Mfanyabiashara adaiwa kujinyonga Moshi, sababu yatajwa

Moshi. Mfanyabiashara katika sekta ya utalii, Azizi Msuya (39), mkazi wa Sambarai wilayani Moshi, amekutwa amefariki dunia akidaiwa kujinyonga nyumbani kwake kwa kutumia kamba ya katani iliyokuwa imefungwa juu ya kenchi.

Tukio hilo limetokea leo Alhamisi, Oktoba 2, 2025 saa 2 asubuhi katika kata ya Kindi, tarafa ya Kibosho, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa taarifa za Polisi, marehemu alikuwa akijihusisha na biashara ya kusafirisha wageni (tours) katika mkoa huo.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa marehemu alijinyonga kutokana na msongo wa mawazo.

Amesema msongo huo ulisababishwa na madeni ya benki na watu binafsi aliyokuwa anakabiliana nayo kwa muda mrefu.

“Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha marehemu kujinyonga ni msongo wa mawazo kutokana na madeni ya benki na watu binafsi,” amesema Maigwa.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa ajili ya uchunguzi na taratibu za mazishi.