Pemba. Meli na vifaa vya kisasa vya uvuvi ni miongoni ahadi zitakazotekelezwa na Chama cha ACT – Wazalendo ili kuboresha shughuli za sekta hiyo, endapo kikishika dola ya kuiongoza Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.
Ahadi hizo ni kwa mujibu wa mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho, Othman Masoud Othman, utekelezaji wa hilo utaanza punde atakapoapishwa kuwa rais wa awamu ya tisa wa visiwa hivyo.
Othman ameeleza hayo leo Alhamisi Oktoba 2, 2025, wakati akizungumza na wavuvi wa kijiji cha Shumba, Wilaya ya Micheweni Pemba katika mwendelezo wa kusaka kura ngazi ya awali kabla ya jioni kuhutubia mkutano wa hadhara.
Othman amesema Zanzibar imebarikiwa neema ya bahari, lakini bado wananchi hawajanufaika ipasavyo na rasilimali hiyo kutokana na kukosekana kwa vyombo vya kisasa vya kuvulia kwenye bahari kuu.
Ili kuondoka na changamoto hiyo, Othman amesema Serikali itakayoundwa na ACT -Wazalendo itahakikisha wavuvi wa Zanzibar wanapatiwa meli bora na vifaa vya kisasa vya uvuvi badala ya kutegemea boti ndogo na ‘fiber’ zinazodaiwa kutolewa pasipo kuzingatia mahitaji halisi.

“Tungeitumia bahari ipasavyo, wananchi wote wangenufaika kupitia sekta hii na samaki ingekuwa si bidhaa ya anasa, bali ya heshima kwa familia na hoteli za kitalii zisingekosa bidhaa hii muhimu,” amesema Othman.
Amesema chama cha ACT – Wazalendo kimedhamilia kuigeuza sekta ya uvuvi kuwa nguzo kuu ya uchumi wa Zanzibar kikilenga kuwanufaisha wananchi wote wa kisiwa.
“Taifa la Seychelles sehemu kubwa ya mapato yake yanatoka na uvuvi wa bahari kuu na usafirishaji wa samaki kwenye masoko ya kimataifa. Sasa kama Seychelles wanaweza, kwa Zanzibar tusifanye?” amesema.
“Zanzibar ina eneo kubwa la bahari, tuna vijana wengi na tuna hoteli zinazohitaji samaki kila siku.Kinachokosekana ni dhamira ya kisiasa na uwekezaji wa kweli,” ameeleza.
Amesema akishika dola Oktoba 29, Serikali atakayoiunda itajenga vituo maalumu vya baridi na masoko ya kisasa ya samaki katika visiwa vya Unguja na Pemba ili kuhakikisha wavuvi wanapata bei nzuri ya mazao yao.
Katika mkutano huo, Othman amesema sekta ya uvuvi injini ya ajira kwa vijana wa Zanzibar, hivyo atahakikisha Serikali inawekeza katika meli za kisasa, viwanda vya kusindika samaki, na masoko ya kimataifa ili kuongeza ajira kwa vijana za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Othman amesema ununuzi wa meli za kisasa za uvuvi, utakwenda sambamba na ununuzi wa boti maalumu za uokozi zitakatumika kusaidia wavuvi wanaopata ajali baharini.
“Haiwezekani kila mwaka tupoteze maisha ya wavuvi kwa sababu hakuna msaada wa haraka. Serikali nitakayoiongoza itanunua boti za uokozi na kuziweka katika maeneo maalumu, kuwasaidia wavuvi pale wanapopa matatizo, tunataka wawe na uhakika wa msaada wa haraka,” amesema.
Othman amesema usalama wa wavuvi si suala la hiari bali ni jukumu la Serikali, kwa sababu Kundi hilo ndio wachangiaji wakubwa wa chakula na mapato ya taifa.
“Tunakwenda kuwalinda wavuvi wetu, tutalinda familia zao na tunalinda uchumi wa Zanzibar,” amesema.
Juma Ali anayejishughuli na uvuvi katika eneo hilo amesema, “Tumeishi maisha ya uvuvi kwa vizazi vingi, lakini bado tunatumia boti ndogo zisizo salama. Tunavua karibu na pwani tu kwa sababu hatuna meli za kwenda bahari kuu au maji marefu.
“Kuna wakati tukienda kuvua, tunarudi mikono mitupu, licha ya Samaki kuwa wengi. Tunashukuru ahadi ya ununuzi wa meli na vifaa vya kisasa vya uvuvi itakayoongeza thamani katika sekta hii,” amesema Ali.