Moshi. Wakati mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, akiendelea kuinadi ilani ya chama hicho na kuomba ridhaa ya miaka mitano ijayo, wajumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho wameeleza kwanini Watanzania wanapaswa kumchagua mgombea huyo.
Wajumbe hao, Nape Nnauye na Profesa Kitila Mkumbo, ambao ni miongoni mwa wanasiasa waliopanda jukwaani katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mashujaa Moshi Mjini, kumuombea kura Samia.
Nape, ambaye pia ni mgombea ubunge wa Mtama, amesema uamuzi wa CCM kumteua Samia kuwa mgombea urais haukufanywa kwa kukurupuka.
Amesema hakuna sababu ya Watanzania kuvurugwa na mambo ya mtandaoni, akieleza CCM ilifanya tathmini ya kina na kikajiridhisha na uimara na uzalendo wa mgombea wake.
“Wakati tunapitisha jina la mgombea, tulifanya tathmini kuangalia rekodi yake ya uadilifu, uzalendo na utu katika kusimamia rasilimali za nchi yetu. Tulijiridhisha bila shaka kuwa anastahili, na ndiyo maana tukamteua kuwa mgombea.
“Wale wenye mashaka, waje na takwimu tushindane mezani, waache porojo za barabarani. Sisi tuna takwimu na ushahidi kwamba mgombea wetu anafaa na hilo limeonekana kwenye kazi alizofanya, alivyoongeza makusanyo na kusimamia mgawanyo wa rasilimali,” amesema Nape.
Ametumia fursa hiyo pia kuwaomba vijana kujitokeza kwa wingi Jumatano, Oktoba 29, 2025, kumpigia kura mgombea urais wa CCM ili apate ushindi wa kishindo.
“Nawaomba Watanzania tumpe kura mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan. Wapuuzeni wanaosema ameshindwa. Serikali ya Samia ingekuwa na matundu ya rushwa tusingeona haya makusanyo yakiongezeka,” amesisitiza Nape.
Kwa upande wake, Profesa Kitila, ambaye pia ni mgombea ubunge wa Ubungo mkoani Dar es Salaam, amesema kuna sababu tatu za Watanzania kumchagua Samia kwa kuwa amegusa maisha yao.
“Samia, kupitia falsafa yake ya R4 kuifungua nchi, amefungua fursa za biashara katika ukanda wa kaskazini, kuwezesha kufanya biashara na nchi jirani pamoja na masoko. Kanda hii, utalii ulizima lakini katika kipindi cha miaka minne utalii umefunguka,” amesema Profesa Kitila.
Amesema alipoingia madarakani uchumi ulikuwa asilimia 3.9, lakini sasa ni asilimia 5 na wanatarajia mwaka huu utafika asilimia 6. “Mama huyu, kupitia sera zake, amefungua uwekezaji zaidi ya miradi 900 iliyosajiliwa kanda ya kaskazini,” amesema Profesa Kitila.
Amesema katika kipindi cha miaka minne, Serikali imepeleka kwa wananchi Sh5.7 trilioni na wananchi wamenufaika kupitia fedha hizo zilizotolewa kwenye programu mbalimbali za maendeleo zinazotekelezwa.
“Niwaambie Watanzania, Samia ni fursa kubwa ya kuleta mageuzi ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Ana uzoefu wa kutosha, hivyo anastahili kupewa nafasi,” amesema Profesa Kitila.
Akihutubia maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro waliojitokeza kwenye mkutano huo, Samia ametoa ahadi kadhaa huku mkazo mkubwa ukiwa kwenye sekta ya miundombinu.
Katika sekta hiyo, amesema ahadi yake ni kuufungua mkoa huo na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa kujenga barabara zitakazoweza kupitika mwaka mzima.
Kauli ya mgombea huyo kuwa anatambua hitaji kubwa la wakazi wa mkoa huo ni miundombinu ya barabara, iliibua shangwe katika viwanja hivyo. Ombi hilo pia liliwasilishwa na wagombea ubunge wa majimbo mbalimbali ya Kilimanjaro.
