Dar wamkabidhi Dk Nchimbi kero tano

Dar es Salaam. Kampeni za mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi katika mkoa wa Dar es Salaam, zimekutana na changamoto kuu tano na kuahidi kuzitafutia ufumbuzi.

Dk Nchimbi amefanya mikutano kwa siku nne katika mkoa huo wenye majimbo 12 ya Kigamboni, Kawe, Kivule, Ukonga, Mbagala, Segerea, Chamanzi, Ilala, Ubungo, Kibamba, Temeke na Kinondoni.

Mkoa wa Dar es Salaam ni wa 15 kwa kampeni za Dk Nchimbi kutafuta ushindi wa CCM wa mgombea urais, Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.

Mikutano ya kampeni Dar es Salaam ilianza Jumapili ya Septemba 28 na inahitimishwa leo Jumatano, Oktoba 1, 2025 kisha atasafiri hadi Mtwara na Lindi kuendelea kuzitafuta kura za chama hicho tawala.

Changamoto ambazo zimeibuliwa na wagombea ubunge wa majimbo hayo na kumwomba Dk Nchimbi kuzifikisha kwa Samia ni, ubovu wa barabara, uhaba wa maji, masoko ya wafanyabiashara, umeme wa uhakika na adha ya usafiri na usafirishaji.

Dk Nchimbi ameeleza mikakati mbalimbali ya kuitatua iwapo wananchi wa Jiji hilo la kibiashara Tll watakichagua tena chama hicho ili kuwatumikia katika kipindi cha miaka mitano ijayo akisisitiza: “CCM ndiyo chama chenye uzoefu na uthubutu wa kubaini matatizo ya wananchi na kuyashughulikia.”

Mradi wa Kuendeleza Miundombinu Dar es Salaam (DMDP) awamu ya pili umeelezwa na wagombea ubunge kwamba unaweza kumaliza tatizo la ubovu wa barabara kama fedha zitatola kwa wakati.

Wagombea ubunge, Haran Sanga (Kigamboni), Kakulu Burchard (Mbagala), Abdallah Chaurembo (Chamanzi), Jerry Silaa (Ukonga), Bonnah Kamoli (Segerea),  Angellah Kairuki (Kibamba),  Profesa Kitila Mkumbo (Ubungo) na Mussa Zungu wa Ilala ni miongoni mwa waliowasilisha changamoto hizo hususan za barabara na maji.

Dk Nchimbi akiwa Kigamboni, alikabidhiwa changamoto tatu za barabara, umeme wa uhakika kwanini umekuwa unakatika katika pamoja na vivuko.

“Sisi wana Kigamboni tuna changamoto mbalimbali na kubwa sana ni barabara, imekuwa ni changamoto ambayo tuna amini ndiyo inaendesha uchumi wetu, tunawaomba mtuwekee bajeti ya kutosha kwenye eneo hili,” amesema Sanga.

Tatizo la barabara limezungumzwa na Chaurembo wa Chamanzi akiomba kwa Dk Nchimbi kuweka msukumo. Kakulu wa Mbagala naye aliweka msisitizo kwenye eneo hilo la barabara akisema zikikarabatiwa na au kujengwa zitawarahisisha wananchi kusafiri.

Bonnah wa Segerea hakuwa nyuma kubainisha changamoto hiyo pamoja na maji akisema: “Wananchi wa Segerea hawana shaka Oktoba 29 tunatiki, lakini wanaomba tatizo la maji lishughulikiwe kwani wanahangaika hasa kina mama.”

Katika ahadi za Dk Nchimbi kwenye eneo la barabara, amesema Ilani ya uchaguzi mkuu 2025/2030 imebainisha jinsi ambavyo barabara za kila jimbo zinakwenda kujengwa.

Mathalani, Kigamboni anasema miaka mitano ijayo wanakwenda Kukamilisha ujenzi wa barabara ya  Kibada hadi Mwasonga. Ujenzi wa barabara Tungisongani hadi Kimbiji JKT, Kibada hadi Stendi, Mji Mwema- Kimbiji hadi Mpemba Mnazi.

“Uboreshaji wa barabara ndogondogo za mtaa utafanyika,” amesema Dk Nchimbi.

Baadhi ya barabara ambazo Dk Nchimbi ameahidi kujengwa kwa lami na changarawe  Ukonga, Kivule na Segerea ni za Pugu- Majohe, Mombasa- Kivule, Pugu Mpakani, Majohe – Kigogo Fresh na barabara ya Chuo cha Kimataifa cha Kampala.

Barabara zingine ni ya Bonyokwa – Majichumvi, ya Kimanga, Segerea- Kanisa la KKKT, Kifuru- Pugu Stesheni.

Eneo la usafiri na usafirishaji, ni miongoni mwa changamoto ambazo zinalikumba jiji la Dar es Salaam na Sanga aligusia vivuko vya Kigamboni vilivyokwenda kwenye matengenezo akiomba vimalizike haraka.

Katika mkutano wa Maturubahi wenye majimbo ya Mbagala na Chamanzi, Dk Nchimbi anasema barabara ya mwendokasi ya Mbagala imekamilika na kinachosubiriwa ni mabasi yaanze kufanya kazi.

“Mabasi 155 yameshaingia nchini tayari, kinachofanyika sasa ni kukamilisha mambo ya kiutendaji na yakianza kutumika yatamaliza changamoto ya usafiri,” anasema.

