Riba ya BoT kwa mabenki kubaki asilimia 5.75

Dar es Salaam. Matokeo chanya yanayoonekana katika shughuli za kiuchumi yametajwa kuwa kichocheo cha kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) kusalia kuwa asilimia 5.75 kama ilivyokuwa robo mwaka uliopita.

Riba hiyo imesalia kama ilivyo ikiwa ni baada ya Kamati ya Sera za Fedha (MPC) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kufanya mapitio na kujiridhisha na uthabiti wa uchumi.

Uamuzi huu unadhihirisha kuendelea kwa imani katika mwelekeo wa uchumi wa nchi, huku viongozi wakisisitiza umuhimu wa sekta zote kudumisha kasi hiyo.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amesema uamuzi huo unatokana na makadirio ya mfumuko wa bei ambao unatarajiwa kubaki ndani ya kiwango cha lengo cha asilimia 3 hadi 5.

Hilo pia linatokana na ukuaji wa uchumi unaochochewa na shughuli za kibiashara na misingi ya uchumi.

“Uamuzi wa kuendelea na CBR kama ilivyo ni kielelezo cha maendeleo chanya katika mazingira ya uchumi ya ndani na duniani,” amesema Gavana Tutuba.


 “Tunaona uthabiti katika mfumuko wa bei, ukuaji thabiti katika sekta mbalimbali na hali nzuri ya uchumi duniani inayounga mkono mtazamo wetu wa uchumi,” amesema.

Amesema takwimu za hivi karibuni zinathibitisha kwamba uchumi wa Tanzania bado uko kwenye ukuaji thabiti.

Katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, Pato la Taifa la Tanzania Bara limekua kwa asilimia 5.4, likiwa limeongezeka kutoka asilimia 5.2 katika kipindi kama hicho mwaka jana na kuongozwa na sekta za madini, kilimo, huduma za fedha na viwanda. Uchumi wa Zanzibar ulionyesha ukuaji wa asilimia 6.4 katika kipindi hicho.

Amesema kasi hii inatarajiwa kuendelea, huku makadirio yakionyesha kiwango cha ukuaji wa zaidi ya asilimia sita katika robo ya pili na ya tatu na kasi kama hiyo katika robo ya nne huku uchumi wa nchi unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.3 mwaka 2025, huku sekta kuu kama utalii, ujenzi, na kilimo zikiongoza katika ukuaji.

Kuhusu mfumuko wa bei, Tanzania Bara ulikuwa asilimia 3.4  Agosti 2025, ikiwa ndani ya lengo la asilimia 3 Hadi 5. Zanzibar ulipungua kidogo kutoka asilimia 4.2 hadi 4.0, hasa kutokana na bei za chakula kupungua.

 “Sekta zote mbili zinatarajiwa kudumisha viwango vya mfumuko wa bei chini ya asilimia tano, vikiwa vinachangiwa na usambazaji thabiti wa chakula, viwango vya kubadilishana vya shilingi, na bei za mafuta za wastani,” amesema.

Ujazi wa fedha uliendelea kuongezeka kwa kasi kama ilivyokuwa katika vipindi vilivyopita, ukichagizwa na ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi.

 Katika robo mwaka iliyoishia Septemba 2025, ujazi wa fedha ulikua kwa wastani wa asilimia 20.4, ikilinganishwa na asilimia 19.1 katika robo iliyotangulia.

“Mikopo kwa sekta binafsi, iliendelea kuongezeka kwa kasi ya asilimia 15.9, ikichangiwa na uwepo wa ukwasi wa kutosha kwenye uchumi pamoja na ongezeko la uwekezaji katika sekta hiyo,” amesema.

Sekta ya kibenki iliendelea kuwa thabiti ikiwa na ukwasi, mtaji wa kutosha na yenye kutengeneza faida huku vihatarishi katika utoaji wa mikopo viliendelea kupungua na mikopo chechefu iliendelea kupungua hadi asilimia 3.3  Agosti 2025, ndani ya kiwango kinachohimilika cha asilimia 5.

“Sekta ya nje imeendelea kuimarika ikichangiwa na ongezeko la mauzo ya mazao ya biashara nje ya nchi, utalii na dhahabu, pamoja na kupungua bei za mafuta ghafi katika soko la dunia,” amesema.

Hali hiyo ilifanya nakisi ya urari wa malipo ya kawaida kwa Tanzania Bara kupungua hadi asilimia 2.4 ya Pato la Taifa kwa mwaka unaoishia Septemba 2025, kutoka  asilimia 3.8 ya pato la Taifa kwa mwaka uliotangulia.

 Kwa upande wa Zanzibar, ziada ya urari wa malipo ya kawaida iliongezeka hadi Dola za Marekani milioni 685.6 kwa mwaka ulioishia Septemba 2025, kutoka Dola milioni 499.0 mwaka uliotangulia, kutokana na ongezeko la mapato ya huduma, hususan shughuli za utalii.

Kuimarika huku kwa sekta ya nje kulichangia ongezeko la ukwasi wa fedha za kigeni katika uchumi na kuimarika kwa thamani ya shilingi.

Hiyo ni baada ya shilingi ya Tanzania kuendelea kuwa imara, huku thamani yake ikiongezeka kwa asilimia 8.4 katika robo ya tatu ya mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 0.7 katika robo mwaka iliyotangulia.

Akiba ya fedha za kigeni iliendelea kuwa ya kutosha, ambapo mwishoni mwa Agosti 2025 ilifikia Dola za Marekani milioni 6.4, kiwango kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa zaidi ya miezi 5, sanjari na lengo la nchi na vigezo vya kikanda kwa EAC vya miezi 4.0 na 4.5, mtawalia.

Ukwasi wa fedha za kigeni unatarajiwa kuendelea kuongezeka kutokana na mauzo ya korosho na dhahabu, pamoja na shughuli za utalii.

“Utekelezaji wa bajeti za Serikali katika robo ya kwanza ya mwaka 2025/26 ulikuwa wa kuridhisha kwa Tanzania Bara na Zanzibar. Mapato ya ndani yalivuka lengo kutokana na mwenendo mzuri wa makusanyo ya kodi kufuatia kuongezeka kwa utayari katika ulipaji wa kodi kwa hiyari, sambamba na usimamizi thabiti,” amesema.

Kuhusu matumizi ya Serikali amesema yaliendelea kuoanishwa na rasilimali zilizopo, hali inayoakisi usimamizi madhubuti  wa fedha za umma.

“Deni la taifa halikuwa na mabadiliko makubwa kutoka robo mwaka iliyotangulia, ambapo sehemu kubwa ya fedha zilizokopwa zilielekezwa kwenye miradi ya kimkakati ya ujenzi wa miundombinu,” amesema.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC na Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania, Theobald Sabi alisifu maendeleo chanya ya uchumi yaliyotajwa katika ripoti.

“Kupungua kwa nakisi ya akaunti ya sasa, pamoja na utendaji mzuri katika sekta kuu kama kilimo, madini, na utalii, kunadhihirisha ustahimilivu wa uchumi wa Tanzania,” amesema Sabi.

Alisisitiza pia uthabiti wa sekta ya fedha ya Tanzania na uthabiti wa hifadhi za fedha za kigeni kama viashiria muhimu vya ustahimilivu wa uchumi wa nchi, hata katika hali ya kutokuwa na uhakika duniani.