HUSSEIN ALI MWINYI: Kuijaza Zanzibar shule za ghorofa na neema ya ajira

Dar es Salaam. Rais akiwa madarakani anapoomba kuchaguliwa muhula wa pili, anachopaswa kwanza ni kueleza aliyoyafanya, kisha aahidi yajayo endapo atachaguliwa. Hivyo ndivyo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, anavyofanya.

Mwinyi, mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), anatambia mafanikio ya miaka yake mitano madarakani kama sehemu ya kuwaambia Wazanzibari kuwa anaaminika, na anapoahidi hutekeleza.

Mafanikio ya miundombinu, kwa ujenzi wa barabara za kisasa mpaka madaraja ya kupitisha magari juu, ni eneo linalompambanua Mwinyi kwa ufahari mkubwa.

Si uongo, eneo la miundombinu, Mwinyi amefanya kazi kubwa Zanzibar.

Ujenzi wa hospitali na shule, ni eneo lingine ambalo Mwinyi analisemea kwa kujiamini, kwa sababu amefanikiwa.

Msisitizo wake ni kuwa kila ambacho alikihiahidi na chama chake, CCM, amekitekeleza, kwa hiyo anaomba miaka mingine mitano afanye mambo makubwa zaidi.

Mwinyi anasema miaka yake mitano ofisini, amejenga shule nyingi za ghorofa. Hivyo, miaka mitano mingine, atatumia kuijaza Zanzibar kwa shule za ghrofa.

Ahadi ya Mwinyi ni kujenga shule 29 za ghorofa katika muhula wake wa pili endapo Wazanzibari watamchagua.

Ujenzi wa viwanja vya michezo, unampambanua Mwinyi kwa utekelezaji. Mwonekano bora wa viwanja vya Amaan, Unguja na Gombani, Chakechake Pemba, ni kete anayotembea nayo anapoahidi yajayo endapo atachaguliwa.

Viwanja vya Amaan na Gombani, vimefanyiwa ukarabari mkubwa, vimekuwa na mwonekano wa kisasa. Kazi kubwa imefanywa na Dk Mwinyi. Bila shaka, Wazanzibari wapenda michezo na Watanzania kwa jumla, wana jambo la faraja kuhusu Dk Mwinyi.

Angalau uchaguzi mkuu 2025 Zanzibar ni mchuano wa ajenda. Uchaguzi Mkuu 2020 Zanzibar 2020 uliibuliwa msemo wa “royal families” kwa maana ya koo za kifalme. Zanzibar si dola ya kifalme na usultani uliondoshwa na Mapinduzi ya Zanzibar tangu Januari 12, 1964.

Royal families ni msemo uliotumika kipindi hiki cha mchakato ndani ya CCM kumpata mgombea urais kama kielezi cha familia za waliopata kuwa viongozi wa Zanzibar, watoto wao kujirudia kuongoza kwa kurithishwa kama vile tawala za kifalme.

Rais wa Kwanza wa Zanzibar ni Abed Aman Karume, mwanaye Aman Abed Karume akawa Rais wa sita wa visiwa hivyo.

 Yupo mtoto mwingine wa Karume, Ali Abed Karume, aliyeusaka urais mwaka 2020. Hii ni familia inayotetwa kuwa ni royal family.

Dk Mwinyi, ni mtoto wa Rais wa Tatu wa Zanzibar, Ali Hassan Mwinyi, ambaye pia ni Rais wa Pili, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Uamuzi wa Dk Mwinyi kuomba uteuzi CCM ili awe mgombea urais Zanzibar kwenye uchaguzi mkuu 2020, ni sababu familia yake kutetwa ikiitwa nayo ni koo ya kifalme.

Ukiachana na hoja ya royal family, ukweli ni kuwa Dk Mwinyi ni kati ya viongozi waliodumu serikalini na katika nafasi ya uwaziri, kwa muda mrefu bila kashfa wala misukosuko.

Na kama kuna swali,  kwa nini alikuwa akidumu sana Wizara ya Ulinzi? Jibu alilitoa Rais wa Tano, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli.

Rais Magufuli alipokuwa anamwapisha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, Januari 27, 2020, alimtaka kumuiga Hussein kwa sababu anajua jinsi ya kuongoza majeshi.

Rais Magufuli alisema, vyombo vya ulinzi na usalama vina namna yake ya kuviongoza, na kwa sababu ya Dk Mwinyi kujua vizuri uongozi wa majeshi, ndio maana alidumu sana Wizara ya Ulinzi. Hiyo ni kutambua ubora wa Dk Mwinyi hata kabla hajawa Rais wa Zanzibar.

