Moshi. Dereva wa gari aina ya Toyota Noah lililopata ajali wakati likitoka harusini na kusababisha vifo vya watu sita wakiwemo abiria na dereva mwenyewe, ameagwa na kuzikwa nyumbani kwao, Moshi.
Ajali hiyo ilitokea Jumapili, Septemba 28, 2025, katika eneo la Njiapanda, Moshi, baada ya gari dogo aina ya Toyota Noah, walilokuwa wakisafiria kutoka harusini mkoani Tanga, kugongana uso kwa uso na lori la mizigo lenye tela.
Dereva huyo, Samueli Nyerembe (44), amezikwa leo, Oktoba 1, 2025, katika mazishi yaliyofanyika Kijiji cha Chekereni, Bonite, Wilaya ya Moshi.

Akitoa salamu za rambirambi kwenye mazishi hayo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Chekereni, Jacob Kampande, amesema msiba huo ni pigo kwa wananchi wa eneo hilo.
“Tumepoteza mtu mahiri, msikivu na mdau wa maendeleo ya kijiji chetu. Ajali hii imeondoa watu wengi kutoka hapa, ni msiba mzito sana,” amesema Kampande.
Mtoto wa kwanza wa marehemu, Johnson Samueli, akisoma wasifu, amesema baba yake alizaliwa Arumeru mkoani Arusha Septemba 23, 1981 na amefariki dunia Septemba 28, 2025, akitoka harusini Tanga.
Kwa upande wake Mchungaji msaidizi wa Kilimanjaro Revival Temple (KRT), Nelson Mwasha, amewataka wananchi kusaidia familia ya marehemu, hasa mjane na watoto waliobaki.
“Tupo hapa kutoa faraja. Naomba tuwe vyombo vya msaada, tusimame pamoja kuwasaidia familia hii isiwe peke yao kwenye msiba huu,” amesema Mwasha.
Akitoa salamu za rambirambi, Mwenyekiti na Mratibu wa Matawi ya Klabu ya Yanga mkoani Kilimanjaro, Wilbad Lyimo amesema kuwa marehemu Samueli alikuwa mwanachama mwaminifu na shabiki wa dhati wa klabu hiyo.

Ameeleza kuwa kifo chake ni pigo kwa familia ya Yanga, kwani mara nyingi alikuwa mstari wa mbele kutoa huduma za usafiri kila wanachama walipohitaji, hususan katika shughuli mbalimbali za klabu.