Arusha/Mtwara. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kuyarudisha chini ya umiliki wa Serikali mashamba makubwa ya maua yaliyokuwa yakimilikiwa na taasisi ya Kili Flowers, baada ya wawekezaji hao kushindwa kuyaendeleza.
Samia yupo mkoani humo akiendelea kuinadi Ilani ya CCM na kuomba ridhaa ya wananchi kumchagua kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Amesema mpango uliopo ni mashamba hayo kuingizwa kwenye programu ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT) ambapo tathmini itaonesha ni mazao gani yanapaswa kulimwa.
Akizungumza kwenye mkutano uliofanyika viwanja vya Sheikh Amri Abeid leo Alhamisi, Oktoba 2, 2025, Samia amesema Serikali itayachukua mashamba hayo na kuyaendeleza kwa kuyawekewa miundombinu ya kilimo na mojawapo litapimwa na kukatwa viwanja vya makazi.
“Wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza, hivyo tumeunda timu ya makatibu wakuu ambao wamekwenda kuyafanyia tathmini ili tukae na wawekezaji tuelewane, tuyachukue, tuyaendeleze na tuyaingize kwenye BBT kwa ajili ya vijana wetu.
“Tutaangalia ni mazao gani yanaweza kulimwa. Shamba la Nduruma tunakwenda kuligawa mara mbili, sehemu moja tutafanya kilimo cha mjini na sehemu iliyosalia tutapima kwa ajili ya makazi ya watu,” amesema Samia.
Mgombea huyo pia ameahidi kuvifufua viwanda vilivyokufa na kuanzisha vipya mkoani humo ili kutengeneza ajira kwa vijana, akitolea mfano wa kiwanda cha Magadi Soda kitakachojengwa wilayani Monduli.
Katika jitihada za kukuza uchumi wa mkoa huo, mgombea wa urais ameahidi kujengwa kwa kituo cha treni ya kisasa kwa kile alichoeleza kuwa Arusha itakuwa mkoa utakaopitiwa na reli ya kisasa kutoka Tanga hadi Musoma.
“Hii reli itasaidia shughuli za usafiri na usafirishaji. Sasa, kwa kuwa Arusha ni jiji kubwa, lazima kutakuwa na kituo kikubwa. Kituo hiki kitaleta fursa za ajira kwa wafanyabiashara na vijana wetu wa hapa,” amesema Samia.
Amesema hilo litakwenda sambamba na kuanzishwa kwa vyuo vya ufundi kila wilaya mkoani humo ili vijana wapate ujuzi wa kuhudumia miradi mikubwa ikiwemo ule wa reli.
Kwenye sekta ya utalii, amesema akipata ridhaa ya kuongoza Serikali kwa miaka mitano ijayo itaendeleza mikakati ya kukuza sekta hiyo kwa kuwa ni kimbilio la ajira kwa vijana wengi wa Arusha.
Samia amesema, kwa kutambua umuhimu wa sekta ya utalii na mchango wake katika uchumi, Serikali yake itachukua hatua kuchagiza ukuaji zaidi wa sekta hiyo.
Baadhi ya hatua hizo ni maboresho ya viwanja vya ndege vya Arusha na Karatu, kujenga kituo cha kimataifa cha mikutano jijini Arusha, ujenzi wa mji wa Afcon City pamoja na ujenzi wa kituo cha urithi wa jiolojia katika eneo la Ngorongoro Lengai.
Ahadi nyingine ni kuvutia uwekezaji wa hoteli za hadhi ya juu ili watalii waje nchini wakiwa na uhakika wa sehemu za kufikia.
“Tumetumia Sh17 bilioni kuufanyia maboresho uwanja wa ndege wa Arusha. Kufikia Desemba mwaka huu utakuwa umekamilika na Januari utaanza kutumika usiku na mchana kusaidia safari za watalii, wafanyabiashara na Watanzania kwa ujumla.
“Tumeimarisha pia shirika letu la ndege, tutaongeza ndege nane…Lengo letu, kabla ya kufikia 2030, ni idadi ya watalii wanaokuja nchini ifikie milioni nane,” amesema Samia.
Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ameeleza kuwa mgombea huyo wa urais, ameonesha kwa vitendo anaweza kulitekeleza jukumu hilo kwa ufanisi.
Amesema wakati Samia alipoingia ofisini baada ya kuapishwa alikutana na makundi matatu ya ahadi ambayo yote ameyatekeleza na matokeo yake yameonekana.
Kwa mujibu wa Kinana, kundi la kwanza la ahadi ni zilizotolewa na CCM kupitia Ilani ya 2020/2025, kundi la pili ni ahadi zilizotolewa na mtangulizi wake (hayati John Magufuli) wakati akiomba ridhaa ya urais na kundi la tatu ni ahadi alizotoa yeye akiwa mgombea mwenza.
Kinana amebainisha kuwa Samia amefanyia kazi sekta zote, akifanikiwa kutekeleza ilani kwa asilimia 98, huki akitekeleza ahadi za mtangulizi wake kwa asilimia 100 na ahadi zake kwa asilimia 100.