Na kwa historia, kabla ya kuwa Rais wa Zanzibar, Dk Mwinyi alihudumia wizara tatu tu kipindi chote cha kuwamo kwenye Serikali za marais watatu. Mwaka 2000 mpaka 2005, aliteuliwa na Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa kuwa naibu waziri wa afya.

Miaka 10 ya Rais Jakaya Kikwete, Hussein alihudumia wizara tatu; Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano kwa miaka miwili, kisha Ulinzi na Afya kwa vipindi tofauti vya miaka nane.

Na Rais Magufuli tangu alimpomteua kuwa Waziri wa Ulinzi Desemba 2015, hakumwondoa, hadi alipogombea urais wa Zanzibar mwaka 2020.

Zipo taarifa kuwa wanajeshi walimpenda sana Dk Mwinyi kwa sababu ni kiongozi mwelewa. Ndani ya Wizara ya Ulinzi, alishapitia nyakati ngumu na kuvuka.

Milipuko ya mabomu, ghala kuu la silaha za kijeshi, Gongo la Mboto na Kambi ya Kizuiani, Mbagala, Dar es Salaam, ni matukio yaliyotokea Dk Mwinyi akiwa Waziri wa Ulinzi, na kukawa na presha ya kutaka awajibike kwa kujiuzulu, lakini alivuka salama.

Inawezekana pia ni mwenye bahati, maana hupishana na mitikisiko ya wizara. Mwaka 2012, wakati aliyekuwa Waziri wa Afya, Haji Mponda, alipoondolewa pamoja na naibu wake, Lucy Nkya, kwa kushindwa kuwajibika, Dk Mwinyi  alikuwa Waziri wa Ulinzi.

Na mwaka 2013, kipindi cha aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Majeshi ya Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, alipoondolewa kwa sababu ya kashfa ya wanajeshi kutesa raia katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, Dk Mwinyi  alikuwa Waziri wa Afya.

Na mara zote, Mponda alipoondolewa Wizara ya Afya, Dk Mwinyi aliondolewa Ulinzi kwenda Afya, kisha Nahodha alipowajibika Ulinzi mwaka 2013, Dk Mwinyi alipelekwa Ulinzi kutokea Afya.

Si dhambi kukiri kuwa kama sio bahati, basi Dk Mwinyi ni kiongozi mzuri, ndio maana madudu hayatokei, yeye akiwa waziri, kama utaacha lile la mabomu kulipuka Gongo la Mboto na Mbagala, ambalo halikuwa kosa lake la moja kwa moja.

Alizaliwa Desemba 23, 1966. Elimu ya msingi na sekondari alisoma Dar es Salaam, Tanzania na Misri. Msingi alianzia Shule ya Oysterbay, Dar es Salaam, aliposoma miaka mitatu kuanzia mwaka 1974 mpaka 1977, kisha akamalizia Shule ya Minor House Junior, iliyopo Misri mwaka 1974 hadi 1980.

Mwinyi alianzia Shule ya Sekondari Minor House, Misri, mwaka 1981 mpaka 1982. Alirejea Tanzania kuendelea na kidato cha pili Shule ya Sekondari Azania, Dar es Salaam mwaka 1982 na alimaliza kidato cha nne Azania.

Kidato cha tano na sita, alisoma Shule ya Sekondari Tambaza, Dar es Salaam alikohitimu mwaka 1986.

Dk Mwinyi alisoma shahada yake ya kwanza ya udaktari wa binadamu Chuo Kikuu cha Marmara, Uturuki, kuanzia mwaka 1986 mpaka 1992.

Mwaka 1993 mpaka 1997, Dk Mwinyi alisoma shahada ya uzamili ya Utabibu wa Kimataifa, Chuo Kikuu cha Hammersmith Hospital, London, Uingereza.

Huyo ndiye Dk Mwinyi ambaye mwaka 2000 alikuwa mbunge wa Mkuranga, Pwani (CCM) na kuanzia mwaka 2005 mpaka 2020, alikuwa mbunge wa Kwahani, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Na sasa ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, akiomba kuchaguliwa kwa muhula wa pili.

Kwa haiba, Mwinyi si mtu wa malumbano. Tangu akiwa waziri, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hadi Rais wa Zanzibar, ni muhali kumwona akilumbana na wanasiasa.

 Ni mkimya na muda mwingi akijielekeza kufanya kazi zake bila kelele. Oktoba 29, 2025, uamuzi wa Wazanzibari utakuwa jibu la jinsi wanavyomwelewa Dk Mwinyi na uongozi wake.