Mfanyabiashara wa Dar akutwa ameuawa wilayani Makete

Njombe. Mfanyabiashara wa mazao Elia Juma Msabaha (27) ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam  amekutwa ameuawa wilayani Makete Mkoa Njombe.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 1, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga wakati akizungumza  na waandishi wa habari makao makuu ya Jeshi la Polisi mkoani humo.

Amesema Agosti 28, 2025 mfanyabiashara huyo aliondoka Dar es Salaam na kuelekea wilayani Makete kwa ajili ya kununua mazao alipofika huko Agosti 29, 2025 inadaiwa aliuawa na mtu aliyefahamika kwa jina la Khalfan Mbilinyi kwa kumpiga na kitu chenye ncha butu kwenye paji la uso.

“Alimuua kisha kuchimba na kumfukia nyuma ya ghala lake ya kuhifadhia mazao,” amedau Banga.

Amesema ndugu wa mfanyabiashara huyo walijaribu kufanya mawasiliano naye bila mafanikio na kufunga safari mpaka Wilaya Makete na kumtafuta bila ya mafanikio ya kumpata.

“Waliamua kufika kituo cha polisi wilayani Makete na kutoa taarifa ya kutoonekana kwa ndugu yao na jalada lilifunguliwa na uchunguzi ukaanza,” amesema Banga.

Amesema jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili ambao ni Khalfan Mbilinyi na Amasha Mbeilo dereva bodaboda na baada ya mahojiano ya kina Amsha Mbwilo alieleza kuwa kuna siku alimbeba Mbilinyi mpaka mkoani Mbeya.

Amedai huko walikwenda kutupa simu ya marehemu Msabaha ili asikamatwe na kupoteza ushahidi na baada ya askari kupata ushahidi huo walimkamata Mbilinyi alieleza ukweli kuwa marehemu Msabaha alifika kwake na kununua mazao.

Banga amedai Mbilinyi aliona marehemu Msabaha alikuwa na fedha zaidi ya Sh4 milioni na kuingiwa na tamaa na kwakuwa alikuwa anadaiwa benki akaamua kumpiga na kitu butu usoni.

Amedai baada ya maelezo hayo alikwenda kumfukia marehemu huyo na kueleza simu ya marehemu huyo alikwenda kuitupa Uyole  na anaweza kwenda kuionyesha.

Amesema askari wakiwa na mtuhumiwa wakielekea huko Uyole wakiwa na gari walipata pancha ndipo mtuhumiwa huyo alikurupuka na kuanza kukimbia ndipo askari walipiga risasi hewani kumtahadharisha.

Amesema lakini mtuhumiwa huyo alikaidi na kulengwa risasi mguuni lakini ikampata karibu na kiunoni na kudondoka chini na kumchukua na kumpeleka hospitalini na kubainika kuwa amefariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi.

Amesema jeshi hilo linatoa onyo kwa baadhi ya wananchi wanaotanguliza tamaa kujipatia fedha au mali kwa kuongozwa na tamaa kinyume na sheria za nchi kwa sababu madhara yake ni makubea kwao na kwa nchi