NIKAIPOKEA ile simu huku nikiendesha gari nikijua fika kwamba kwa kachero kama mimi kitendo hicho kilikuwa kosa, lakini mapenzi ni kitovu cha uzembe. Nikakikumbuka kitabu cha Ngoswe.
“Hello baby…!”
“Hello. Habari yako?” Sauti ya Hamisa ikasikika kwenye simu. Ilikuwa kama muziki masikioni mwangu.
“Nzuri. Unaendeleaje?”
“Sijambo, sijui wewe?”
“Mimi nashukuru Mungu. Niambie…?”
“Leo niko ‘off’. Nimepumzika nyumbani,” akaniambia.
“Upo nyumbani?” nikamuuliza kama vile sikusikia vizuri.
“Ndiyo, niko nyumbani.”
“Basi ninakuja.”
Sikusikia sauti iliyoniambia ‘njoo au usije’, nikageuza gari hapo hapo.
“Unakuja sasa hivi?” Hamisa akaniuliza.
“Niko kwenye gari, ninakuja.”
Nikaona simu imekatwa. Nikaipiga tena.
Hamisa alipopokea nikamuuliza:
“Mbona umekata simu?”
“Si umesema unakuja?”
“Ndiyo, ninakuja.”
“Sasa simu ni ya nini tena?”
“Nimekuelewa.”
Nikakata mimi na kuongeza mwendo wa gari.
Baada ya nusu saa tu nikafika nyumbani kwa Hamisa. Nilikuwa na pupa na Hamisa. Msichana niliyempenda na aliyekuwa amenikasirikia alianza kuonyesha dalili za kuwa karibu nami.
Nilipobisha mlango wa nyumba yake, Hamisa alikuja kunifungulia. Akanikaribisha ndani.
“Karibu.”
Sauti yake ilikuwa ya adabu na nidhamu. Niliomba Mungu asibadilike tena na kuwa chui.
Nilikumbuka siku aliyonitimua nyumbani kwake. Ilikuwa hivi:
“Kwenda zako. Tafadhali Fadhil, ondoka uende zako. Mimi nataka kufunga mlango wangu.”
Hamisa akatazama saa yake ya mkononi kisha akaongeza:
“Nachelewa kazini.”
Nikaelekea kwenye mlango, mahali ambapo alikuwa amesimama. Kama vile hakutaka nimsogelee karibu, akatoka nje na kusimama kando ya mlango.
“Mbona unatoka?” nikamuuliza.
“Nataka kwenda zangu kazini,” akaniambia.
“Hamisa, nina mazungumzo na wewe. Niambie nikufuate saa ngapi kazini kwako?”
“Toka… toka… toka…!” akaniambia huku akisisitiza kwa mkono wake kuwa nitoke. Nikatoka.
Tangu Hamisa aliponifukuza nyumbani hapo siku ile, leo ndiyo nilikuwa naijua nyumba yake.
“Karibu ukae,” akaniambia huku akifunga mlango.
Nikakaa kwenye kochi, na yeye akaja kukaa kwenye kochi jingine. Sikupenda akae mbali nami lakini nilimvumilia.
“Mwenzako ninaumwa na kichwa, ndiyo maana nilikuwa nimelala.”
“Umemeza dawa?”
“Unajua mimi natibu wenzangu lakini ni mvivu sana wa kunywa dawa. Nilimeza vidonge tangu asubuhi.”
“Bado kinaendelea kuuma?”
“Kinauma upande mmoja lakini si sana. Halafu pia nasikia mafua.”
“Labda una malaria.”
“Mbona unaniombea maradhi, Fadhil!”
“Sikuombei maradhi, ila ninakujuza tu kwamba huenda una malaria.”
“Usiniombee bwana. Unajua naogopa sana kuumwa.”
“Kama wewe ni binadamu lazima uugue. Sasa utaishi vipi bila kuumwa?”
