Morogoro. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ameahidi kushughulikia na kuleta suluhu ya kudumu ya migogoro ya muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji inayowasumbua wakazi wa Mikumi moani Morogoro na maeneo mengine nchini, endapo atapewa ridhaa ya kuongoza nchi.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni Uliofanyika leo Jumatano Oktoba Mosi, 2025 katika Kata ya Ulaya, Mikumi, Mwalimu amesema kumaliza migogoro hiyo ni moja ya dhamira yake kuu akisisitiza kuwa Chaumma kimejipanga kuleta suluhisho la kudumu kwa changamoto hiyo ambayo imekuwa ikigharimu maisha ya watu na kupotea kwa mifugo.
“Kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji ni dhamira ya kweli. Chaumma tumejipanga kumaliza jambo hili kwa kuwa hakuna faida kwa Taifa. Mkinichagua, dhamira hiyo ninayo. Sera yangu inalenga watu walime na kufuga kwa amani. Tunahitaji kuwekeza kwenye viwanda vya mazao na ngozi,” amesema Mwalimu.
Hata hivyo, ameonyesha kusikitishwa na hali ilivyo katika maeneo kama Mikumi, ambako migogoro ya ardhi imekuwa sugu kwa miaka mingi bila hatua madhubuti kuchukuliwa.
“Ng’ombe anakula nyasi, sasa inakuwaje wafugaji wanafukuzwa maeneo yenye malisho? Nikichaguliwa, ndani ya siku 100, nitaanzisha Tume Maalum ya Mapitio ya Matumizi ya Ardhi itakayoshughulikia migogoro hii na kupendekeza suluhisho la kudumu,” amesema.
Pamoja na hilo, amepinga vikali mipango ya kutenga maeneo ya hifadhi inayowaondoa wananchi walioko karibu na maeneo hayo, akisema hatua hiyo haizingatii maslahi ya wananchi.
“Matatizo haya yanasababishwa na ukosefu wa utashi wa viongozi. Chaumma iko tayari kupitia upya mpango huo. Tutasitisha mara moja mipango isiyo na tija ya kutenga hifadhi kwa njia inayowaumiza wananchi,” ameongeza.
Pia, ameahidi serikali yake itahakikisha wananchi wanaoishi karibu na hifadhi za Taifa wananufaika moja kwa moja, hatua ambayo itasaidia kupunguza ujangili.
Imani Mzude, Mgombea ubunge wa Mikumi, amesema jimbo hilo lina rasilimali nyingi lakini wananchi wake wamenyimwa fursa ya kunufaika nazo, hususan vijana ambao wengi wao ni wajasiriamali wanaojitahidi kujikwamua kimaisha licha ya ukosefu wa mitaji na ajira.
“Vijana wengi hawapewi mikopo kutunisha misuli ya mitaji yao, vijana wako hoi mtaani na hawana ajira.”amesema
Amesema endapo atapewa ridhaa ya kuwa mbunge, atapambana na changamoto hizo kwa kuhakikisha ndani ya miaka mitano anasambaza pikipiki aina ya bodaboda kwa vijana, ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi.
Kuhusu, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Mzude amesema hifadhi hiyo ni rasilimali muhimu kwa wananchi wa jimbo hilo, lakini hadi sasa hawajafaidika nayo kwa namna yoyote.
“Hatujui hata wananufaikaje nayo ilhali iko jirani nasi,” amesema
Aidha, Mzude ametaja migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji kama moja ya changamoto kubwa, akidai kuwa viongozi waliopo ndio chanzo cha migogoro hiyo kwa kuitumia kisiasa.
“Ardhi ya Kilosa imepingwa; watu wanauana lakini hakuna anayesimamia kutatua matatizo haya,” amesema.
Kwa upande wa miundombinu, Mzude amesema wananchi wa Mikumi wanakabiliwa na changamoto ya vivuko vya madaraja, hasa wakati wa mvua ambapo wanashindwa kufika upande wa pili kuchukua mahitaji muhimu.
“Nimekuwa nikifikisha taarifa kwa viongozi wa juu, lakini hakuna utekelezaji. Nikichaguliwa nitahakikisha suala hili linapewa kipaumbele,” ameahidi.
Akizungumzia sekta ya kilimo, amesema wakazi wengi wa Mikumi wanajihusisha na kilimo cha mazao kama mbaazi, lakini wanakosa soko la uhakika na viongozi hawachukui hatua.
“Wananchi wamegeuzwa machizi, hawajui bei wala soko la mazao yao,” amesema.
Kwa upande wake, John Mrema Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa chama hicho, alihitimisha kwa kusema kuwa chama chao kimejipanga kuleta mageuzi ya kweli katika maeneo yenye changamoto kama Mikumi, endapo kitaaminiwa na wananchi.