Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya Sh8.97 trilioni kati ya Julai hadi Septemba 2025 Ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.1 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.
Makusanyo hayo ni sawa na ufanisi wa asilimia 106.3 ya lengo la kukusanya Sh8.43 trilioni.
Taarifa iliyotolewa na TRA leo Oktoba 2, 2025 inaeleza kuwa, makusanyo yaliyokusanywa kwenye robo ya Julai hadi Septemba 2025 ni sawa na ukuaji wa asilimia 104 ukilinganisha na Sh4.40 trilioni zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka 2020/2021.
Pia, taarifa hiyo inaeleza kuwa, wastani wa makusanyo kwa mwezi pia umeongezeka kutoka cha Sh1.47 trilioni kwa mwezi, mwaka 2021/22 mpaka Sh2.99 trilioni kwa mwezi kwa mwaka 2025/26.
“Kwa mara ya kwanza Mamlaka ya Mapato Tanzania imeweza kukusanya Sh3.47 trilioni kwa mwezi mmoja wa Septemba, ni kiasi kikubwa kuliko miezi mingine ya nyuma kama hiyo,” inaeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hii iliyosainiwa na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Yusuph Mwenda ufanisi huu katika makusanyo ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26, umechagizwa na vitu mbalimbali ikiwamo kuendelea kuboresha uhusiano na walipakodi nchini.
“TRA imeendelea kuboresha mahusiano na ushirikiano na wizara, taasisi mbalimbali za Serikali, pamoja na mashirika ya kimataifa katika kuhakikisha wote wanashirikikatika
uhamasishaji wa ulipaji kodi kwa hiari nchini,” inaeleza taarifa hiyo.
Hali hiyo imefanya kuongezeka kwa uwajibikaji wa ulipaji kodi wa hiari miongoni wa walipakodi jambo lililoenda sambamba na ukuaji wa shughuli za kiuchumi kutokana na sera nzuri za uchumi na mazingira ya biashara yaliyowekwa na Serikali.
Taarifa hiyo inafafanua kuwa, matokeo hayo pia ni yanatokana na uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara nchini kupitia madawati ya uwezeshaji biashara yaliyopo nchi nzima.
Madawati hayo yamekuwa yakisaidia na kuwawezesha wafanyabiashara na walipakodi wote nchini kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika shughuli zao ili waweze kuongeza uhiari wao katika kulipa kodi.
“Pia, tutaimarisha usimamizi wa vyanzo vyote vya forodha kupitia matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Forodha (TANCIS) ulioboreshwa, pamoja na kuboresha ufanisi katika uondoshaji wa mizigo katika vituo vyote vya Forodha,” inasema taarifa hiyo.
Pia, inaeleza kuwa TRA itaendelea kuboresha uhusiano na wafanyabiashara kwa kutenga siku ya Alhamisi ya kila wiki kuwa ni maalumu ya kusikiliza walipakodi, kupitia ofisi zote za TRA nchini.
Mtaalamu wa Uchumi, Oscar Mkude amesema ili watu waweze kuona kodi inayolipwa inawanufaisha ni vyema Serikali iwekeze katika ujenzi wa miundombinu inayowagusa wananchi ikiwamo barabara, shule na vituo vya afya.
“Lakini inawezekana sehemu ya fedha hii inakwenda kulipa madeni ambayo tulikopa ili kutekeleza miradi mbalimbali ili tufanye miradi yetu na tukipata fedha hizo turudishe. Kwa hiyo hata wanapokopa ni vyema wananchi watambue kuwa zile ni fedha zao,” amesema.
Eneo lingine linaloweza kugusa wananchi ni kuhakikisha sekta zinazozalisha ajira nyingi zinafanyiwa uwekezaji ili mtu mmoja mmoja aweze kuguswa badala ya watu kuendelea kubaki nyumbani.