Othman aahidi kuboresha muundo wa ZEC

Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar (ACT Wazalendo), Othman Masoud Othman, amesema Serikali atakayoiunda itafanya mabadiliko ya muundo wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ili kulinda maslahi ya sasa na vizazi vijavyo, kuepuka kasoro zinazojitokeza wakati wa uchaguzi.

Ametoa msimamo huo, leo Jumatano Oktoba Mosi, 2025 wakati akizungumza na wazee mashuhuri wa Shehia ya Pujini, Wilaya ya Chake Chake Pemba katika mwendelezo wa kampeni zake za kusaka kura zitakavyomhakikishia ushindi Oktoba 29, mwaka huu.

Othman amedai kuwa muundo ZEC uliopo hivi sasa umekuwa ukisababisha migogoro kutokana na kasoro zinajitokeza kwa nyakati tofauti na kusababisha wagombea hasa wa upinzani kutopata haki zao.

Katika maelezo yake, amesema mara kadhaa wamekuwa wakishauri na kujishusha kudai mabadiliko ya muundo wa ZEC ili kuepusha kasoro zinazojitokeza katika chaguzi ikiwemo vurugu na zinazosababisha uvunjifu wa amani.

Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ametolea mfano katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 baadhi ya wananchi Pemba na Unguja walipoteza maisha, huku wengine wakiacha wajane na yatima.

“Haiwezekani kuwepo na ushindani wa kweli wa kisiasa, kwa Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Tume wanachaguliwa na Rais ambaye naye ni sehemu ya wagombea,” amesema na kuongeza;

“Hali hii, inavunja misingi ya kidemokrasia na kuondoa matumaini ya wananchi kuona Zanzibar yenye siasa safi na uchaguzi wa haki,” amedai Othman.

Katika mkutano huo, Othman alikumbushia kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU), hatua ilikuwa na nia njema na makubaliano ya wazi baina ya Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi wa Serikali wakati huo.

Hata hivyo, Othman amedai makubaliano hayo yalipuuzwa na kugeuzwa mtaji wa kisiasa bila kutekelezwa kikamilifu, jambo ambalo limeendelea kuileta sintofahamu visiwani humo.


Othmana amesema si wananchi wote wa Zanzibar wanakubaliana na muundo wa ZEC ndio maana kwa nyakati tofauti ACT Wazalendo imekuwa ikidai mabadiliko makubwa ili kuondoa utegemezi wa ZEC kwa Rais wa Zanzibar.

Othman amesema Serikali itakayoundwa na ACT Wazalendo itahakikisha tume mpya inaundwa kwa kuzingatia misingi ya uhuru, haki na uwakilishi wa kweli wa wananchi wote, ili kuepusha Zanzibar na vurugu katika uchaguzi.

“Itakuwa Tume Huru yenye kuaminika, ndio msingi wa uchaguzi wa haki.Bila kufanya hivyo, Zanzibar itaendelea na migogoro ya kisiasa.

“Hatua hii ndio itakayojenga Zanzibar mpya yenye amani ya kudumu na maendeleo yanayomgusa kila mwananchi bila ubaguzi,” ameeleza.

Mkazi wa Pujini Mzee Suleiman Salim amesema wamefarijika kusikia dhamira ya ACT – Wazalendo ya kuleta mageuzi ya kweli katika ZEC akidai chombo hicho kimekuwa kikwazo cha muda mrefu.

“Tumeshuhudia chaguzi nyingi, na tumekuwa tukiona matatizo yale yale kila wakati. Kauli ya Othman imetupa matumaini kuwa safari hii Zanzibar inaweza kuanza ukurasa mpya wa kisiasa,” amesema.

Naye Mwanakombo Hassan, amesema, “Wanawake na vijana ndio wamekuwa wakipata mateso makubwa katika kila uchaguzi.Tunataka mabadiliko, tunataka amani ya kudumu,Othman ametupa imani kuwa anaweza kulinda heshima ya kila mwananchi,” amesema.