Maswali saba kusuasua usafiri mwendokasi Dar

Dar es Salaam. Ikiwa kuna jambo linaloshangaza jijini Dar es Salaam, basi ni wingi wa watu wanaohitaji huduma za usafiri kila siku. Lakini kilicho zaidi ya mshangao huo ni yanayoendelea katika mradi wa mabasi mwendokasi, ambao ulikuwa ukitarajiwa kuwa suluhisho la tatizo la msongamano wa magari.

Mradi huo ulioanzishwa mwaka 2016, ukiibuliwa kama tiba ya changamoto za usafiri jijini, leo hii umebaki kuwa biashara yenye wateja wengi lakini isiyoimarika.

Badala ya kufanikisha ndoto za kuwa mwarobaini wa usafiri, umekuwa miongoni mwa miradi inayolalamikiwa zaidi na kuacha maswali lukuki kwa wananchi.


Uhaba wa mabasi umesababisha foleni kubwa vituoni, huku abiria wakilazimika kubanana ndani ya mabasi hadi kupitia madirishani.

Baadhi ya video na picha zilizovuma mitandaoni zimeonyesha abiria wakiketi madirishani kwa kukosa nafasi ndani ya mabasi ishara ya hali tete ya mradi huo.

Changamoto hizo zimewafanya baadhi ya wananchi kukata tamaa na hata kuamsha vurugu.

Oktoba 1, 2025, vilijitokeza vitendo vya baada ya wananchi kushambulia kwa mawe mabasi mawili na vituo vya huduma, na kusababisha uharibifu wa vioo.

 Jeshi la Polisi limesema watu watatu wamekamatwa kwa uharibifu huo.

Kwa mtazamo wa wachambuzi na wananchi, hali hii inazua maswali mengi kuliko majibu: Je, mradi huu wa mabilioni ya shilingi umeshindwa kufanikisha malengo yake? Na suluhisho la kweli kwa usafiri wa Dar es Salaam lipo wapi? Na hata mifumo ya malipo inashangaza.

Mradi ulipozinduliwa mwaka 2016, aliyekuwa Mkurugenzi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Donald Rwakatare alisema wameanza na mabasi 104, idadi iliyokuwa chini ya yaliyopangwa 305.


Hata hivyo, Dart iliwahi kuweka wazi kuwa, uamuzi wake wa kuanza kutoa huduma licha ya kutokuwa na mabasi kama ilivyopaswa, ulitokana na kulinda barabara zake ambazo tayari zilishaanza kutumiwa na waendesha bodaboda.

Ingawa mradi ulianza kwa mguu wa kushoto, angalau barabara zilijaa magari mapya na ilitoa matumaini ya kubadili sura ya usafiri.

Lakini sasa, hali ni tofauti, wananchi wanabaki kujiuliza ni mabasi mangapi bado yapo barabarani na kwa nini idadi inapungua badala ya kuongezeka.

Kinachoshangaza ni idadi ya abiria kuongezeka, lakini mabasi yanazidi kupungua bila suluhisho.

Nini kinaendelea kuhusu e-ticket?

Wakati mfumo ulipoanza, MaxMalipo walijitokeza na suluhisho la tiketi za kielektroniki. Baadaye mfumo ukaondoka, kisha ukarudi kivingine, ukiwa na changamoto nyingi.

Mara mifumo inakwama, mara tiketi hazisomeki na mara abiria hulipa kwa fedha taslimu na kupewa teketi za karatasi. Hali hii inaibua maswali kuwa, tatizo ni teknolojia, usimamizi au kuna masilahi yanayogongana nyuma ya pazia?

Nini kilibadilika kutoka Udart ya Simon Group na hii ya sasa?

Wakati fulani, Kampuni ya Udart ilikuwa chini ya Robert Kisena ambaye ndiye aliyekuwa mtoa huduma na aliyeleta mabasi ya awali.

Zilitokea sintofahamu kadhaa, hadi mamlaka za kijinai zikatumika na sasa Kisena yuko jela. Baadaye, Serikali ikachukua usukani. Je, nini kilisababisha mabadiliko hayo?

