Gamondi aanza kunogewa Singida Black Stars

WAKATI timu inajiandaa na kusherehekea ubingwa wa mashindano ya Kanda ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), kocha mkuu wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi amesema bado wana kazi kubwa ya kufanya kuendeleza ushindani.

Ligi Kuu Bara inatarajia kusimama kwa muda wa wiki mbili kupisha kalenda ya Fifa, huku timu hiyo ikiwa inaongoza msimamo baada ya kushinda mechi zote mbili ilizocheza katika michuano hiyo.

Akizungumza na tovuti ya Mwanaspoti, Gamondi amesema licha ya kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa na ligi hawapaswi kuamini kuwa wapo vizuri na kujisahau kwa kupumzika wiki zote mbili, hivyo watakuwa na mapumziko ya muda na kuendelea na ratiba ya kujifua kama kawaida.

“Tumeanza vizuri na tuna timu bora, lakini hilo halitufanyi tukaendelea na ratiba ya kuijenga timu ambayo bado inahitaji kutengeneza muunganiko zaidi ili kuweza kuendelea kutoa ushindani,” amesema na kuongeza:

GAMO 02


“Bado naendelea kuijenga timu na siku zote timu bora ni ile inapata mbinu mpya kila siku ni kweli kuna mapumziko ya wiki mbili lakini siwezi nikawaacha wachezaji kwa wiki zote mbili watatakiwa kuwahi kurudi kuendelea na maandalizi.”

Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Masanza amesema timu hiyo inaanza safari ya kurudi mjini Singida leo ambapo watapokewa na mashabiki wao kuanzia Itigi wilayani Manyoni kwa makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Yohana Msita.

“Baada ya mapokezi kutoka kwa mashabiki wa timu yetu Singida kwa paredi Jumapili tutafanya sherehe za ubingwa wa Cecafa makao makuu ya klabu Singida mjini.” amesema Masanza.

GAMO 01


Singida Black Stars ndio mabingwa wa Cecafa 2025/26 na imeanza vizuri ligi ya ndani ikishinda mechi zote mbili dhidi ya KMC bao 1-0, na kuilaza Mashujaa kwa ushindi wa bao 1-0, huku kimataifa ikifuzu hatua inayofuata baada ya kuifunga Rayon Sport ya Rwanda nyumbani na ugenini.