KMKM yavuna Sh10.5 millioni, yaanza kuiwinda Azam kimataifa

MABAHARIA wa KMKM, wamefanikiwa kuvuna Sh10.5 millioni kutoka kwa Mkuu wa Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM), Azana Hassan Msingiri ikiwa sehemu ya kuipongeza timu hiyo kwa kuingia hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika.

KMKM imefuzu hatua ya pili ya michuano hiyo baada ya kuiondosha AS Port ya Djibouti kwa jumla ya mabao 4-2.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa KMKM, Hababuu Ali amesema pongezi hiyo imetoa ari na hamasa kwao kujipanga ili kufanya vizuri hatua inayofuta.

Wakati kikosi cha Mabaharia kikipokea pongezi hizo, kimeanza maandalizi kuelekea mechi ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Azam inayotarajiwa kuchezwa kati ya Oktoba 17 na 19, 2025, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

MABA 01


Hababuu amesema anawafahamu wapinzani wao lakini zote ni timu hivyo lengo ni kupambana kwa kuvuka na kwenda makundi.

Ameeleza kuwa, watazitumia mechi za Ligi Kuu Zanzibar kukijenga kikosi hicho na kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika mechi za raundi ya kwanza ili kuhakikisha wanaitoa Azam nje ya mashindano hayo.

Hababuu amesema, licha ya wachezaji kuwa na ugeni wa mashindano ya kimataifa lakini wanacheza kwa mipango kupata matokeo ya kuvuka kila hatua.

“Hatukucheza vizuri raundi ya awali kwa sababu ya ugeni wa wachezaji katija mashindano haya, wengine hawajawahi hata kucheza Ligi Kuu, tulilazimisha matokeo na tumefanikiwa,” amesema Hababuu.

MABA 02


Amefafanua kuwa siri ya mafanikio hayo ni umoja wa viongozi wa kikosi hicho na kila mmoja kufanyakazi yake ipasavyo.

Amesema, anaamini wapinzani wao wamejipanga kufuzu hatua ya makundi na amefurahishwa na baadhi ya wachezaji walioonesha kiwango kikubwa katika mechi hizo ikiwemo Kipa Nassor Abdalla, Martin Ather na Arafat Farid.

Kocha huyo, ameendelea kulia na mashabiki kwa kuonyesha kejeli za kuwazomea wachezaji wanapopoteza mechi katika mashindano ya kimataifa jambo ambalo lilionekana Mlandege ilipocheza dhidi ya Ethiopian Insurance.

Amesema, tabia hizo hazijengi timu badala yake zinaibomoa na kuwavunja moyo wachezaji ambao wamefanya kazi yao ipasavyo.