Siri iliyojificha utemaji wa mate

Wakati wengi huona aibu au huchukulia kutema mate kama jambo dogo lisilo na maana, wataalamu wa afya wanasema tabia hiyo ina faida nyingi kwa mwili, hasa pale mate yanapochanganyika na makohozi au uchafu kutoka kooni na kwenye mapafu.

Mate ni majimaji ya asili yanayozalishwa na tezi za mate zilizopo mdomoni. Majimaji haya yana mchanganyiko wa maji, vimeng’enya (enzymes), protini, madini, na kemikali nyingine muhimu zinazosaidia katika kazi mbalimbali za mwili.

Daktari wa afya ya jamii, Dk Ayoubu Msalilwa, anasema mate husaidia kusafisha koo na mdomo. Hivyo, yanapokuwa mazito au yamechanganyika na makohozi, ni vyema kutema badala ya kumeza.

“Unapotema, unaondoa bakteria, virusi na uchafu ambao vinginevyo unaweza kuendelea kusababisha maambukizi mwilini,” anasema.

Kwa mujibu wa Dk Ayoubu, kutema mate huondoa vimelea na sumu. Anasema kwa mfano, mate yenye makohozi yakitemwa, hupunguza hatari ya kuendeleza maambukizi mwilini na hulinda tumbo dhidi ya kuingiza uchafu.

Daktari huyo ambaye pia ni bingwa wa afya ya mama na mtoto, anaongeza kuwa kutema mate husaidia mapafu na koo kuwa huru, hupunguza kubanwa, na pia huchangia katika usafi wa mdomo kwa kuwa hupunguza harufu mbaya.

“Kwa mtu wa kawaida, ikitokea umepata changamoto yoyote ya kiafya au dalili za mafua, ukijisikia kutema mate, yale yanayotoka mazito au mepesi yanakuwa na maana. Yakiwa mazito, unaweza kutema vimelea kama bakteria au virusi. Ukiyatema utakuta yana rangi ya njano; hii inaonyesha kuwa mwili unajaribu kuyasukuma ili kupunguza kiwango chake,” anafafanua.

Anaongeza: “Kwa mfano, ukipata mafua mwili huwa unazuia uchafu usiingie kwenye koo la hewa kupitia vinyweleo vidogo vinavyoitwa ‘cilia’ vinavyosukuma matemate na makohozi kutoka kwenye mapafu.”

Aidha, anasema mate ambayo yanatemwa kwa sababu ya kuwa na harufu au rangi isiyo ya kawaida, yanaweza kusaidia madaktari kutambua chanzo cha tatizo la kiafya.

“Kwa mfano, ukimwambia daktari umetema mate yenye damu, hilo linaweza kumsaidia kujua kama una tatizo kwenye mapafu au unaugua kifua kikuu. Kama yanavutika, inaweza kumjulisha daktari kuwa kuna changamoto kwenye mfumo wa mmeng’enyo wa chakula,” anasema.

Kwa wanawake wajawazito, Dk Ayoubu anasema hali ya kuvutika kwa mate inaweza kuwa ishara ya mabadiliko ya homoni wakati wa ujauzito.

Pia anashauri kuwa mtu anayejisikia kutema mate wakati wa kuumwa, asiyazuie kwani inaweza kuwa ni ishara kuwa kinga ya mwili inafanya kazi kwa kasi zaidi, hali inayosababisha wengine kujisikia kichefuchefu.

Utafiti wa mwaka 2024 uliofanywa na watafiti wawili kutoka Chuo Kikuu cha Kyushu na Hiroshima nchini Japani, ulionesha kuwa mate hufanya kazi ya kusafisha kinywa kiasili.

Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Cancers, ulionyesha kuwa mate sio kioevu cha kawaida tu bali pia ni chombo chenye nguvu chenye vimeng’enya (enzymes) vinavyovunja wanga na mafuta, hivyo kuongeza uwezo wa mmeng’enyo wa chakula.

Aidha, mate husaidia kudumisha uwiano wa bakteria wazuri na wabaya kinywani na hivyo kupunguza hatari ya magonjwa ya meno. Watafiti walibainisha kuwa mate yana protini na viashiria vya kinga vinavyosaidia kuponya vidonda vya ndani ya kinywa.

