Mabasi mapya yaongeza nguvu Kimara-Gerezani

Dar es Salaam. Mabasi ya Kampuni ya Mofat Limited, yaliyopangwa kutumika katika Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) katika njia ya Gerezani–Mbagala, yameanza rasmi kutoa huduma ya muda ya usafiri katika njia ya Kimara-Gerezani.

Uwepo wa mabasi hayo yanayotumia mfumo wa nishati ya gesi asilia umeleta mabadiliko chanya katika huduma za usafiri kati ya Kimara na Gerezani, kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano wa abiria katika vituo vya mabasi.

Kituo cha Kimara wilayani Ubungo, ambacho kwa kawaida huzongwa na idadi kubwa ya abiria, leo Oktoba 2, 2025, kimeonekana kuwa na abiria wachache, wakiingia kwenye mabasi kwa utaratibu maalumu wa kupanga mstari.


Hali kama hiyo imeshuhudiwa pia katika vituo vya Korogwe, Kibo, Magomeni hadi Gerezani, ambapo idadi ya abiria imepungua ikilinganishwa na siku za kawaida, hatua inayochangiwa na kuongezeka kwa idadi ya mabasi yanayotoa huduma.

Mwananchi digital leo Oktoba 2, 2025 imeshuhudia mabasi zaidi ya 10 mapya ya Kampuni ya Mofat Limited yakiwa kazini, yakitoa huduma ya usafiri na kuongeza nguvu kwenye mfumo wa mabasi yaendayo haraka (Dart).

Hatua hii imekuja siku moja tu baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kufanya ziara katika kituo cha mabasi cha Kimara na kuwataka wananchi kuwa watulivu na wavumilivu, wakati Serikali ikiendelea kushughulikia changamoto ya usafiri wa mwendokasi, hususan katika kituo hicho.


“Ndani ya wiki hii mabasi hayo yataanza kutoa huduma. Tayari yapo ‘yard’-ini yakisubiri kuingizwa barabarani. Tumekutana na kampuni husika na baadhi yataanza kazi muda wowote kuanzia sasa,” alisema Chalamila.

Ahadi ya Chalamila baada ya kutembelea kituo cha mabasi yaendayo haraka eneo la Kimara ni kufuatia video zilizosambaa mitandaoni zilionyesha abiria waliojazana kwenye usafiri huo, wakipaza sauti hawataki Chama cha Mapinduzi (CCM).

Jana usiku kuanzia saa mbili kutokana na adha ya usafiri huo, abiria walifanya fujo na kuharibu miundombinu ya mradi huo kwa kupasua vipo vya vituo na baadhi ya mabasi.


Tukio hilo limeshuhudiwa katika vituo vya Mwembe Chai na Magomeni Usalama, Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amethibitisha tukio na hadi sasa watu watatu wanashikiliwa kwa madai ya kuhusika na uharibifu wa miundombinu ya usafiri huo.