“Nitaenda kupima kesho nikienda kazini.”
“Nenda kapime, kama una malaria uanze dozi mapema.”
“Sawa.”
Nilishindwa kuendelea kuvumilia kukaa mbali na Hamisa. Nikainuka ili niende nikakae naye.
“Unakwenda wapi?” Hamisa akaniuliza kwa ukali kidogo. Sauti yake ya ukali haikunishtua. Nilikuwa naijua akili yake ilivyo.
“Nakuja kukaa hapo.”
“Kwani hapo kuna nini?”
“Naona tuko mbalimbali sana.”
Nikakaa kando yake.
“Nahitaji kukaa na wewe.”
“Nani amekupa ruhusa ya kukaa na mimi, Fadhil?”
Maswali yake ya ajabu ajabu pia nilikuwa nimeyazoea.
“Kwani nani amenipa ruhusa ya kuingia humu ndani?”
“Sasa ukipewa kidole, unataka kushika mkono?”
“Maana yake wewe ni wangu.”
“Bila maadili?”
“Maadili ninayo.”
Akaanzisha upuuzi wake:
“Maadili ya kumpenda Helena?”
“Hamisa, unaanzisha tena maneno!”
“Kwani Helena si mpenzi wako?”
Nikanyamaza na kutikisa kichwa kwa kusikitika.
“Nataka uniambie ukweli. Helena si mpenzi wako?”
“Nikwambie mara ngapi, Hamisa? Nimeshakwambia mara nyingi tu kwamba Helena ni mfanyakazi mwenzangu, lakini si mpenzi wangu.”
“Kwanini ulikuwa unamshikashika?”
“Nilimshikashika wapi?”
“Kwenye harusi ya dada yake.”
“Unajua, wakati mnacheza mnaweza kushikana bila hata kudhamiria. Ile haionyeshi kuwa tunapendana, ila inaonyesha kuwa tumekolea kucheza.”
“Si kweli.”
“Ni kweli, na sijui ni nani aliyekurushia ile video. Huyo ndiye mchonganishi kati yangu mimi na wewe. Bila shaka alikwambia na maneno mengi ya uongo ili kutugombanisha. Mimi najua uchumba wetu umewaudhi watu wengi, lakini bado nitakupenda hadi dakika ya mwisho.”
“Nakupa muda ujirekebishe, usirudie.”
“Nimeshapata fundisho, sitarudia tena.”
“Ukirudia nikufanye nini?”
“Kwanza sijakuelewa. Nikirudia nini?”
“Kuwa na Helena.”
“Helena sijawahi kuwa naye.”
“Kwenye ile video mlikuwa mnafanya nini?”
“Tulikuwa tunacheza.”
“Sasa nakwambia nisikuone naye tena!”
“Unamshuku bure msichana wa watu.”
“Iwe bure, iwe kwa pesa, nakwambia nisikuone naye tena! Tumeelewana?”
“Nimekuelewa.”
“Mimi simpendi na ninamchukia. Ninajua mnapendana, lakini ole wenu siku nikiwafuma!”
“Na hutatukuta hata siku moja kwa sababu hatujawahi kuwa pamoja. Wasiwasi wako tu.”
“Kama leo ni wasiwasi wangu, siku nikiwafuma utakuwa wasiwasi wako wewe na yeye.”
Kimoyomoyo nilijiambia kwamba Hamisa alikuwa amesharudi mikononi mwangu. Kilichobaki ni mikwara yake tu. Nikamwambia:
“Hamisa, tuache dhihaka. Niambie harusi yetu itakuwa lini?”
“Umekwenda mbali sana. Tuzungumzie ule uchumba kwanza.”
“Tuzungumzie kitu ambacho kipo. Wewe ni mchumba wangu.”
“Uchumba si niliuvunja na niliwaambia wazee wangu kwamba wewe si mchumba wangu tena, na akitokea mchumba mwingine waniambie.”
