Musoma. Wajasiriamali pamoja na wafanyabiashara wadogo mkoani Mara wametakiwa kutumia fursa za uwepo wa taasisi wezeshi zikiwemo za mafunzo na kifedha, ili kuboresha biashara zao na kuzifanya kwa tija.
Wito huo umetolewa mjini Musoma leo Alhamisi Oktoba 2, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi alipokuwa akifunga kongamano la wafanyabiashara wadogowadogo mkoani humo.
Kanali Mtambi amesema uwepo wa taasisi kama Sido, Veta na taasisi za kifedha ni fursa muhimu na adhimu ambazo zinatakiwa kutumiwa na wafanyabiashara hao, ili kufanya shughuli zao kwa tija na hatimaye wawe wajasiriamali wa kati na wakubwa.
Amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa kundi hilo muhimu kwa uchumi wa nchi, ambapo amesema kuanzia Januari hadi Septemba 2025 zaidi ya Sh403.6 milioni zimetolewa na benki ya NMB kama mkopo kwa wafanyabiashara hao.
“Naiagiza benki ya NMB kuhakikisha inaongeza kasi ya kutoa mikopo kwa wafanyabiashara hawa ili kufikia malengo ya Serikali ya kuliwezesha kundi hili kufanya vizuri kiuchumi, kwa ngazi ya familia jamii na nchi kwa ujumla,” amesema Kanali Mtambi.
Pia ameziagiza taasisi zinazohusika na uratibu wa shughuli za wafanyabiashara hao kuhakikisha huduma zote muhimu zinapatikana kwa wakati, ili waweze kuboresha mitaji yao na kuwa chachu ya maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
“Hili kundi ni kubwa na muhimu sana kwa uchumi wa mtu mmojammoja, mkoa na Taifa kwa ujumla, hivyo linahitaji uangalizi na uratibu wa karibu na wakati ili kila kitu kiende sawa,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema lengo la kongamano hilo ni kutaka kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa wajasiriamali ambapo kupitia kongamano hilo, watapata nafasi ya kuzitambua fursa kwa ajili ya kuboresha shughuli zao.
“Hili sio kongamano tu tunataka kuona matokeo kutokana na kongamano hili, hili sio kongamano la kupeana matumaini ni linalokuja na majibu ya changamoto za wajasiriamali ili shughuli zao ziwe na tija,” amesema Chikoka.
Chikoka amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara hao wadogo ikiwemo upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu ili kuwasaidia kuboresha shughuli zao.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, meneja wa benki ya NMB Musoma. Sospeter Justin amesema changamoto kubwa wanayokutana katika utoaji wa mikopo kwa wajasiriamali wadogo ni kusuasua kwa marejesho.
Amesema hali hiyo kwa kiasi kikubwa kumesababisha kushuka kwa idadi ya wajasiriamali wenye sifa za kukopa kwenye benki hiyo kutoka 300 hadi 150 tangu kuanza kwa utaratibu wa ukopeshaji kwa wajasiriamali wadogo miaka miwili iliyopita.
Hata hivyo, amesema wapo baadhi ya wajasiriamali ambao wameweza kurejesha kwa uaminifu mikopo yao na kusababisha kupata mikubwa zaidi, huku akitoa wito kwa wajasiriamali kutumia fursa ya mikopo hiyo kuboresha shughuli zao.
Shaban Saasita ambaye ni miongoni mwa wanufaika wa mikopo hiyo ya wajasiriamali, amesema siri ya mafanikio ni kukopa kwa malengo huku akiwataka wenzake kuhakikisha wanaitumia kwa ajili ya shughuli husika na si vinginevyo.
Amesema hadi sasa amefanikiwa kupata mkopo wa Sh8 milioni kutoka wa awali wa Sh1 milioni, ambapo amesema nidhamu ya matumizi ya fedha za mkopo na biashara kwa ujumla ni moja ya nyenzo muhimu kwa mafanikio ya mjasiriamali.
Neema Odira amesema miongoni mwa sababu zinazokwamisha kurejesha mikopo kwa wakati ni pamoja na ukosefu wa elimu ya fedha, hivyo kuziomba mamlaka husika kutoa elimu kwa wajasiriamali ili wanufaike na fursa zilizopo.
“Hapa leo wameeleza vizuri namna ambavyo sisi wajasiriamali tunaweza kunufaika na mikopo hii, lakini huko mitaani uelewa ni tofauti kwani wengi wetu tunajua huko kwenye benki sisi hatuna vigezo vya kukopeshwa,” amesema.
Kaimu Meneja wa Biashara benki ya CRDB Musoma, Yohana Michael amewataka wajasiriamali kutumia fursa za mikopo inayotolewa na benki kunufaika nayo.