Msiwatishe wachezaji kwenda Yanga, Simba

MCHEZAJI anapotoka timu nyingine ya hapa nchini na kujiunga na Yanga au Simba  kumekuwa na maneno mengi ya kuonyeshwa kwamba anaenda katika hizo klabu mbili kusotea benchi.

Lengo hapo ni kutaka kuaminisha kwamba mchezaji anatakiwa kubaki katika timu ya daraja la kati au la chini kiuchumi ili apate nafasi ya kucheza na sio kufuata hela tu kwenye timu kubwa.

Lakini kwa niaba ya kijiwe, tunawahimiza wachezaji wasijaribu kuzidengulia ofa zinapokuja za kutakiwa kusajiliwa na Simba, Yanga au Azam na wasitishwe na hizo dhana kwamba wanakwenda kuua vipaji vyao.


Wachezaji wetu wakumbuke kwamba katika klabu hizo kubwa wanaenda kulipwa mishahara mikubwa na stahiki nyingine tena kwa wakati kulinganisha na hizo klabu nyingine ambazo nyingi hali zao za kiuchumi ni duni.

Ndugu zangu hawa wachezaji ni tegemeo kwenye familia zao na wamezungukwa na idadi kubwa ya watu ambao wanaishi kwa kutegemea vipato ambavyo wanavipata kupitia mpira wa miguu hivyo kuendelea kukaa katika klabu yenye maisha ya kuungaunga kisa unapata nafasi ya kucheza sio jambo sahihi.

Lakini kitu kingine ni kwamba katika hizo timu kubwa wachezaji wanapata huduma nyingine zinazohitajika kwa kiwango kizuri na ndani ya muda zinapohitajika tofauti na hali ilivyo katika hizo timu zisizo na misuli ya kiuchumi.

Safari za mbali na ndefu wanatumia usafiri wa ndege wakati timu zetu nyingine ni mwendo wa basi kukatiza katika milima na mabonde, mvua na jua ili wafike katika kituo cha mchezo.


Na isitoshe hizo timu za Yanga, Azam na Simba zina mabenchi ya ufundi yenye wataalam wa viwango vya juu kuliko timu nyingi za Ligi Kuu hivyo hata kama mchezaji hapangwi katika kikosi, mazoezini anakutana na darasa bora zaidi la makocha na wasaidizi wengine.

Tujitahidi kupunguza pengo la kiuchumi baina ya hizo timu kubwa na nyinginezo ili tuwe na timu nyingi zinazoweza kutoa huduma nzuri na bora na kuwashawishi wachezaji kuzichezea na kukataa kuzitumikia timu kubwa.