Sikujali kama yalikuwa maneno ya mzaha au ya kweli, lakini yalinigutusha.
“Sasa kwanini uliwaambia hivyo?” Nikamuuliza.
“Ni kwa sababu ya vile vituko vyako. Niliona hutofaa kuwa mume wangu. Sasa ni lazima nifikirie cha kuwaambia tena wazee wangu ambao wanajua siko na wewe.”
“Hamisa, uliharibu sana…”
“Ni kwa sababu yako!”
“Sasa utawaeleza nini?”
“Nitafikiria cha kuwaambia.”
“Waambie leo.”
“Una haraka ya nini, Fadhil?”
“Ndoa. Nataka nikuweke ndani.”
“Uniweke ndani halafu unitese na wanawake zako!”
“Amini Mungu. Mimi sina mwanamke mwingine zaidi yako, mchumba wangu.”
“Nidanganye tu, lakini ujue mwisho wa muongo ni kuja kuumbuka!”
“Wala sitaumbuka kamwe. Mimi mwenyewe najitambua kwamba kwako ni mkweli, na ninachokwambia ni kweli tupu.”
Nilihisi kama vile maneno yangu yalikuwa yakimuingia Hamisa. Mtazamo wake sasa ulikuwa umebadilika. Alikuwa akinitazama kwa pozi na kwa macho ya haiba.
Nikaendelea kumwambia:
“Nilikuwa silali katika kipindi chote ulichonisusia. Najua ulifanya hivyo kwa sababu ulijua nakupenda.”
Hamisa aliendelea kunyamaza akinitazama.
“Nataka uharakishe kuwaambia wazazi wako.”
“Nikipata utulivu nitazungumza nao.”
“Lini?”
“Hata kesho naweza kuzungumza nao.”
“Sawa. Zungumza nao na uwajulishe kwamba mimi niko tayari kwa harusi.”
“Nitawajulisha.”
Kwa vile moyo wangu ulikuwa umeridhika, nikamwambia Hamisa: “Nitakuja kukuchukua usiku tukale chakula cha usiku Nyumbani Hotel.”
“Utanifuata saa ngapi?”
“Niambie wewe nikufuate saa ngapi.”
“Njoo saa moja.”
“Sawa. Nitakufuata saa moja.”
Nikamshumu midomoni kisha nikainuka.
“Nakwenda zangu.”
Hamisa naye akainuka.
“Ngoja nikutoe.”
Alinisindikiza hadi kwenye mlango. Nikatoka na kujipakia kwenye gari. Alibaki mlangoni hadi nilipoliondoa gari.
Hamisa aliponiita nyumbani kwake nilikuwa na furaha, lakini wakati ule ninaondoka furaha yangu ilikuwa imezidi.
Kikubwa kilichonipa furaha ni kurudisha uhusiano wangu na Hamisa.
Katika siku chache tulizoachana nilijihisi nimekonda kwa mawazo yake. Sasa niliamini kuwa mwili wangu utarudi.
Nilirudi ofisini kwangu, nikaliacha gari nje ya kituo na kuingia kituoni.
Mara tu nilipoingia ofisini mwangu, niliyaacha mawazo ya Hamisa. Nikayapeleka mawazo yangu kwa Thomas Christopher, kijana ambaye amekuwa akisumbua akili yangu vilivyo.
Nilikaa kwenye kiti nikajiuliza kama kweli Thomas ndiye aliyekuwa akiwanyonga kina Unyeke.
Atakuwa ni mfu wa aina gani? Nikajiuliza.
Haidhuru palikuwa na hoja kwamba alikuwa analipa kisasi, lakini ni mfu wa aina gani anayelipa kisasi?
Nikatoa simu yangu na kujaribu kuipiga ile namba ya Thomas, ambayo mara zote nilipojaribu kuipiga haikupatikana. Nilipoipiga kwa mara ile pia haikupatikana.
Bado Watatu – 46 | Mwanaspoti
