Coastal yamtimua Kocha, mrithi wake huyu hapa

Coastal Union imefikia uamuzi wa kuachana na Kocha Ali Ameir baada ya kuinoa katika mechi tatu tu za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Ameir ameinoa timu hiyo katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons, JKT Tanzania na Dodoma Jiji.

Mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika mechi hizo, unaonekana kuchangia kufupishwa kwa mkataba baina ya pande hizo mbili.

Taarifa iliyotolewa na Coastal Union leo Jumatano, Oktoba Mosi imefafanua kwamba mkataba wa kocha huyo umesitishwa kwa makubaliano binafsi.

“Uongozi wa Klabu ya Mpira wa Miguu ya Coastal Union umefikia makubaliano ya pande zote ya Kusitisha Kandarasi na Kocha Mkuu Ali Mohammed Ameir.

“Klabu inamshukuru Mwalimu Ali Mohammed Ameir kwa mchango wake uliotukuka kwa kipindi chote alichoiongoza Timu yetu.

“Uongozi wa Coastal Union utaujulisha umma juu ya Muundo na Uongozi Mpya wa benchi la Ufundi muda mchache ujao,” imefafanua taarifa ya Coastal Union.

Ameir alianza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons, akafungwa mabao 2-1 na JKT Tanzania kisha akafungwa mabao 2-0 na Dodoma Jiji FC.

Inaripotiwa kwamba timu hiyo ipo katika hatua za mwisho za kumalizana na Kocha Mohamed Muya kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Ameir.