Watatu wakamatwa tuhuma kushambulia mabasi, vituo vya mwendokasi

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za uharibifu miundombinu ya mabasi ya mwendokasi.

Taarifa ya kukamatwa watu hao imetolewa usiku wa kuamkia leo Alhamisi Oktoba 2,2025 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, ikiwa ni saa chache tangu kusambaa kwa video zikionyesha baadhi ya mabasi hayo yakiwa yamevunjwa vioo.

Mabasi hayo yalishambuliwa kwa mawe na watu wasiojulikana usiku wa Oktoba Mosi, 2025 katika eneo la Magomeni Usalama.

Taarifa ya Muliro imeeleza watu watatu wamekamatwa kwa tuhuma za kuharibu miundombinu ya mabasi hayo.

“Kati ya saa mbili usiku maeneo ya Gerezani Kariakoo, Magomeni Mapipa, Magomeni Usalama na Magomeni Kagera kwenye vituo vya mabasi ya mwendokasi baadhi ya mabasi yalirushiwa mawe na baadhi vioo vyake kuvunjwa.”

“Watuhumiwa watatu walikamatwa, wanahojiwa na chanzo cha matukio hayo kinafuatiliwa,” imeeleza taarifa ya Muliro.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa watuhumiwa wengine waliohusika katika tukio hilo wanatafutwa huku ikionya watu kutojihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwemo ya kuharibu miundombinu ya umma.