiendelea.

Kwenye vituo vya Kamata hadi Mbagala Rangi Tatu kulikuwa na mafundi wakiendelea na kazi, ikiwemo kuvifanyika usafi kwenye vituo.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi, wamesema licha ya kazi zinazoendelea kufanyika, wataamini iwapo huduma itatolewa pale watakapopanda mabasi.

“Kufungwa mashine, kufanywa usafi hakuwezi kutuaminisha kwamba ndiyo huduma zinaanza, isipokuwa tutaamini siku tutakapokuwa ndani ya mabasi,” amesema Zuwena Kimweri, mkazi wa Mbagala Rangi Tatu.

Kwa upande wake, Doto Charles, amesema tangu mabasi hayo yaingine nchini takribani mwezi mmoja, wanayaona kituoni tu licha ya wao kutaabika kutokana na adha ya usafiri.

Mabasi 99 yaliwasili nchini Agosti 5 na mengine 52 Agosti 26, 2025. Yote yapo katika karakana ya Mbagala Rangi Tatu.

Mabasi hayo yenye urefu wa mita 18 kila moja yana uwezo wa kubeba abiria 160 na matarajio ya Mofat ni kusafirisha abiria 325,000 hadi 400,000 kwa siku.

Awali, huduma kwa barabara ya Mbagala zilikuwa zianze Septemba mosi, 2025 lakini ilishindikana kutokana na kutokamilika kwa kituo cha kujazia gesi na kufungwa mageti janja yatakayotumika kuchanjia kadi wakati wa kuingia kwenye vituo hivyo.


Lengo ni kuondokana na matumizi ya tiketi, hali ambayo inaaminika itasaidia uhifadhi wa mazingira na kudhibiti upotevu wa mapato.