Kipigo chamzindua Kocha Mashujaa FC

BAADA ya Mashujaa kuchapwa bao 1-0 juzi na Singida Black Stars, kocha Salum Mayanga amesema anahitaji muda wa kutengeneza balansi maeneo yote mawili kwa maana ya kujilinda na kushambulia.

Kichapo hicho ni cha kwanza kwa timu hiyo msimu huu Ligi Kuu Bara baada ya kuanza na sare ya bao 1-1 dhidi ya JKT Tanzania Septemba 18, 2025, kisha kushinda 1-0 mbele ya Mtibwa Sugar, Septemba 21.

“Tulistahili kupata pointi tisa katika mechi tatu, lakini tumepata nne na kudondosha tano, sio mbaya wala sio nzuri sana pia kwetu kwa sababu ya ubora wa washindani wetu. Tuna wiki mbili za kutengeneza balansi ya timu,” amesema Mayanga.

Kocha huyo amesema timu hiyo ina wachezaji bora na wazoefu, ingawa wanahitaji muda zaidi wa kuzoeana ili kutengeneza kikosi cha ushindani, hivyo, wiki mbili ligi inaposimama zitasaidia kufanikisha hilo.

MAYA 01


Bao la Mkenya Elvis Rupia dakika ya 45+5 lliifanya Mashujaa kuendeleza uteja kwa Singida kwani msimu uliopita ilichapwa bao 1-0 la Marouf Tchakei dakika ya 87 pambano lililopigwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, Oktoba 4. Mechi ya raundi ya pili iliyopigwa kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida, Singida ilishinda mabao 3-0 Februari 26, 2025 yaliyofungwa na Mghana Jonathan Sowah aliyefunga mawili na Rupia.

Pambano hilo la Februari 26, 2025, ndilo lililositisha rasmi mkataba wa aliyekuwa Kocha wa Mashujaa, Abdallah Mohamed ‘Baresi’, baada ya kukiongoza kikosi hicho jumla ya mechi 22 za Ligi Kuu, akishinda tano, sare minane na kupoteza tisa.

Baada ya kuondoka Baresi, Machi 21, 2025, uongozi wa Mashujaa ukamtangaza Mayanga kukiongoza kikosi hicho akitokea Mbeya City iliyokuwa inashiriki Championship, kisha timu hiyo kupanda daraja na kucheza Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026.

Kwa msimu wa 2024-2025, Mayanga aliiongoza Mbeya City katika mechi 23 za Ligi ya Championship, ambapo alishinda 14, sare saba na kupoteza miwili tu, huku kwa upande wa Mashujaa akiiongoza kumaliza nafasi ya saba na pointi 35 katika Ligi Kuu.