Pacome aitwa Ivory Coast kufuzu Kombe la Dunia 2026

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua ameitwa kwa mara ya pili kwenye timu ya taifa ya Ivory Coast kwa ajili ya mechi mbili za kufuzu Kombe la Dunia 2026.

Pacome anaungana na Kessie Franck, Fofana Seko na Ibrahim Sangare anayecheza Nottingham Forest ya England kwenye eneo la kiungo kujiandaa na mechi dhidi ya Seychelles ugenini Oktoba 10, 2025 na Kenya nyumbani Oktoba 14, 2025.

Pacome aliyeanza vizuri msimu huu kwa kufunga bao la ushindi dhidi ya Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii wakati Yanga ikishinda 1-0 na kubeba taji hilo, anaungana na nyota wengine 23 walioitwa kwa ajili ya mechi hizo mbili.

TATI 03


Nyota wengine walioitwa ni makipa, Fofana Yahia, Kone Mohamed na Lafont Alban. Katika eneo la ulinzi ni Agbadou Emmanuel, Doue Guela, Gbamin Jean Philippe, Konan Ghislain, Kossounou Odillon, Ndicka Evan, Operi Chtistopher, Singo Wilfriend na Milieu De Terrain.

Wakati eneo la ushambuliaji likiwa na Adingra Simon, Diakite Oumar, Diallo Amad, Diomande Yan, Guessand Evann, Haller Sebastien, Pepe Nicolas na Tourw Bazoumana.

Pacome Zouzoua kwa mara ya kwanza alijumuishwa kwenye kikosi cha awali cha wachezaji 53 kilichoandaliwa kwa ajili ya AFCON 2023 lakini baadae jina lake likatolewa baada ya mchujo kufanyika.

NDO 01


Mara ya pili kiungo huyo kujumuishwa kwenye kikosi hicho ilikuwa 2024, Ivory Coast ilialikwa kushiriki michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Uruguay na Benin, Machi 2024 ambapo majeraha aliyokuwa nayo kipindi hicho, akashindwa kucheza.

Katika kufuzu Kombe la Dunia 2026, Ivory Coast inaongoza Kundi F ikikusanya pointi 20 baada ya kucheza mechi nane, bado mbili kumaliza hatua hiyo na kama ikibaki kileleni, itafuzu moja kwa moja.

Ivory Coast tayari imewahi kushiriki Kombe la Dunia ikianza mwaka 2006 nchini Ujerumani, kisha 2010 Afrika Kusini na 2014 Brazil ambapo zote imeishia makundi.