Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Kombo amesisitiza umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti na endelevu ya ushirikiano kati ya nchi za Afrika na Nordic (Denmark, Finland, Iceland, Norway na Sweden).
Imeelezwa ushirikiano huo na nchi hizo za Ulaya lazima ulete matokeo halisi kwa wananchi wa pande zote mbili.
Balozi Kombo ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na ujumbe unaohudhuria mkutano wa 22 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje kati ya nchi za Afrika na za Nordic, unaofanyika mjini Victoria Falls, Zimbabwe, unaofanyika kuanzia Oktoba 2 hadi 3, 2025.

Waziri Kombo amesema mkutano huo ni fursa muhimu ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii, sambamba na kuchochea biashara, uwekezaji, teknolojia na nishati safi.
Mkutano wa mwaka huu unaongozwa na kaulimbiu isemayo: (Ubunifu kwa Matokeo: Kutumia Teknolojia na Ushirikiano kwa Jamii Zinazojitayarisha kwa Baadaye).
“Ushirikiano huu haupaswi kubaki kwenye makaratasi pekee. Tunapaswa kuhakikisha tunazitumia fursa zilizopo kwa vitendo ili kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi,”amesema.
Waziri Kombo amesisitiza utayari wa Tanzania kushirikiana na nchi za Nordic kuendeleza miradi ya kimkakati yenye matokeo ya haraka.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Suzan Kaganda, amewahimiza washiriki kutumia mkutano huo kama jukwaa la kuimarisha diplomasia ya uchumi, kupitia sekta za biashara, uwekezaji, utalii, kilimo, elimu na ulinzi.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi, amesisitiza fursa zilizopo Tanzania kwa ushirikiano wa kibiashara na kiuwekezaji na nchi za Nordic.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje, Seifu Kamtunda ameeleza kuwa mkutano huo utajadili mada kuu zinazolenga kuimarisha uhusiano wa Afrika na Nordic, sambamba na kongamano la biashara litakalokutanisha wafanyabiashara, sekta binafsi, wavumbuzi vijana na taasisi za kitaaluma.

Taasisi mbalimbali kutoka Tanzania zikiwemo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) na idara tofauti za wizara ya mambo ya nje zinashiriki ili kuonesha maeneo ya kipaumbele na kukuza majadiliano ya kiuchumi na kidiplomasia.