Kwa kushirikiana na tafiti zilizopita, watafiti hao, Okuyama na Yanamoto waligundua kuwa mate yanaweza kutumika kama chombo cha uchunguzi wa magonjwa.

Kupitia uchambuzi wa viashiria vya kibaiolojia (biomarker) vilivyomo kwenye mate, madaktari wanaweza kubaini hali kama saratani ya mdomo, ugonjwa wa moyo, na hata kisukari.

Hii inaonesha kuwa mate si tu huduma ya ndani ya kinywa, bali pia ni dirisha muhimu la afya ya mwili kwa ujumla.

Dk Ayoubu anasema hakuna kiwango maalum cha mtu kutema mate kwa siku. Kwa kawaida, mate safi yanamezwa bila tatizo na ni sehemu ya kinga ya mwili.

Hata hivyo, anasisitiza kuwa pale mtu anapokuwa na mafua, kikohozi au makohozi mengi, ni bora kutema badala ya kumeza.

“Nikiyameza, mwili utayameng’enya kama chakula kingine, lakini kama mate yalikuwa na sumu kama bakteria au virusi, na ukayameza, yanaweza kuingia kwenye damu na kusababisha maambukizi zaidi,” anasema.

Anaongeza kuwa miili yetu huzalisha kati ya nusu lita hadi lita moja na nusu ya mate kwa siku, ambayo humezwa bila matatizo na husaidia kuvunja vyakula, hasa vya wanga, mara tu vinapoingia mdomoni.

Madhara ya kumeza mate machafu

Kwa mujibu wa wataalamu, kumeza makohozi kunaweza kuongeza mzigo wa bakteria tumboni, kuendeleza kero kooni na kuchangia harufu mbaya ya mdomo.

Kwa hiyo, kutema mate si jambo la kudharau, hasa pale yanapokuwa yamechanganyika na makohozi au uchafu mwingine kutoka kwenye mfumo wa upumuaji.

Baadhi ya wakazi wa Jiji la Mwanza wanasema kutema mate ni muhimu kiafya,  lakini wanasisitiza umuhimu wa kufanya hivyo kwa njia ya heshima na kwa kuzingatia usafi wa mazingira.

“Tatizo linapoanzia ni watu kutema mate ovyo bila kujali usafi au afya za wengine waliopo karibu. Hii inaweza kusababisha uchafu wa mazingira, harufu mbaya, na hata maambukizi. Nashauri mtu ateme mate  chooni au sehemu zilizotengwa kwa usafi,” anasema Mapesa Anthony.

Kwa upande wake, Nadia Abbas, anasema si vibaya kutema mate lakini ni muhimu kuzingatia heshima na mahali pa kufanya hivyo.

“Watu wa afya wanapaswa kutoa elimu zaidi kwa jamii. Wengine wanatema mate mazito hadharani bila kujali ustaarabu wala afya ya wengine. Elimu itolewe na ikiwezekana faini zitolewe kwa wanaotema mate ovyo,” anashauri.

Faida zaidi za kutema mate

  • Kupunguza hatari ya maambukizi: Mate yanapokuwa na vimelea, kutema kwa njia sahihi husaidia kuzuia maambukizi kwa watu wengine.
  • Usafi wa mdomo: Mate yaliyochanganyika na uchafu au mabaki ya chakula yanapotemwa, hupunguza harufu mbaya ya mdomo na kusaidia usafi wa kinywa.
  • Kuimarisha kinga ya mwili: Kutema mate husaidia kuondoa sumu na uchafu, hivyo kuuweka mfumo wa kinga katika hali nzuri.
  • Kupunguza kichefuchefu na msukumo wa kutapika: Kwa baadhi ya wagonjwa, kutema mate husaidia kupunguza hali ya kichefuchefu kwani mate hayo huchukuliwa kama kinga ya mwili dhidi ya hali zisizo za kawaida tumboni.

Kutema mate si jambo la aibu. Ni sehemu ya mchakato wa asili wa mwili kujilinda, kujisafisha na kuwasiliana na wataalamu kuhusu hali ya afya.

Hata hivyo, ni muhimu kufuata maadili, heshima na usafi wa mazingira katika utemaji wake.