KATIKA kuipa hadhi Ligi Kuu Bara ambayo ni ya nne kwa ubora Afrika, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliutambulisha rasmi mpira utakaotumiwa kwa mashindano hayo msimu huu 2025-2026.
Utambulisho huo umefanyika Septemba 22, 2025, ikiwa ni siku tano baada ya ligi kuanza, hata hivyo, kumekuwa na mvutano wa ubora wake kutoka kwa watumiaji.
Wakati ukiendelea kutumika, baadhi ya wachezaji na makocha wanaulalamikia kwa madai kuwa una ubora tofauti na mipira waliyoizoea misimu ya nyuma, huku washambuliaji na makipa kila mmoja akitoa mtazamo wake wakidai ni mwepesi na unapaa sana ukiupiga.
Mpira huo maalumu ulizunduliwa na kutambulishwa Septemba 22, 2025, umeifanya Ligi Kuu Bara kuwa na utambulisho kama zilivyo ligi kubwa duniani zikiwemo Ligi Kuu ya England (EPL), La Liga, Serie A na Bundesliga, ambazo zote hutumia mipira maalumu iliyoundwa kwa ubora wa hali ya juu na ambayo hutolewa mapema ili wachezaji na timu kuuzoea kabla ya kuanza kwa msimu mpya.

Hata hivyo, licha ya juhudi hizo na historia hiyo kubwa kwa soka la Tanzania, baadhi ya wachezaji na makocha mbalimbali wa timu za Ligi Kuu Bara wamekuwa na mitizamo tofauti kuhusiana na mpira huo, jambo linaloibua gumzo kutokana na ubora ulionao.
Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, amesema mpira unaotumika kwa sasa hauko katika viwango vizuri, kwa sababu unaweza ukaupiga sehemu uliyokusudia ukaenda kwingine, hivyo kama kuna uwezekano ufanyiwe maboresho ya haraka sana kabla ya mambo hayaharibika mbele ya safari.
Kauli hiyo imeungwa mkono na kocha wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi, aliyesema mpira unaotumika kwa sasa ni mbovu, ikiwa ni muda mfupi tangu timu hiyo ishinde bao 1-0 dhidi ya Mashujaa, katika mechi iliyopigwa, Septemba 30, 2025.
Kipa wa Namungo raia wa Burundi, Jonathan Nahimana, amesema mpira wa sasa unazidiwa ubora mkubwa na uliotumika msimu uliopita, kwa sababu huu wa sasa una ujazo mkubwa na hata ukipiga sehemu uliyokusudia ni ngumu kwenda kama unavyotaka.
“Mpira wa sasa hivi tunaotumia unayumba sana kwa maana hautulii mguuni, kwa mfano mechi yetu na Simba kuna muda naupiga ili ukamfikie mchezaji fulani, ila kwa bahati mbaya unapoteza mwelekeo na kwenda sehemu nyingine,” amesema kipa huyo wa kimataifa wa Burundi.
Mshambuliaji wa Coastal Union, Athumani Masumbuko ‘Makambo’, amesema bila kuonyesha juhudi binafsi ni ngumu kuutumia mpira huo wa sasa hivi, kwa sababu hautulii mguuni na unapocheza viwanja visivyoboreshwa inakuwa changamoto zaidi.
“Siro siri kuna changamoto juu ya huu mpira, kwani usipokuwa makini unaweza kuonekana unazingua wakati kinachosababisha ni aina ya mpira, hatutapata nafasi ya kuutumia mapema ili kuuzoea, wahusika walifanyie kazi haraka,” amesema Masumbuko anayemiliki bao moja kwa sasa.

Kwa upande wa kipa wa Mashujaa, Patrick Munthary, amesema mpira wa sasa ni mwepesi na unapoteza mwelekeo tofauti na wa msimu uliopita.
Wachezaji wengine ambao hawakutaka kutajwa majina yao, baadhi walikiri hawaoni tofauti yoyote ya mpira huo na wa misimu ya nyuma, ingawa wanashangaa kuzinduliwa na kutambulishwa wakati timu zimeshaanza kucheza ligi.
“Ninavyojua mpira unatakiwa kusambazwa mapema hata kabla ligi haijaanza ili wachezaji wauzoee, ila kwetu tumekutana nao uwanjani, hii sio sawa na ndio maana tunashindwa kuutumia,” amesema mmoja ya nyota hao, huku mwingine akisema hakuwa anajua kama mpira unaotumika ni mpya.
Mmoja wa mabosi wa klabu ya ligi hiyo kutoka nje ya Dar, amesema bado hawajapewa mpira kama inavyotakiwa, lakini wanakutana nao uwanjani na kuhoji labda kwa timu za Dar es Salaam ndizo zilizofikiriwa kwani hata mazoezini wanaonekana kuwa nayo.
Leo Oktoba 2, 2025, Mwanaspoti limemtafuta Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Ibrahim Mwayela ili atoe ufafanuzi juu ya madai hayo ya mpira huo mpya wa Ligi Kuu, lakini amesema atafutwe Ofisa Habari wa TPLB, Karim Boimanda.
Boimanda alipopatikana alisema hawakuwa wamepata malalamiko juu ya mpira huo, lakini watalifanyia kazi kwa haraka kama kuna tatizo lolote.
“Hatujapata hayo madai kwa sasa. Ila Bodi itakusanya maelezo ya walioutumia mpira huo kisha itatoa taarifa rasmi kwa umma,” amesema Boimanda.
Licha ya kulalamikiwa, mpira huo uliotambulishwa rasmi Septemba 22, 2025, siku tano tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu huu 2025-2026, umetajwa na ubora wa kimataifa ambapo vipengele vilivyowekwa wakati wa utambulisho vinasomeka hivi;

– Ni moja kati ya mipira bora ya kitaalamu iliyotengenezwa kwa ubora wa hali ya juu na muonekano wa kuvutia.
– Imetengenezwa kwa ngozi maalum ya sintetiki rafiki kwa mazingira, pamoja na tabaka 4 za kitambaa maalum na safu ya ndani ya TPU, ikileta mpira wenye ubora mzuri na mguso laini.
– Una vipande 32 vilivyoshonwa kwa mkono, vinavyohakikisha mpira unaenda sawasawa na kuwa thabiti hata baada ya makumi ya maelfu ya mateke.
– Teknolojia ya High Frequency Embossing inaboresha urahisi wa kuuchezea na muonekano wa mpira.
– Ndani yake kuna blada ya mpira laini yenye valve ya ubora wa juu kuzuia upotevu wa hewa.
– Haunyonyi maji kwa urahisi kwa sababu ya mbinu maalum ya kushona paneli, hivyo unaweza kuutumia hata katika mvua bila matatizo.
– Huu ni mpira wa kiwango cha juu cha FIFA QUALITY PRO.