Dodoma. Halmashauri ya Jiji la Dodoma imefunga CCTV kamera kwenye barabara kuu za kuingia na kutoka kwenye jiji hilo na kwenye mikusanyiko mikubwa ya watu, ili kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na kudhibiti wizi na uhalifu.
Aidha watu binafsi na wamiliki wa majengo marefu wameombwa kufunga kamera hizo kwenye majengo yao ili kuimarisha usalama kwani zilizofungwa na Jiji hazina uwezo wa kupata picha kwenye majengo yenye ghorofa zaidi ya 10.
Hayo yameelezwa leo Jumatano Oktoba 1, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabiri Shekimweri wakati wa ukaguzi wa kamera hizo ambazo ndiyo mara ya kwanza kufungwa jijini humo.
Amesema mpango wa kufunga CCTV kamera kwenye mitaa ya Jiji la Dodoma ni wa muda mrefu lengo likiwa ni kuimarisha ulinzi na usalama kwenye mali za umma .
“Dira ya mpango huu ni kuunga mkono ujio wa makao makuu ya Serikali na sisi kama watendaji ni jukumu letu kuongeza usimamizi na usalama wa mji kwa kuwa hivi sasa kuna wageni wengi wanaingia hapa,” amesema Shekimweri.
Amesema mradi huo umegharimu Sh473 milioni ambapo jumla ya CCTV kamera 106 zimefungwa kwa kipindi cha miezi mitatu na zimeshaanza kufanya kazi.
Amesema kamera hizo zimeunganishwa na akili unde (AI) pamoja na mifumo mingine ya Serikali kama vile trafiki na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa ajili ya utambuzi zaidi wa matukio ya uhalifu na uvunjifu wa amani.
Amesema kamera hizo pia zitasaidia kuwatambua watu wasiokuwa na vibali vya ujenzi wanaojenga kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kama vile milimani, maeneo ya wazi, kwenye maegesho na kuimarisha usafi wa mazingira.
Shekimweri amesema usimikaji wa kamera hizo umezingatia vigezo kadhaa ikiwemo barabara kuu zote nne zinazoingia na kutoka kwenye Jiji la Dodoma, maeneo yenye matukio ya uhalifu na maeneo ya uwekezaji wa viwanda na biashara.
Naye mkandarasi aliyefunga kamera hizo kutoka kampuni ya Smart Systems, Wisley Ussiri amesema wamefunga aina tatu za kamera zenye uwezo tofauti ambazo zitatumika kufuatilia na kugundua sura za wahalifu, kusoma namba za magari na kujua kama mtu amevaa kofia ngumu (helmet) na kamera za masafa marefu ambazo zina uwezo wa kuvuta picha ya mtu aliye umbali wa kilomita 4.5.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema kamera hizo zitasaidia ulinzi kwenye jiji hilo.
Aidha amewapongeza wananchi ambao wamefunga kamera hizo kwenye maeneo yao ya biashara kwani wameonyesha uzalendo na ulinzi .
Mwenyekiti wa madereva bodaboda kijiwe cha Bahiroad, William Michael amesema kamera hizo zitasaidia kuwakamata madereva ambao hawafuati sheria za usalama barabarani, lakini pia waharibifu wa miundombinu ya barabara.
Naye mfanyabiashara katika soko la Machinga, Neema Ndoje amesema jitihada zilizofanywa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni za kupongeza kwani kuna matukio mengi ya uhalifu yanayofanyika kwenye mikusanyiko ya watu, lakini wahusika hawachukuliwi hatua kwa sababu hawakuonekana.
Amesema kufungwa kwa kamera hizo kutasaidia kuwabaini wahalifu hata bila kutumia askari polisi ambao ni wachache na hawawezi kuwepo kila mahali.