TRA YAENDELEA KUNG’ARA KWA MAKUSANYO MAKUBWA YA KODI

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kuandika historia mpya ya makusanyo ya kodi kwa kukusanya kiasi cha Sh. Trilioni 8.97 sawa na ufanisi wa asilimia 106.3 ya lengo la kukusanya Sh. Trilioni 8.44. katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26 (Julai hadi Septemba 2025).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa (TRA) leo tarehe 02.09.2025 Bw. Yusuph Juma Mwenda imeeleza kwamba makusanyo hayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 15.1 ikilinganishwa na kiasi cha Sh. Trilioni 7.79 kilichokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2024/25.

Amesema makusanyo yaliyokusanywa kwenye robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26 (Julai – Septemba 2025) ni sawa na ukuaji wa asilimia 104 ukilinganisha na kiasi cha Shilingi Trilioni 4.40 kilichokusanywa katika kipindi kama hicho toka Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipoingia madarakani mwaka wa fedha 2020/21.

Amesema wastani wa makusanyo kwa mwezi pia umeongezeka toka kiasi cha Sh. Trilioni 1.47 kwa mwezi mwaka 2021/22 mpaka kufikia kiasi cha Sh. Trilioni 2.99 kwa mwezi kwa mwaka 2025/26.

“Kipekee, kwa mara ya kwanza TRA imeweza kukusanya kiasi cha Sh. Trilioni 3.47 kwa mwezi mmoja wa tisa ambacho ni kiasi kikubwa kuliko miezi mingine ya nyuma kama hiyo” inaeleza taarifa ya Mwenda.

Amesema ufanisi huo katika makusanyo ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26 umechagizwa na mambo kadhaa ikiwemo kuendelea kuboresha mahusiano na walipakodi nchini, ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji kwa vitendo wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuendelea kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari nchini bila uonevu.

Aidha, TRA imeendelea kuboresha mahusiano na ushirikiano na Wizara, Taasisi mbalimbali za Serikali, pamoja na mashirika ya kimataifa katika kuhakikisha wote wanashiriki katika uhamasishaji wa ulipaji kodi kwa hiari nchini ambapo kumekuwa na ongezeko la uwajibikaji wa kulipa kodi kwa hiari miongoni wa walipakodi. 

Amesema kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi kutokana na sera nzuri za uchumi na mazingira ya biashara yaliyowekwa na Serikali ya awamu ya sita, matokeo chanya ya uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara nchini kupitia kwa uanzishwaji wa “Dawati la Uwezeshaji Biashara” nchi nzima lenye lengo la kusaidia kuwawezesha wafanyabiashara na walipakodi wote nchini kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika shughuli zao ili waweze kuongeza uhiari wao katika kulipa kodi.

Ameeleza kuwa TRA itaendele kuweka kipaumbele katika utoaji wa huduma bora zinazozingatia mahitaji ya walipakodi, kupitia kuwahudumia walipakodi siku za mapumziko (Jumamosi na Jumapili) kupitia ofisi zote za TRA nchini, kuwezesha biashara kuendelea kufanyika kupitia majadiliano na wafanyabiashara ili kuwawezesha walipe madeni yao ya kodi pasipo kuathiri mwenendo wa biashara zao.

Katika hatua nyingine taarifa hiyo imeeleza kuwa Ufanisi wa makusanyo uliofikiwa na TRA kwa miezi ya Julai – Septemba ni kiashiria chanya katika kuhakikisha kuwa lengo la makusanyo ghafi kwa mwaka wa fedha 2025/26 la Sh. Trilioni 36.066 linafikiwa.

Katika kufanikisha hili, Menejimenti ya TRA inaendelea kutekeleza kikamilifu maagizo yote ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu usimamizi wa kodi nchini na uhamasishaji wa ulipaji kodi kwa hiari na kuendelea kuwezesha ufanyikaji wa biashara nchini kupitia “Dawati la Uwezeshaji Biashara”;

Amesema TRA inapenda KUWAHAKIKISHIA wananchi wote kuwa jitihada za ukusanyaji mapato zinaendelea kwa ukamilifu wake, na lengo la makusanyo kwa mwaka huu wa fedha 2025/26 linafikiwa lote. Kwa kushirikiana na wananchi, TRA inaamini makusanyo haya yatafanikishwa kwa UADILIFU, UWAZI na UFANISI, ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na huduma nyingine muhimu za kijamii, kwa manufaa ya Taifa zima.