Raundi tatu za Ligi Kuu Bara,Fountain Gate hadi aibu

JANA Oktoba 1, 2025, raundi ya tatu ya Ligi Kuu Bara ilihitimishwa kwa kuchezwa mechi mbili, Simba ikiifunga Namungo mabao 3-0, huku JKT Tanzania ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam.

Wakati raundi ya tatu ikikamilika, Fountain Gate imetia aibu, si kwa kuwa na idadi ndogo ya wachezaji kutokana na changamoto ya usajili iliyokumbana nayo, bali ni matokeo ya uwanjani.

Timu hiyo iliyoponea kushuka daraja msimu uliopita kwa kushinda mechi za mtoano wa pili dhidi ya Stand United, hadi sasa ndiyo timu pekee isiyoambulia pointi hata moja.


Mbali na kushindwa kukusanya pointi, pia timu hiyo katika mechi tatu ilizocheza haijafunga bao huku yenyewe ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita, ikiwa ndiyo iliyoruhusu mabao mengi zaidi. Ina wastani wa kuruhusu mabao mawili kila mechi.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Fountain Gate, vinara wa msimamo wa ligi, Simba SC imekuwa na ushindi wa asilimia mia kufuatia kushinda mechi mbili ilizocheza sawa na Singida Black Stars. Tofauti yao ni mabao ya kufunga, zote zikiwa hazijaruhusu nyavu kutikiswa. Simba imefunga mabao sita ikiwa na wastani wa kufunga mabao matatu kila mechi, Singida Black Stars inayo mawili, wastani ni bao moja kwa mechi.


Ni timu tatu pekee hazijaonja ladha ya ushindi hadi sasa, ukiiweka kando Fountain Gate ambayo haina pia pointi yoyote, zingine ni TRA United na Pamba Jiji lakini kila moja ina pointi mbili kufuatia sare ilizopata.

Hii ikiwa ni raundi ya tatu imemalizika huku timu sita pekee zikiwa zimeshuka dimbani mara mbili, jumla ya mechi 22 zimechezwa na kufungwa mabao 36, ikiwa ni wastani wa bao 1.6 kwa mechi.

Wastani huo wa ufungaji ni mdogo kulinganisha na msimu uliopita

2024-2025 ambapo katika raundi tatu za kwanza, licha ya kuchezwa mechi nyingi 24, pia yalifungwa mabao mengi 42 kwa wastani wa bao 1.8 kwa mechi.