WANAJESHI wa JKT Tanzania, wameambulia pointi moja kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa leo Oktoba 1, 2025 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya matajiri wa Chamazi, Azam FC.
Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 43 kupitia kwa kiungo Feisal Salum ambaye alimalizia kwa kichwa mpira uliopigwa na Himid Baraket.
Licha ya mechi kuwa na ushindani na kila timu kupambana kuhakikisha inapata bao, lakini Azam ambayo ilikuwa inaongoza iliendelea kuzuia mashambulizi ya JKT Tanzania.
Hata hivyo, wakati ambao baadhi ya mashabiki wa Azam waliamini mechi imeisha na wanaondoka na pointi tatu, Paul Peter Kasunda akaharibu shughuli hiyo baada ya kusawazisha bao dakika ya 90 kwa kichwa.
Kasunda kwenye mechi tatu alizocheza msimu huu amefikisha mabao mawili, na leo ameondoka na tuzo ya mchezaji bora wa mechi ikiwa ya pili baada ya kwanza kuchukua dhidi ya Mashujaa.
Matokeo hayo yanaifanya JKT Tanzania kuwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikikusanya pointi tano ambazo ilizipata baada ya kutoa sare ya 1-1 na Mashujaa, ikapata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union ya Tanga na sare ya leo.
Mara ya mwisho Azam kucheza kwenye uwanja huo dhidi ya JKT Tanzania, ilikuwa Agosti 24, 2024 ambapo timu hizo hazikufungana.