“Ilihitaji kiongozi mwenye utulivu kuhakikisha kazi zote hizo zinafanyika kwa ufanisi. Licha ya kuwa aliingia katika kipindi kigumu, amefanya kazi ya kutukuka, alijituma na kujitolea.
“Matokeo ya kazi yake yanaonekana kila mahali nchini na ndiyo maana nasema tumpe kura aendeleze kazi hiyo nzuri,” amesema.
Kuhusu kaulimbiu ya Kazi na Utu, Kinana amesema msingi namba moja wa utu ni haki, na mgombea huyo alisikia kilio hicho na ndiyo sababu akaunda Kamati ya Haki Jinai.
“Bila kufikiria uchaguzi, bila kufikiria kuomba kura, alisikiliza shida za wananchi. Akagundua na kutambua kuwa tatizo kubwa katika taifa letu ni kasoro zilizopo katika kutoa na kusimamia haki.
“Wakati kamati hii inaundwa si Rais wala chama kilichokuwa kinafikiria uchaguzi. Alifanya hivyo baada ya kusikia kilio cha haki kutoka kwa wananchi. Akaamua kufanyia kazi. Hatua kadhaa zilichukuliwa. Sasa kwanini tusimchague mtu huyu anayejali na kusikiliza changamoto za wananchi?” amehoji Kinana.
Nchimbi atoa ahadi nne Mtwara
Kwa upande wake, mgombea mwenza, Dk Emmanuel Nchimbi, akiwa mkoani Mtwara leo, ameahidi miradi mikubwa minne ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa meli kubwa ya mizigo itakayokuwa ikisafirisha bidhaa kuelekea nchini Comoro.
Ahadi nyingine ni kuboreshwa kwa uwanja wa ndege wa Mtwara kwa kujengwa majengo ya kisasa ya abiria, jengo la zimamoto na mnara wa taa, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa shughuli za usafiri wa anga mkoani humo.
Pia, Dk Nchimbi ameahidi kuwa CCM ikipatiwa ridhaa ya kuendelea kuongoza, itatatua changamoto ya upatikanaji wa majisafi kwa kujengwa mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Ruvuma pamoja na ujenzi wa bomba la gesi lenye urefu wa kilomita 34 kutoka Mtonya hadi Madimba.
Ametoa ahadi hizo leo katika mikutano ya kampeni iliyofanyika kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Nanguruwe (Jimbo la Mtwara Vijijini), Nanyamba na kwenye Uwanja wa Mpira wa Kassim Majaliwa (Jimbo la Tandahimba).
Dk Nchimbi amesisitiza dhamira ya CCM ni kuendeleza kasi ya utekelezaji wa ahadi kwa miaka mitano ijayo.
Amesema zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa Mtwara wanajihusisha na kilimo, lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa masoko ya uhakika.
“Wakulima wanazalisha mazao mengi lakini wanashindwa kuyauza yote. Tutajenga meli kubwa ya mizigo itakayokuwa ikipeleka bidhaa zetu Comoro,” ameahidi Dk Nchimbi.
Aidha, ameahidi kuwa Samia akishinda, ataboresha uwanja wa ndege wa Mtwara kwa kujenga majengo ya kisasa ya abiria, jengo la zimamoto na mnara wa taa ili kuongeza hadhi na ufanisi wa kiwanja hicho.
Kuhusu changamoto ya maji, Dk Nchimbi amesema wataanzisha mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Ruvuma, akisisitiza haiwezekani mkoa wenye mto huo mkubwa ukakosa huduma ya uhakika ya majisafi.
“Kazi kubwa imefanyika, lakini bado ipo ya kufanya. Tutaanzisha mradi mkubwa wa Mto Ruvuma kuhakikisha maji yanawafikia wananchi hadi vitongoji,” amesema.
Pia, amesisitiza dhamira ya mgombea urais wa CCM ni kuendeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia. “Tutajenga bomba la gesi kilomita 34 kutoka Mtonya hadi Madimba ili kinamama watumie nishati salama na kuondokana na changamoto za kupikia kuni na mkaa,” amebainisha.
Katika sekta ya kilimo, amesema wataendeleza mbolea ya ruzuku, kuongeza wigo wa mazao yanayolimwa na kuanzisha miradi ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji zaidi ya korosho pekee.
Akiwa katika mkutano wa kampeni Tandahimba, mgombea mwenza huyo ameahidi utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa visima vitano ili kuwawezesha wakulima kupata maji ya uhakika na kuendelea kutoa ruzuku ya mbegu na mbolea kwa wakati.
Aidha, amesema huduma za chanjo na tiba kwa mifugo zitaendelea kutolewa kwa ruzuku, huku akibainisha kuwa katika eneo hilo hakuwapo machinjio ya kisasa, hivyo Serikali ya CCM imepanga kujenga machinjio matatu kwa ajili ya kukuza sekta ya mifugo na biashara ya nyama.