Mageuzi ya mifumo CRDB yanavyofungua fursa mpya

Dar es Salaam. Mageuzi ya mfumo mkuu wa kibenki ya CRDB yametajwa kuwa hatua kubwa ya kimkakati inayoonesha ukomavu katika sekta ya fedha nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, wakati akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, kuhusu mageuzi ya mfumo huo, akisema yanaenda kuongeza ufanisi na usalama wa fedha za wateja.

Tutuba amesema hayo kwenye mkutano maalumu kati ya menejimenti ya CRDB na BoT, uliohudhuriwa pia na manaibu gavana na wakurugenzi wa Benki Kuu.

Kauli ya Tutuba inakuja ikiwa ni siku chache baada ya mageuzi ya kihistoria ya mfumo wa benki hiyo yaliyolenga kuongeza ubora wa huduma, kuimarisha usalama wa miamala na kupanua wigo wa huduma bunifu kwa wateja wake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 2, 2025, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CRDB, Tully Esther Mwambapa, amesema pongezi hizo kutoka kwa Gavana wa BoT zinadhihirisha imani endelevu ya wadau wa sekta ya fedha kwa CRDB.

Amesema nafasi ya CRDB kama benki kiongozi barani Afrika kwenye ubunifu wa kidijitali na uthubutu wa kimaamuzi unaongeza thamani na kuendelea kuaminika kwa wateja wake.

“Hakuna safari ya mageuzi ambayo imewahi kuwa rahisi, na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwetu pia. Katika kipindi cha mabadiliko, baadhi ya wateja walipata changamoto za muda mfupi, jambo ambalo ni la kawaida katika mageuzi makubwa ya mifumo.


“Timu yetu ya wataalamu imekuwa ikifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha changamoto hizo zinashughulikiwa kwa haraka,” amesema na kuongeza;

“Leo hii nafurahi kuwajulisha kuwa huduma zetu zimerejea katika hali ya kawaida na mabadiliko yaliyofanyika yamejenga msingi imara wa kutoa huduma hapa Tanzania, Burundi, DRC, Dubai, ambapo tunapanua wigo wetu na masoko mengine mapya tunayoyaendea.”

Tully, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, amesema mageuzi hayo ya mfumo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa benki hiyo wa 2023–2027, unaoweka ubunifu wa kiteknolojia kama msingi wa ukuaji wa benki na uchumi.

Mageuzi hayo pia yanaonesha ustahimilivu wa benki kwa kusimamia mabadiliko katika nchi tatu (Tanzania, Burundi na DRC), huku huduma zikiendelea bila kukatika, jambo ambalo wadau wa ndani na nje ya nchi wamevutiwa nalo.

Hivi karibuni, Nsekela alialikwa kushiriki katika Kongamano la Biashara kati ya Marekani na Afrika (US–Africa Business Forum), lililofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) jijini New York.

Katika kongamano hilo, lililohudhuriwa na viongozi wa juu wa nchi wakiongozwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, mageuzi ya mfumo mkuu wa kibenki yaliyofanywa na CRDB yalitambuliwa kama mfano wa kuigwa Afrika na duniani. Wawekezaji walivutiwa kuona taasisi ya kifedha kutoka Afrika Mashariki ikipiga hatua kubwa kimageuzi.

Hatua hiyo imeifanya CRDB kuwa miongoni mwa benki chache Afrika zinazotajwa kwa uwekezaji madhubuti wa teknolojia katika majukwaa makubwa ya kiuchumi duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama (ICTC), Dk Nkundwe Mwasaga, ameyatambua mageuzi hayo kama mabadiliko ya kimkakati yanayodhihirisha uwezo wa Tanzania kuendesha mageuzi makubwa ya kidijitali kwa ufanisi mkubwa na salama.

Wataalamu wa ndani wa Tehama, akiwemo Nguvu Kamando wa Vodacom, wamesema mageuzi hayo yanaiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa kama kiongozi wa ubunifu wa kifedha.

Kwa mujibu wa Tully, mbali na kuongeza ufanisi, mageuzi hayo yamefungua fursa mpya za ushirikiano wa kimataifa, ikiwemo makubaliano yaliyosainiwa kando ya mkutano wa UNGA na Shirika la Crop Trust ili kuimarisha usalama wa chakula kupitia kilimo stahimilivu, na makubaliano na shirika la fedha la DIFC ya uwezeshaji wa wajasiriamali wadogo na wa kati.

Pia, CRDB imesaini makubaliano ya ushirikiano wa kiteknolojia na kampuni ya Huawei kwa ajili ya kuimarisha mabadiliko ya kidijitali, usalama wa mifumo na matumizi ya Akili Unde.

“Ushirikiano huu ni wa kimkakati na utafungua fursa kubwa kwa wakulima wadogo kupitia teknolojia za kilimo stahimilivu, kwa wafanyabiashara kupitia huduma za kifedha zilizo salama zaidi, na kwa sekta za maendeleo kupitia ubunifu wa kidijitali na akili mnemba. Ni hatua inayoongeza ushindani wa uchumi wetu kikanda na kimataifa,” amesema Tully na kuongeza:

“Kama mnavyotambua, hivi karibuni tumepata kibali cha kufungua ofisi yetu huko Dubai, hatua inayothibitisha nafasi ya CRDB kama daraja kati ya Afrika na masoko ya kimataifa. Hii ni hatua ya kimkakati ya kuwaunganisha wateja wetu na mitaji, teknolojia na fursa mpya zinazopatikana katika masoko ya kimataifa.”