Dar City, DB Lioness zaishika fainali DBL

MECHI za pili za fainali ya Ligi ya Mpira wa Kikapu Dar es Salaam (BDL) zilipigwa juzi Jumanne na Dar City na DB Lioness ziliendeleza ubabe kwa kuzifunga JKT na JKT Stars, kwenye viwanja vya EDonbosco, Upanga.

Katika mchezo wa wanaume Dar City dhidi ya JKT, ulikuwa wa kuvutia na kutokana na ushindani wa pande zote mbili huku JKT ikitawala na kuamsha shangwe uwanjani licha ya kupoteza mchezo huo wa pili kati ya mitano ya kumsaka bingwa wa michuano hiyo.

City ilishinda pointi 71-64, na ilikuwa inasubiri mchezo wa tatu uliopigwa jana Alhamisi na 4endapo itashinda ingetangazwa bingwa wa mwaka 2025.

Awali katika fainali ya kwanza, City ilishinda pointi 68-44 na kuongeza mzuka wa kushinda mchezo wa pili.

Katiak fainali hiyo ya pili, JKT ilizishika robo zote  nne, huku City ikicheza kwa tahadhari kubwa ikiongozwa na nyota wao kama Clinton Best,  Sharon Ikedigwe (Nigeria ), Jamel Marbuary (Marekani) walioshirikiana na wazawa Hasheem Thabeet, Amin Mkosa, Fotius Ngaiza na Ally Abdallah.

City iliongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 23-14, robo ya pili JKT ikaongoza kwa pointi 27-18.

Hadi mapumziko, zilikuwa zimefungana pointi 41-41 na robo ya tatu City ikaongoza  kwa pointi 12-9,  huku ya nne ikapata 18-14.

Katika mchezo huo, Abdallah  alifunga pointi 21, akifuatiwa na  Marbuary aliyefunga 21.

Kwa upande JKT Omary Sadiki alifunga 15, akifuatiwa na Saidi Shabani aliyefunga 13.

Kwa upande wa DB Lioness, sasa ilikuwa ikisubiri mchezo wa tatu jana Alhamisi ili kutetea ubingwa wake wa WBDL.

Tayari imeshinda mechi mbili kati ya tano za kusaka ubingwa na katika mchezo wa juzi Jumanne, iliifunga JKT Stars kwa pointi 68-48 baada ya awali kushinda 61-17.

Akiongea na Mwanasposti kocha wa JKT, Alfred Ngalalija alisema kupoteza kwa timu yake kunatokana na kukosekana kwa baadhi ay nyota wake muhimu.

Alisema nyota wake hao wako mkoani Tabora, na timu ya JKT Stars inayoshiriki mashindano  taifa ya netibali, akiwamo Jesca Ngisaise, Grance Innocent, Wade Jaha na Sara Budodi.

Katika mchezo huo, JKT Stars ilikuwa na wachezaji sita, watano wakiwa uwanjani na mmoja wa akiba.

Timu zote zilimaliza robo  ya kwanza kwa kufungana pointi 13-13, huku robo ya pili DB Lioness ikiongoza kwa  pointi 22-10, 25-14 na 15-9.

Mchezaji Michele Sokoudjou wa timu ya DB Lioness alifunga 15, akifuatiwa na Lovenda Opondo aliyefunga pointi 14.

Kwa upande wa JKT Stars alikuwa Dina Mussa aliyefunga pointi 24 akifuatiwa na Bahome  Selemani aliyefunga pointi 11.

Wakati huo huo, DB Troncatti ilishika  nafasi ya tatu baada ya kupewa pointi 20-0.

DB Troncatti imepata nafasi hiyo, baada ya Jeshi Stars kutofika uwanjani, kutokana na timu hiyo  kuwa Tabora kwa ajili  ya mashindano ya taifa ya netibali.