Amesema katika Jimbo la Moshi Mjini, ahadi ni kujenga barabara ya mchepuko kutoka Kae hadi Airport yenye urefu wa kilomita 31 kwa kiwango cha lami, sambamba na kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 17 za barabara ndani ya mji huo.
Katika Jimbo la Moshi Vijijini, ahadi ni kukamilisha barabara tano zinazojengwa kwa kiwango cha lami, na hilo litafanyika pia katika barabara mbili za Jimbo la Vunjo, ikiwemo moja iliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi.
“Same pia kuna tatizo la barabara za milimani. Tutakwenda kuzijenga ili zipitike mwaka mzima. Rombo pia tutakamilisha ujenzi wa barabara ya Holili-Tarakea ambayo itatusaidia kukuza biashara na wenzetu wa Kenya na kupunguza msongamano wa magari yanayopita barabara ya Mwika,” amesema.
Ahadi nyingine iliyopokelewa kwa shangwe katika mkutano huo ni ufufuaji wa viwanda vilivyokufa baada ya kubinafsishwa.
Samia amesema Kilimanjaro ni miongoni mwa mikoa iliyoathiriwa na ubinafsishaji wa viwanda hivyo, na ahadi yake ni kuvifufua viwanda hivyo kwa kuwatafuta waendeshaji wengine, vikiwemo vyama vya ushirika.
“Mji wa Moshi ulikuwa na viwanda vingi vya kimkakati, lakini baada ya kubinafsishwa vingi vilishindwa kuendelea na uzalishaji, ajira nyingi zikapotea.
“Tunakwenda kutafuta waendeshaji wengine, ikiwemo vyama vya ushirika. Vyama hivi tumevijenga kiasi ambacho vinaweza kuendesha viwanda, na pia tutatafuta wawekezaji wengine kusaidia ufufuaji wa hivi viwanda, na hili litafanyika nchi nzima,” amesema.
Akitolea mfano wa Kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools kilichopo Moshi, ambacho kilifufuliwa baada ya kusimamisha uzalishaji kwa zaidi ya miaka 20, amesema sasa kimeanza uzalishaji wa vipuri vya mashine mbalimbali.
“Ahadi yetu ni kukiimarisha kiwanda hiki kwa kuhakikisha kinapata malighafi ya chuma na makaa ya mawe ya kutosha kwa ajili ya kuinua uchumi wa mkoa huu,” ameahidi Samia.
Akizungumzia sekta ya kilimo, Samia amewaahidi wakulima wa kahawa kwamba Serikali yake itaendelea kutoa pembejeo na mbolea za ruzuku, pamoja na kuanzisha vituo vya zana za kilimo.
Kwenye sekta ya ufugaji, amesema licha ya kutoa ruzuku ya chanjo ya mifugo, Serikali itaongeza maeneo maalumu kwa ajili ya wafugaji kutoka ekari milioni 3.6 hadi ekari milioni sita.
Amesema katika maeneo hayo wafugaji watafundishwa mbinu za kisasa za ufugaji, ikiwemo upandaji wa majani na kuwafanya ng’ombe wale sehemu moja, mpango utakaochangia kupunguza migogoro na wakulima.
Kwenye sekta ya afya, amesema Serikali itaendeleza maboresho katika hospitali za Moshi, Mwanga na Rombo, pamoja na kuiongezea uwezo hospitali ya rufaa ya Mawenzi kwa kuipatia vifaa tiba, dawa zote muhimu na watumishi ili kuimarisha utoaji wa huduma za kibingwa.
“Mbali na kuiongezea uwezo hospitali hiyo, tumejenga vituo vya afya na zahanati na tutaendelea kujenga na kuviwekea vifaa tiba na dawa ili kusogeza huduma zaidi kwa wananchi. Kwa kifupi, Mkoa wa Kilimanjaro unakwenda kujitosheleza kwa huduma zote za afya,” amesema.
Kwenye sekta ya maji, amesema licha ya mpango wa kutekeleza awamu ya pili ya mradi wa Same-Mwanga-Korogwe, endapo atapata ridhaa, Serikali yake itatekeleza miradi mingine ya maji katika mkoa huo, lengo likiwa kuhakikisha kila mwana Kilimanjaro anapata maji safi na salama.