Maswa. Mwenyekiti Mstaafu wa Vyama vya Siasa nchini, John Shibuda ametoa wito kwa wazee kote nchini kuchukua nafasi yao kama mabalozi wa amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.
Pia, Shibuda ambaye pia ni mmoja wa wazee wa heshima katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, amebainisha kuwa wao ndio nguzo kuu katika kuimarisha maelewano ndani ya familia na jamii kwa ujumla, hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linakabiliwa na changamoto za mivutano ya kisiasa na kijamii.
Shibuda amesema kuwa kwa busara, uzoefu na heshima waliyonayo katika jamii, wazee wana uwezo mkubwa wa kuzuia migogoro, kudhibiti kauli za chuki na kusaidia kujenga jamii inayojali maadili, uvumilivu na kuheshimu tofauti za mawazo.
“Wazee ni kama dira ya jamii. Tunapaswa kutumia nafasi hiyo kuhimiza mazungumzo ya kujenga, siyo kubomoa. Tuwaongoze vijana na familia zetu katika njia ya amani, siyo kutumiwa kusambaza chuki au taarifa za kupotosha,” amesisitiza.
Akizungumza leo Oktoba 1, 2025 katika kuadhimisha siku ya wazee duniani katika mkutano wa wazee wa mkoa huo uliofanyika wilayani Maswa, Shibuda amesema kuwa migogoro mingi ya kisiasa nchini huanzia katika mazungumzo ya kila siku majumbani, ambako mara nyingi huzaliwa kwa misingi ya chuki, upotoshaji au ushabiki usio na mipaka wa kisiasa.

“Sisi wazee pamoja na kina mama, ndio nguzo kuu za familia. Tuna jukumu kubwa la kuhakikisha tunalinda amani kuanzia ngazi ya familia. Tusikubali kuwa chombo cha kusambaza taarifa za uongo au za kuchochea chuki, iwe mitandaoni au kwenye vijiwe vya mazungumzo,” amesema Shibuda.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila mzazi na mlezi kuwalea watoto katika misingi ya uzalendo, upendo kwa taifa, na kuheshimu tofauti za kisiasa bila kuvuka mipaka ya utu.
“Tuwe walimu wa kuhimiza vijana na watoto wetu kupenda nchi yao kwanza kabla ya vyama vyao. Kauli za upotoshaji na uchochezi ambazo zinaweza kusababisha vurugu au kuvuruga amani ya taifa, tuzikemee waziwazi na kwa uthabiti,” ameongeza.
Kauli ya Shibuda imekuja wakati ambapo mijadala ya kisiasa nchini inaendelea kushika kasi, huku baadhi ya maeneo yakishuhudia migawanyiko ya kijamii inayochochewa na taarifa potofu na siasa za chuki.
Pia, amehimiza viongozi wa mila, dini na kijamii kushirikiana kwa karibu katika kuendeleza maadili, mshikamano na maelewano ya kitaifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri Mkoa wa Simiyu, Lameck Mkilila amesema kuwa jamii inapaswa kutambua kuwa uchaguzi ni tukio la kupita na si sababu ya kuharibu undugu au kuvunja mshikamano wa kijamii.
Amesema kuwa uzoefu wao wa maisha umewajengea hekima ya kuona kuwa hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana bila kuwepo kwa mazingira ya amani na utulivu pia alionya kuwa chaguzi mara nyingi huwa na viashiria vya migawanyiko ya kijamii endapo hakuna tahadhari, busara na maadili katika kuendesha shughuli za kisiasa.

Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha (Mwenye miwani) akifuatilia mkutano wa Wazee wa mkoa huo uliofanyika wilaya ya Maswa. Picha na Samwel Mwanga
“Tanzania ni yetu sote. Uchaguzi ujao ni nafasi ya kidemokrasia, siyo vita. Tuwahimize vijana wetu, vyama vyetu na wagombea wote wajiepushe na lugha za uchochezi au vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani tuliyoijenga kwa miaka mingi,” amesema.
Kwa upande wake, Mary Mashala, mzee kutoka Wilaya ya Meatu, amesema huu ni wakati muafaka kwa viongozi wa dini kuendelea kuombea taifa, ili liendelee kuwa na amani, utulivu na mshikamano, hasa katika kipindi ambacho taifa linakumbwa na changamoto mbalimbali za kijamii na kisiasa.
Amesisitiza kuwa maombi pekee hayawezi kutosha iwapo jamii haitajifunza kusameheana, kuvumiliana na kuangalia masilahi mapana ya taifa badala ya kuendekeza masilahi binafsi au ushabiki wa kisiasa.
“Sisi wazee tunasisitiza amani, mshikamano na kuliomba Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola kuwa makini dhidi ya watu au makundi yatakayojaribu kuvuruga utulivu wa nchi kupitia propaganda au uchochezi,” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha ametoa pongezi kwa wazee kwa kuonesha mfano wa kuigwa wa kizalendo na akawataka vijana kufuata nyayo hizo kwa kuepuka mihemko isiyofaa.
“Amani si jambo la bahati mbaya. Ni matokeo ya juhudi, uvumilivu, na hekima ya wananchi wake. Tunahitaji kila mmoja wetu kuwa mlinzi wa amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025,” amesema.