Je, kulikuwa na mapungufu katika usimamizi binafsi, au ni Serikali iliyohitaji kurejesha udhibiti wa moja kwa moja?

Mradi umezaa nini hadi sasa?

Swali jingine kubwa ni je, katika miaka yote tangu kuanzishwa kwake, mradi huu umezaa nini? Je, mabasi yameongezeka kadri idadi ya abiria inavyoongezeka? Au ni ahadi nyingi kuliko vitendo?

Ikiwa abiria wanapoteza muda mrefu wakisubiri basi moja kati ya mamia yaliyoahidiwa,  kuna namna mradi huo unazalisha matunda yanayoonekana kufidia hali hiyo?

Kubadili watendaji kuna siri gani?

Katika kipindi cha miaka tisa ya mradi, wamepita watendaji wengi katika mradi, akiwemo Ronald Rwakatare, Edwin Mhede, Athuman Kihamia na sasa ameingia Said Tunda. Kama ilivyo kwa Dart vivyo hivyo kwa Udart.

Ubadilishaji uongozi wa Udart pia unazua maswali magumu. Je, mabadiliko hayo ya mara kwa mara yanamaanisha tatizo ni watu waliokabidhiwa majukumu au mfumo mzima wa uendeshaji?

Ahadi za mabasi zisizoisha

Kuna pia kumbukumbu za ahadi za mabasi mapya ambazo mara nyingi zimebaki kwenye makaratasi. Mfano yale mabasi 72 yaliyoka bandarini kwa muda mrefu bila kuingia barabarani n ahata mengine yaliyoahidiwa baada ya hapo nayo yanazua maswali, kwamba kasoro kwenye upangaji, au kulikuwa na masilahi yanayokinzana ndani ya mipango?

Kuazima mabasi ya Mofart suluhisho?

Leo Oktoba 2, mwaka huu, baadhi ya mabasi yaliyopangwa kwa ajili ya kutoa huduma katika awamu ya pili ya mradi huo, yanayomilikiwa na kampuni ya Mofat, yameanza kutumika katika Barabara ya Morogoro.

Yameanza kutumika kutuliza kilio na hasira za wananchi, hata kabla ya uzinduzi wake katika Barabara ya Kikwa uliahirishwa mara kadhaa bila sababu za kina kuelezwa.

Swwali linaloibuka, ni je, hatua hiyo ni suluhu ya kudumu kwa changamoto ni kitulizo cha muda tu?

Maswali haya na mengine yanaibua mjadala miongoni mwa wadau waliozungumza na Mwananchi, akiwemo Oscar Mkude, mtaalamu wa uchumi anayesema kuchukua mabasi ya njia nyingine kupeleka kwengine si suluhisho la tatizo, bali ni kuzima moto kwa muda mfupi.

“Turudi kwenye lengo la mradi wenyewe ni kuwa na mwekezaji mwenye uzoefu na anayeweza kuleta mabasi ya kutosha. Changamoto iliyopo sasa inaonekana kwa sababu hakuna mabasi yaliyoongezeka tangu mradi umeanza,” amesema.

Mchumi huyo amehoji mabasi hayo ya kuazima yatafanya kazi hadi lini njia ya Kimara? na Mbagala kutapelekwa mabasi gani na kwa wakati gani?

Mkude amesema Udart walichukua mradi wa mwendokasi kwa muda, ili baada ya uwekezaji kupatikana aendelee na mradi huo, lakini yalitokea mabadiliko ambayo yaliifanya Udart iendelee kushikilia mradi huo na wakati huohuo hakuna mabadiliko yaliyoonekana.

Baada ya Udart kuendelea kushikilia mradi huo bila kuongeza mabasi huku ikitegemea Serikali inunue mabasi mapya, ndipo anguko la mradi huo lilipoanza.

Mtaalamu mwingine, Dk Paul Loisulie, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) amesema siasa inapaswa isiwepo kwenye mambo yanayohitaji utaalamu.

“Kama kuna mkono wa wanasiasa kwenye mradi huu wanapaswa kweli wauondoe, lakini pia tuangalie vikwazo vilivyopo kwenye mradi huu ili kuwepo uwajibikaji. Kama ni vikwazo vya kimkataba au kimfumo viondolewe ili tuwe na uwajibikaji,” amesema.

