Mtwara. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amewataka Watanzania kuepuka ubaguzi wa kikabila na kidini katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa madhara yake ni makubwa na yanaharibu mshikamano wa kitaifa.
Akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM mjini Mtwara, Wasira amesema Tanzania imejengwa juu ya msingi wa umoja, ambao umewawezesha wananchi kuishi kwa mshirikiano bila kujali tofauti za makabila na dini.
“Ubaguzi wa makabila na dini ni tatizo kubwa katika nchi nyingi za Afrika. Hapa Tanzania tumejenga taifa lenye umoja. Hamuwezi nyote mkawa kabila moja, lakini mnaishi pamoja kwa mshirikiano. Hivyo mtu akija kuwambia usimpigie fulani kwa sababu ya kabila au dini, mwambie hana uelewa wa historia ya nchi yetu,” amesema Wasira.
Akitolea mfano viongozi wa kitaifa waliowahi kuiongoza Tanzania, Wasira amesema mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan na watangulizi wake waliungwa mkono na wananchi si kwa sababu ya kabila wala dini zao, bali kwa sifa na uwezo wa kuongoza.
“Nani anajua kabila la Rais Samia? Mimi sijui, najua anatoka Kizimkazi, na hicho ni kijiji siyo kabila. Lakini ndiye Rais wa Watanzania wote. Vile vile tulimchagua Mwalimu Nyerere si kwa sababu alikuwa Mkristo au Mzanaki, bali kwa sifa zake za uongozi. Hali kadhalika tulimchagua Mwinyi, Mkapa na Kikwete, hatukutazama kabila wala dini zao,” amesisitiza.
Wasira ameongeza kuwa mtu anayehubiri ubaguzi ni sawa na kuleta sumu katika taifa.
“Nyinyi msionje sumu, maana sumu haionjwi, ukiionja unaweza kufa. Tanzania ni nchi ya umoja na mshikamano. Afrika nzima wanatushangaa namna tulivyoweza kuwaunganisha wananchi wa dini na makabila tofauti kuishi kwa amani,” amesema.
Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara, Saidi Nyangedi, amesema chama hicho kitaendelea kusaka kura za kishindo kwa mgombea urais, Samia Suluhu Hassan pamoja na wagombea ubunge na udiwani.
Amesema katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wake, Samia ameleta maendeleo makubwa yanayoshuhudiwa Mtwara na mikoa mingine nchini.