Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimeahidi kufuta utaratibu wa leseni kwa wavuvi endapo kitapata ridhaa ya wananchi kupitia wagombea wake wa ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa jana, Oktoba 2, 2025 na kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika Kigamboni jijini Dar es Salaam, alipokuwa akinadi mgombea ubunge wa chama hicho katika jimbo hilo, Mwanaisha Mdeme.
Zitto amesema utaratibu wa sasa unaowataka wavuvi kulipia leseni za boti na wasaidizi wao ni kandamizi na wa kibaguzi ikilinganishwa na sekta nyingine, hasa kilimo.
“Mkulima chombo chake cha kazi ni trekta, lakini trekta halina leseni. Mvuvi chombo chake ni boti, tena anatozwa leseni. Tunaposema taifa la wote, maslahi ya wote, maana yake haki iwe kwa wote, kwa mvuvi na mkulima,” amesema Zitto.
Ameongeza kuwa, tofauti na sekta ya usafirishaji ambapo dereva pekee ndiye hulipia leseni, katika uvuvi kila aliye ndani ya boti hulazimika kuwa na leseni, jambo alilosema linaonyesha wavuvi hawana watetezi.

Mwanaisha Mdeme amewataka wananchi wa Kigamboni kumchagua ili akalete sauti yao bungeni na kushughulikia changamoto zinazolikabili jimbo hilo, ikiwemo barabara mbovu na huduma hafifu za kijamii.
“Asubuhi tunapokwenda kwenye shughuli zetu tunashuhudia wanafunzi wakitembea umbali mrefu kwenda shule kwa sababu hakuna mabasi ya abiria kutokana na ubovu wa barabara,” amesema.
Mdeme ameahidi kushirikiana na madiwani wa chama chake kuhakikisha miundombinu na huduma za kijamii zinaboreshwa, sambamba na utetezi wa wavuvi wa Kigamboni na maeneo mengine ya uvuvi nchini.