Mgombea mwenza CCM aahidi watajenga meli kubwa ya mizigo Mtwara – Comoro

Mtwara. Mgombea mwenza wa urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameahidi miradi mikubwa minne ya maendeleo mkoani Mtwara, ikiwamo ya ujenzi wa meli kubwa ya mizigo itakayokuwa ikisafirisha bidhaa kuelekea nchini Comoro.

Ahadi nyingine ni kuboreshwa kwa uwanja wa ndege wa Mtwara kwa kujengwa majengo ya kisasa ya abiria, jengo la zimamoto na mnara wa taa, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa shughuli za usafiri wa anga mkoani humo.

Vilevile, Dk Nchimbi ameahidi kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi kwa kujengwa mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Ruvuma pamoja na ujenzi wa bomba la gesi lenye urefu wa kilomita 34 kutoka Mtonya hadi Madimba.

Ametoa ahadi hizo leo Alhamisi Oktoba 2, 2025, katika mikutano ya kampeni iliyofanyika kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Nanguruwe (Jimbo la Mtwara Vijijini), Nanyamba na kwenye Uwanja wa Mpira wa Kassim Majaliwa (Jimbo la Tandahimba).

Mtwara ni mkoa wa 16 kufikiwa na Dk Nchimbi tangu aanze kampeni zake Agosti 29, 2025 mkoani Mwanza, akiinadi ilani ya uchaguzi mkuu ya CCM sambamba na kumuombea kura mgombea urais chama hicho, Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani.

Tayari ameshafanya kampeni katika mikoa ya Mara, Simiyu, Shinyanga, Geita, Kagera, Rukwa, Katavi, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Ruvuma, Njombe, Iringa na Dar es Salaam.

Kwa upande wake, mgombea urais wa CCM, Samia ameshafanya kampeni katika mikoa 20 ambayo ni Morogoro, Dodoma, Songwe, Njombe, Mbeya, Iringa, Singida, Tabora, Kigoma, Pemba Kusini, Unguja Kaskazini, Unguja Kusini, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Pwani, Tanga, Kilimanjaro na kwa sasa akiendelea na kampeni mkoani Arusha.

Kampeni za uchaguzi mkuu zilizoanza Agosti 28 mwaka huu, zinatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 28, siku moja kabla ya kupiga kura kwa wananchi kote nchini.

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), jumla ya wapiga kura milioni 37.6 wamejiandikisha kwenye Daftari la Kudumu na ndio watakaowachagua madiwani, wabunge na Rais.

Katika mikutano yake ya kampeni mkoani Mtwara, mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, Dk Nchimbi, ameahidi miradi kadhaa mikubwa ya maendeleo, huku akisisitiza dhamira ya chama hicho kuendeleza kasi ya utekelezaji wa ahadi kwa miaka mitano ijayo.

Amesema zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa Mtwara wanajihusisha na kilimo, lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa masoko ya uhakika.

“Wakulima wanazalisha mazao mengi lakini wanashindwa kuyauza yote. Tutajenga meli kubwa ya mizigo itakayokuwa ikipeleka bidhaa zetu Comoro,” ameahidi Dk Nchimbi.

Aidha, ameahidi kuboresha uwanja wa ndege wa Mtwara kwa kujenga majengo ya kisasa ya abiria, jengo la zimamoto na mnara wa taa ili kuongeza hadhi na ufanisi wa kiwanja hicho.

Kuhusu changamoto ya maji, Dk Nchimbi amesema Serikali ya CCM itaanzisha mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Ruvuma, akisisitiza kuwa haiwezekani mkoa wenye mto huo mkubwa ukakosa huduma ya uhakika ya maji safi.

“Kazi kubwa imefanyika, lakini bado ipo ya kufanya. Tutaanzisha mradi mkubwa wa Mto Ruvuma kuhakikisha maji yanawafikia wananchi hadi vitongoji,” amesema.

Vilevile, amesisitiza dhamira ya mgombea urais huyo ni kuendeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Tutajenga bomba la gesi kilomita 34 kutoka Mtonya hadi Madimba ili kina mama waweze kutumia nishati salama na kuondokana na changamoto za kupikia kwa kutumia kuni na mkaa,” amebainisha.

Katika sekta ya kilimo, amesema Serikali itaendeleza mbolea ya ruzuku, kuongeza wigo wa mazao yanayolimwa na kuanzisha miradi ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji zaidi ya korosho pekee.

“Tutaboresha kilimo kwa kitaalamu zaidi. Tutawaongeza maofisa wa kilimo na kuwapatia vitendea kazi vya kisasa,” amesema.

Mbali na hayo, Dk Nchimbi ameahidi ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari, zahanati, vituo vya afya, pamoja na barabara zinazopitika wakati wote.

“Kuna chama kingine kinaweza kuahidi miradi hii? Nani kama Samia? Tunawaomba mjitokeze kwa wingi kumpa kura ili aendelee kutuongoza,” amesema.

Katika mikutano hiyo, viongozi wa CCM wamekuwa wakinadi pia mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka mitano iliyopita katika sekta za afya, elimu, kilimo, ufugaji, utalii, barabara, madaraja na usafiri wa majini na anga, wakisisitiza dhamira ya kuendeleza jitihada hizo.

Akiwa katika mkutano wa kampeni Tandahimba, mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, Dk Nchimbi ameahidi kutekelezwa kwa miradi kadhaa ikiwamo ujenzi wa visima vitano ili kuwawezesha wakulima kupata maji ya uhakika, sambamba na kuendelea kutoa ruzuku ya mbegu na mbolea kwa wakati.

Aidha, amesema huduma za chanjo na tiba kwa mifugo zitaendelea kutolewa kwa ruzuku huku akibainisha kuwa katika eneo hilo hakuwapo na machinjio ya kisasa, hivyo Serikali ya CCM imepanga kujenga machinjio matatu kwa ajili ya kukuza sekta ya mifugo na biashara ya nyama.
Kabla ya hotuba ya Dk Nchimbi, wagombea ubunge na madiwani walipata nafasi kueleza mafanikio na changamoto katika majimbo yao.

Mgombea ubunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota, amesema mwaka 2020 hakukuwapo hata kituo cha afya, lakini kwa sasa vipo vituo vitano. Aidha, alisema kuwa katika kata 17 kulikuwapo shule sita pekee, lakini sasa kila kata inayo shule yake.

Chikota ambaye anawania tena nafasi hiyo, ametaja miradi mikubwa mitatu ya kimkakati inayotekelezwa jimboni humo kuwa ni ujenzi wa kituo cha mabasi, soko jipya na barabara za mjini Nanyamba.

“Tukikamilisha miradi hii, maisha ya wananchi wetu yatabadilika. Tunasisitiza mkandarasi amalize kazi kwa wakati na tunawahakikishia kura nyingi ifikapo Oktoba 20,” amesema.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Tandahimba, Ahamed Katani amesema jimbo hilo kwa sasa lina shule tano za kidato cha tano na sita zenye mabweni, ikilinganishwa na moja pekee iliyokuwapo mwaka 2020.

Amesisitiza kuwa kwa miaka mitano ijayo, jimbo hilo linatarajia kupata maendeleo zaidi kwa kujengwa uwanja mpya wa michezo, stendi ya kisasa na soko jipya.

“Nafikiri hata Simba na Yanga watakuja kucheza hapa. Sasa tunakwenda ‘kumbambagija’ kura kwa Mama Samia, wabunge na madiwani,” amesema Katani, akifafanua kuwa neno hilo linamaanisha kujitokeza kwa wingi kujaza kura kwa wagombea wa CCM.