Watoto Watatu wa familia moja Wafariki kwa Moto Kibaha, Chanzo Chaendelea Kuchunguzwa

Na Mwamvua Mwinyi, Pwani Oktoba 2, 2025

Watoto watatu wa familia moja, wamefariki dunia baada ya moto mkubwa kuteketeza sehemu ya juu ya nyumba ya ghorofa iliyopo mtaa wa Kitende kwa Mfipa, Kibaha, mkoani Pwani.

Tukio hilo limetokea Oktoba 1, 2025 majira ya saa 10 alasiri, katika nyumba inayomilikiwa na Marey John Balele. 

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, kabla ya moto huo kuanza, walisikia mlipuko mkubwa, kisha sauti za watoto zikiita bibi yao wakiomba msaada wakieleza kuwa kuna moto. 

Dakika chache baadaye, sehemu ya juu ya jengo hilo lilianza kuteketea kwa moto mkali, uliosababisha vifo vya watoto hao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kuwataja watoto waliofariki kuwa ni Gracious Kadinas (miaka 3), Gabriela Kadinas (mwaka 1), na Adriela Siprian (miaka 4).

Morcase ameeleza, uchunguzi wa tukio unaendelea kwa ushirikiano wa Jeshi la Polisi, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kubaini chanzo halisi cha moto huo.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa uchunguzi wa kitabibu.

Kadhalika, Morcase alitoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha usalama wa watoto majumbani muda wote, ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.