Dk Loisulie amesema ni jambo la ajabu kushindwa kusimamia mradi wenye wateja, akisisitiza njia rahisi ya kufanya mradi huo uwe endelevu ni watu kuwajibika.

Kupitia mtandao wake wa X, Waziri wa zamani wa Ardhi, Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka amehoji kulikoni mradi huo uliokuwa matumaini kugeuka kero.

“BRT, Mradi wa mwendokasi Dar es Salaam? Kulikoni kugeuka kero kubwa badala ya ukombozi? Tutambue usafiri wa umma si biashara ya faida ni huduma.

Mtalaamu huyo makazi na mipango miji, ameongeza: “Ulaya serikali hutoa ruzuku (kuendesha mradi), Asia waendeshaji makini hufidia kwa umiliki majengo karibu na vituo, ukiuacha (mradi) ujifadhili wenyewe, ati sijui kuna mwekezaji, ni vigumu kufanikiwa.

“Tuutafakari upya, misingi yake inajulikana ili mradi izingatiwe,” ameandika Profesa Tibaijuka kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Wakati wachambuzi wakieleza hayo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefanya ziara na kujibu baadhi ya maswali kwa njia ya maelekezo.

Ameagiza idadi ya mabasi isipunguzwe katika ruti za kila siku za usafiri huo wa umma katika njia hizo, bila kujali muda gani abiria ni wengi au wachache.


“Hata kama abiria ni wanne, wapande basi waondoke, mabasi yasipunguzwe eti kwa madai mchana si muda wa abiria, muda wote mabasi yasipungue,” amesema Majaliwa alipokagua uingizwaji wa mabasi mapya katika njia ya Kivukoni-Kimara.

Akizungumza na abiria katika ziara hiyo, Majaliwa amesema Serikali imeshughulikia changamoto ya uhaba wa mabasi katika njia hiyo kwa kuongeza mabasi mapya 60 kuanzia leo Oktoba 2, 2025.

“Haya yataongeza idadi ya mabasi kufikia 90, ambayo yatamaliza changamoto  iliyokuwepo.

Amesema kwenye njia hiyo hadi leo asubuhi, Oktoba 2, kulikuwa na mabasi 30 tu ya zamani.

“Njia hii ilikuwa na mabasi 140, lakini hadi leo yalikuwa yamebaki mabasi 30 (ya bluu),” amesema Majaliwa.

Awali, Mkurugenzi wa Udart Waziri Kindamba kabla taarifa ya kutenguliwa kwake, amesema mabasi mengi yaliharibika kwa kuwa muda wake wa kuishi uliisha. Yalitakiwa ndani ya miaka minane hadi tisa yafanyiwe ukarabati mkubwa, au kununua mapya mambo ambayo yote hayakufanyika.

“Vilevile kati yake, magari 60 hadi 70 yalipata hekaheka ya kuingiliwa na mafuriko, na matengenezo yaliyofanyika hayakuwa sahihi, pamoja na nauli kuwa chini ya soko, mambo haya haya yakafanya kampuni kudidimia siku hadi siku,” amesema.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Oktoba 2, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka, imeeleza kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Said Tunda kuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart).


Tunda anachukua nafasi ya Dk Athumani Kihamia ambaye uteuzi wake umetenguliwa kuanzia leo Oktoba 2, 2025.

Pia, Rais Samia amemteua Pius Ng’ingo kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), akichukua nafasi ya Waziri Kindamba, ambaye uteuzi wake pia umetenguliwa.

Rais Samia amemteua David Kafulila kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Dart, huku Dk Ramadhan Dau akiteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Udart.

Waziri Mkuu pia amegusia mabadiliko hayo yaliyofanywa na na Rais Samia, akibainisha kwamba anaamini viongozi wapya watafanya mabadiliko ikiwamo ya njia ya utozaji wa nauli kuwa wa kielektroniki ambayo itapunguza mianya ya watendaji wasiowaaminifu kupokea fedha kwa mikono.

Imeandikwa na Imani Makongoro na Baraka Loshilaa.