KWA timu ya Fountain Gate, kile ambacho imekifanya msimu uliopita, imekirudia tena ambacho ni kuanza msimu huku ikiwa haina kikosi kilichokamilika.
Wanacheza Ligi Kuu msimu huu wakiwa na kikosi cha wachezaji 13 tu na labda wa ziada ni wale wa kikosi chao cha vijana chini ya umri wa miaka 20.
Sababu ya Fountain Gate kutumia idadi ndogo ya wachezaji katika Ligi Kuu msimu huu ni kuchelewa kuingiza majina ya wachezaji hao katika mfumo wa kimataifa wa usajili wa FIFA hivyo wale wapya hawajaingia.
Na chanzo cha hayo yote ni madeni ambayo timu hiyo ilikuwa nayo yaliyotokana na uvunjaji wa mikataba ya baadhi ya wachezaji waliochezea siku za nyuma ambao hawakuridhika nao na hivyo kukimbilia FIFA.
Hata hivyo, Fountain Gate imeshalipa madeni hayo na hivyo FIFA ikawaondolea adhabu yao lakini hilo limekuja katika kipindi ambacho tayari dirisha la usajili kwa hapa Tanzania limeshafungwa hivyo wanapaswa kusubiri hadi dirisha dogo ndipo waingize hayo majina.
Kijiwe kinaishauri Fountain Gate iwe na utulivu kwa sasa inapopitia katika kipindi hiki kigumu kwani hiyo ndio itakuwa silaha muhimu kwao kuwawezesha kurudi katika mstari baada ya kuanza vibaya Ligi Kuu.
Wachezaji na maofisa wake wa benchi la ufundi wanapaswa kuwa na uvumilivu wa hali ya juu katika muda huu uliobakia kabla ya dirisha dogo kwa vile ni mfupi. Wajitume kuhakikisha timu angalau inavuna pointi kadhaa kipindi hiki ili hadi pale itakaporuhusiwa kusajili, isiwe imeachwa mbali sana kipointi.
Wakiwa pamoja na kila mtu akawajibika kwa nafasi yake, Fountain Gate haiwezi kuwa katika hali mbaya na nafasi isiyoridhisha katika msimamo wa Ligi Kuu msimu huu huku ikiwa imetoka kuponea chupuchupu katika msimu wa 2024/2025.
Uzuri dirisha dogo la usajili litafunguliwa Desemba 15 mwaka huu. Haliko mbali sana kwa vile kutakuwa na mapumziko ya kupisha mechi za timu za taifa lakini pia kuna AFCON 2025 hivyo hadi dirisha litakapofunguliwa hawatakuwa wamecheza mechi nyingi.