Gomez anataka ndoo Simba | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI wa Kitanzania, Seleman Mwalimu ‘Gomes’ amesema bao la kwanza alilofunga juzi dhidi ya Namungo Ligi Kuu Bara akiwa na uzi wa Wekundu wa Msimbazi ni mwanzo wa mengi yanayofuata, huku akiwa na hesabu za kuisaidia timu hiyo kutwaa mataji msimu huu.

Simba imeanza vizuri msimu huu wa Ligi Kuu Bara baada ya kuibuka na ushindi wa pili mfululizo wa mabao 3-0 katika kila mechi, hivyo kukaa kileleni mwa msimamo kwa pointi sita sawa na Singida BS, ila inabebwa na uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa wakati ligi ikienda mapumziko.

“Nilikuwa nasubiri muda wangu na nilipopewa nafasi nilijua ni lazima nifanye kitu. Huu ni mwanzo tu, bado nina kazi kubwa ya kufanya na ninaamini nitakuwa msaada kwa timu yangu,” alisema Gomes aliyetua Msimbazi msimu huu kwa mkopo akitokea Wydad Casablanca ya Morocco aliyomnunua kutoka Singida BS ambapo ilimtoa kwa mkopo Fountain Gate na kuifungia mabao sita.


Straika huyo aliyetamba visiwani Zanzibar kabla ya kujua Singiga na kupelekwa kwa mkopo Fountain hadi alipouzwa Januari na kushiriki fainali za Kombe la Dunia la Klabu, aliingia dakika ya 69 katika mechi hiyo ya pili, aliihakikishia Simba ushindi huo akifunga dakika ya 84 baada ya kumlamba chenga beki wa Namungo, Hussein Kazi aliyewahi kuzitumikia Geita Gold na Simba.

Mabao mengine ya Simba yalifungwa na mabeki wa kati, Chamou Karabou na Rushine De Reuck lililokuwa bao lake la pili, ndiye beki wa kati mwenye mabao mengi zaidi kwa sasa.

Katika mechi ya kwanza ya ligi dhidi ya Fountain Gate, Gomes hakupata nafasi ya kucheza na badala yake, alitumika Jonathan Sowah aliyekuwa mmoja wa wafungaji wa mabao wakati wanaizamisha Fountain pia kwa mabao 3-0 kwenye uwanja huo huo wa Benjamini Mkapa.

“Najua Simba ni klabu kubwa na ushindani wa namba ni mkali. Hii inanifanya nijitume zaidi. Kila mshambuliaji hapa ana njaa ya kufunga, lakini mimi nimejiwekea malengo binafsi ya kusaidia timu kufanya vizuri na hatimaye kutwaa ubingwa,” alisema Gomes na kuongeza;

“Najua haitakuwa rahisi, lakini naamini nitafanikiwa kwa juhudi na msaada wa wenzangu,” alisema Gomes kwa kujiamini.

Simba ina washambuliaji watatu wa kati ambao wamekuwa wakigawanywa muda tangu kuanza kwa msimu huu katika mashindano yote hivyo kila mmoja anakibarua cha kupigania namba kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Mshambuliaji pekee wa kati ambaye bado hajacheka na nyavu tangu mechi ya Ngao ya Jamii, kimataifa dhidi ya Gaborone United nyumbani na ugenini ni Steven Mukwala aliyeanza dhidi ya Namungo.

Mukwala aliifungia Simba mabao 13 msimu uliopita sawa na Sowah aliyepachika idadi hiyo ya mabao wakati akiichezea Singida Black Stars.

Mara ya mwisho kwa Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ilikuwa msimu wa 2020/21 wakati huo kikosi hicho kilikuwa chini ya kocha, Didier Gomes, imepita misimu minne ya ukame kwa Mnyama.