“Nia ya CCM kumaliza changamoto ya foleni Dar es Salaam, lakini tumedhamiria kujenga barabara ya njia sita na nne. Jambo zuri na heshima kwa nchi yetu, barabara za mwendokasi kwa Afrika Mashariki ni Tanzania pekee,” amesema Dk Nchimbi.

Aidha, mwendokasi kwa sasa utaendeshwa kwa ubia kati ya Serikali itakayojenga miundombinu na uendeshaji kwa maana ya mabasi itaachiwa sekta binafsi.

Kuhusu vivuko, mgombea mwenza huyo ameahidi kuwa serikali ya CCM itapanua maegesho kwenye kivuko cha Kigamboni.

“Mgombea ubunge (Sanga) ameongelea vivuko ambavyo vinasaisia maisha ya wananchi, vitakuwa vinatengenezwa haraka, mimi pia familia yangu inaisha Kigamboni kwa hiyo shida yenu ni shida yangu,” anasema Dk Nchimbi.

Hii ni moja ya changamoto ambayo si wagombea ubunge pekee waliyoiibua bali hata mratibu wa kampeni za CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, Mary Chatanda ameigusia na kuomba msukumo wa haraka.

Chatanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania wa CCM, katika mkutano wa Jimbo la Segerea anasema wanawake hawana tatizo kukipa ushindi chama hicho, lakini wanaomba maji.

Bonnah naye aligusia changamoto hiyo akisema kama hataizungumza wananchi wake hawawezi kumwelewa.

Akizungumza katika mkutano huo, mkazi wa Tabata, Mary Msafiri amesema; “Maji baba ni changamoto kubwa, kuna wakati yanatoka usiku wa manane, sasa tuache kulala tuanze kuchota maji. Tunaomba sana hili waliangalie kwani tunateseka sana.”

Akiwa Kigamboni Nchimbi ameahidi wakipatiwa ridhaa Serikali itaboresha upatikanaji wa maji kwa kuanzisha vyanzo vipya ili wananchi wa Kigamboni wapate huduma hiyo.

Pia, watahakikisha changamoto ya maji katika Wilaya ya Ilala na Jimbo la Segerea inabaki kuwa historia.

Profesa Kitila na Silaa mbali ya kuzungumza changamoto ya barabara, wamegusia umuhimu wa kujengwa ama kukarabatiwa masomo ili wafanyabiashara na wananchi wa maeneo hayo waneemeke na Serikali yao.

Profeasa Kitila ambaye pia ni Waziri wa Mipango na Uwekezaji alisema Ubungo ina jumla ya biashara 8998 kutoka 4220 zilizokuwepo mwaka 2020 na kuomba ujenzi wa masoko mapya.

Silaa naye amesema Gongo la Mboto na Kivule ni maeneo yanakuwa kwa kasi na mahitaji ni makubwa hivyo wakamwomba Dk Nchimbi baada ya uchaguzi kumsaidia Rais Samia ili masoko yapatikane.

Akijibu changamoto hizo, Dk Nchimbi amesema katika miaka mitano ijayo, wanakwenda kurasimisha biashara ndogondogo ili wafanye kihalali na kuwawezesha kupata mikopo kusudi wafanye bishara zenye.

“Kujenga na kukarabati masoko mapya 13, nimeambiwa watu wanakwenda sana Mlimani City, kituo cha Kimataifa cha Afrika Mashariki kwa sababu ya miundombinu mizuri, tumesema miundombinu hii inapaswa kuwa kwenye masoko mengine ili watu wayapende,” amesema Dk Nchimbi.

Kuhusu masoko yaliyoombwa na Silaa, Dk Nchimbi amesema kwa miaka mitano ijayo wakipatiwa ridhaa, wataboresha masoko pia.

Mbali ya Dk Nchimbi kuelezea mikakati ya miaka mitano ijayo kwenye sekta mathalani za afya na elimu, amebainisha mafanikio ya miaka mitano ya utawala wa Samia.

Amesema miaka mitano iliyopita amefanya kazi kubwa ya maendeleo, amekuwa kinara Afrika Mashariki lakini amelinda heshima ya wanawake.

Ametolea mfano, miaka mitano iliyopita, Zahanati zilikuwa 4,838 sasa ziko 7,732. Vituo vya afya vilikuwa 626 sasa 1,276 na Hospitali za Wilaya za Halmashauri zimefikia 293 kutoka

Dk Nchimbi anasema wakati Rais Samia anashika usukani wa kuongoza nchi, mikoa iliyokuwa na mashine za CT Scan zilikuwa tatu, lakini sasa zimefungwa katika mikoa 26:”Nani kama Samia?”

Katika sekta ya elimu, Dk Nchimbi ansema shule za msingi zilikuwa 18,099 sasa zimefikia 2,8099, za sekondari zilikuwa 5,124 lakini sasa zimefika 6,488.

Amesema uwezo wa uzalishaji umeme ulikuwa megawati 1602 sasa zinazalishwa megawati 3078, majisafi na salama mjini ilikuwa asilimia 84 leo asilimia 90, vijijini ilikuwa asilimia 70 na sasa ni asilimia 80.

“Haya ni baadhi ya mafanikio ya kitaifa na hii ndiyo inatupa ujasiri wa kuja tena mbele yenu kuwaomba mmchague Mama Samia kwa kura nyingi na za kishindo,” amesema Dk Nchimbi.